Uhifadhi endelevu wa wanyamapori unahitaji tafiti za kina za mara kwa mara kwa kutumia mbinu sahihi zilizohakikiwa ili kuleta matokeo halisi yanayosaidia katika kuweka mipango endelevu ya uhifadhi.
Tafiti ni mihimu sana katika uhifadhi wa wanyamapori. Lakini tafiti hizi zinatakiwa kufanyika kwa weledi mkubwa kwa kuzingatia mbinu au njia za kufanya utafiti zilizohakikiwa na kukubaliwa katika ulimwengu wa sayansi na tafiti.
Hata hivyo ni jambo la kawaida katika ulimwengu wa sayansi na tafiti, kukosoana, kupendekeza maoni au kutoa ushauri endapo mbinu mpya au njia nyingine ya utafiti imetumika na kuleta matokeo tofauti na njia za awali zilizowahi kutumika.
Mfano, matokeo ya utafiti wa hivi karibuni tarehe 9/09/2025, uliochapishwa katika jarida la PNAS Nexus kuhusu idadi ya nyumbu wanaopatikana katika mfumo wa ikolojia ya Serengeti Masai- Mara, umeonyesha idadi ya nyumbu katika eneo hilo ni 600,000 badala ya nyumbu zaidi ya milioni 1.3 kama ilivyoripotiwa na tafiti nyingi za awali.
Matokeo ya utafiti huo wa Isla Duporge na wenzake umezua taharuki, mshangao na maswali mengi kwa baadhi ya watafiti na wahifadhi wa wanyamapori sehemu mbali mbali duniani, ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakifanya tafiti za nyumbu katika eneo hilo.
Hata hivyo, TAWIRI hawakukaa kimya kuhusu matokeo ya chapisho hilo la Isla Duporge na wenzake, walitolea ufafanuzi wa kina kuhusu matokeo ya utafiti huo na kutokubaliana na namna ulivyofanyika, njia walizotumia nk.

Picha kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), 2023
Huu ndio ufafanuzi kutoka Taasisi ya Utafiti wa wanyamapori Tanzania (TAWIRI); karibu tuusome ili tufahamu sababu za kukataa matokeo ya chapisho hilo.
UFAFANUZI JUU YA CHAPISHO LA ISLA DUPORGE et al., 2025, KWENYE JARIDA LA PNAS NEXUS KUHUSU IDADI YA NYUMBU KATIKA MFUMO IKOLOJIA WA SERENGETI-MAASAI MARA
Taasisi imelipitia kwa kina chapicho la Isla Duporge na wenzake liliotolewa kwenye jarida la PNAS Nexus (Brief report; https://10.1093/pnasnexus/pgaf264, Advance press publication la tarehe 9 Septemba 2025 na kuja na maoni kama ifuatavyo.
Kwanza itoshe tu kusema kuwa matokeo ya idadi ya nyumbu yaliyotolewa (600,000) siyo sahihi ukilinganisha na idadi ya sensa ya TAWIRI ya nyumbu 1,366,109 (SE231,741) kwa sababu ya mapungufu mengi ya kimethodolojia (methods) kwa maana ya namna (design/ approach) na mbinu (technique) ya namna aina hiyo mpya ya kuhesabu nyumbu (soroveya) ambayo ndio inafanyiwa majaribio na inayofanyika kwa mara ya kwanza kwa idadi kubwa ya wanyamapori kama nyumbu ilivyotekelezwa, ikilinganishwa na methodolojia ya kuhesabu nyumbu ambayo imehakikiwa na imekuwa ikitumika kwa muda mrefu na TAWIRI na pia nchi nyingine (Gold Standard method). Hivyo matokeo yake kamwe hayawezi kulinganishwa na idadi iliyotolewa na TAWIRI kwa miaka mingi.
Mapungufu yaliyobainika ambayo yanafanya idadi hiyo ya nyumbu kuwa siyo sahihi ni kama ifuatavyo;
Mbinu (census method) ya kuhesabu nyumbu inayotumiwa na TAWIRI ni ya kupiga picha kwa kamera za hali ya juu sana kwa kutumia ndege inayoruka kima kifupi [Aerial census, Aerial Point Sampling (APS)] ambayo imetumika kwa muda mrefu na imehakikiwa (validated), wakati mbinu iliyotumiwa na Duporge et al ni ya Akili mnemba/ bandia (Artificial Intelligence (AI) based survey, ya picha za satellite tu.
Njia hii ni mpya, haijahakikiwa (not validated), na ni mara ya kwanza inajaribiwa kuhesabu wanyamapori wengi kama nyumbu na katika mzingira tofauti, na haya ni matokeo yake ya kwanza kutolewa, ambayo yametofautiana sana na mbinu zilizohakikiwa, na yametoa idadi ndogo ya nyumbu ambayo haijawahi kutolewa na haina uhalisia.
TAWIRI hufanya sensa ya nyumbu kipindi cha masika (Februari-Machi), kipindi ambacho kundi zima limekusanyika kwenye maeneo ya mbuga za nyasi fupi (short grassland plains) wakati sensa ya Duporge et al imefanyika kipindi cha kiangazi (August 2022 na 2023) ambapo nyumbu wameshaondoka na wapo kwenye maeneo yenye miti na vichaka na kundi limeshatawanyika maeneo mapana.
Hivyo matokeo ya masika hayawezi kulinganishwa na matokeo ya kiangazi, maana nyumbu wanazunguka hasa kufuata chakula na maji, na huwezi kuwaona hata kutoka angani wakiwa ndani ya miti na vichaka.
TAWIRI hufanya Sensa kipindi ambacho nyumbu wako kwenye nyanda za nyasi fupi (southern Serengeti, northern Ngorongoro and Loliondo plains) ambako nyumbu ni rahisi kuonekana kwene picha zinazopigwa na kamera za ndege, wakati sensa ya Duporge et al imefanyika wakati nyumbu wakiwa wametawanyika katika uwanda wa miti au ‘woodlands’ (northern Serengeti and southern Maasai Mara) nchini Kenya, ambako ni vigumu kuwaona nyumbu wote kwenye picha za satellite kutokana na kufunikwa na miti (‘canopy inteference’), hali ambayo haiwezi kuleta idadi sahihi ya wanyamapori kwa aina zao.
Mbinu inayotumiwa na TAWIRI hutumia picha za kamera zenye uangavu au ‘resolution based on height’ wa 3-5cm ambazo zinauwezo mkubwa wa kuona/ kutambua na kutofautisha nyumbu, wakati Duporge et al ametumia picha za satellite za uangavu wa 33-60cm, ambazo zina uwezo mdogo wa kuona/ kutambua/ kutofautisha nyumbu na wanyamapori aina nyingine na hivyo kutowaona nyumbu wengi. ‘The TAWIRI 3-5cm high resolution images provide greater precision and counts than 33-60cm used by Durpoge et al.’
TAWIRI hufanya sensa ya nyumbu wengi wao wakiwa katika mfumo ikolojia wa Serengeti, na inahesabu upande wa Tanzania tu, wakati Duporge et al soroveya yake imejumuisha Tanzania na Kenya, kipindi ambacho nyumbu wametawanyika kotekote.
TAWIRI hufanya sensa zake wakati wa asubuhi, nyumbu wakiwa wako uwandani na wanakula, na hivyo nyumbu wengi kuonekana, wakati picha za satellite (satellite overpasses) zilizotumika na Duporge et al. zinapigwa mchana, kipindi ambacho nyumbu wengi wanakuwa wamepumzika chini ya miti na vichaka, na hivyo wengine kutoonekana.
Nje na muda wa soroveya au kuchukuliwa kwa picha, picha za satellite vilevile zinaathiriwa sana na mawingu, uoto, nk.
Mwisho, imeonekana kuwa tofauti ya idadi ya nyumbu aliyopata Duporge et al. imetokana na utofauti na uwezo mdogo wa mbinu waliyotumia ya satellite image kuona, kutambua na kuhesabu nyumbu, licha ya kuwa eneo linalotumiwa na TAWIRI kuhesabu nyumbu (kilometa za mraba 4,782) liko karibu sawa na eneo lililotumiwa na Durpoge et al. kwa soroveya yao. Na hivyo njia hiyo mpya na iliyotumika kwa mara ya kwanza kuhesabu nyumbu waliyotumia bado inahitaji utafiti wa kina na maboresho ya muda mrefu kabla ya kuamika na kutoa matokeo sahihi.
Tunahitimisha tena kuwa, matokeo haya ya idadi ya nyumbu (600,000) siyo sahihi kutokana na mapungufu mengi ya kiufundi ya soroveya hiyo ilivyofanyika kama yalivyoainishwa hapo juu. Kwa njia waliyotumia Duporge et al. hawangeweza kupata idadi halisi ya nyumbu. Hivyo matokeo yao hayawezi hata kidogo kutumika kulinganisha na idadi ya nyumbu iliyopatikana kwa kutumia ‘Gold standard method’ ya kuhesabu nyumbu.
Tunawashukuru wote kwa uvumilivu wenu. Wataalamu wa Taasisi na wadau wake wanaendelea kulifanyia kazi jambo hili. Imebidi kutumia maelezo marefu kufafanua maana jambo hili liweze kueleweka vizuri.
AHSANTENI SANA.
DKT. JULIUS D. KEYYU
DIRECTOR OF RESEARCH