Utangulizi
Kuzoesha wanyamapori ni kitendo ambacho kinafanywa kwa kudhamiria au kutokudhamiria ili kuhakikisha kwamba wanyamapori wanakuwa karibu na binadamu. Kitendo hicho kinaweza kufanyika kwa Wanyama na ndege pia. Zipo sababu hasi na chanya za kutengeneza mazoea hayo baina ya wanyamapori na binadamu. Kwa upande wa sababu chanya inaweza kuwa ni shughuli za utalii au uhifadhi na sababu hasi ni wanyamapori kujeruhi binadamu, kusababisha hasara na wakati mwingine kusababisha kuenea kwa magonjwa kutoka kwa wanyamapori Kwenda kwa binadamu yaani kitaalamu zoonotic diseases. Katika Makala hii tutajifunza kwa kina juu ya sababu zinazopeleka wanyamapori na binadamu kuwa na mwingiliano lakini pia nini kifanyike ili kuepuka mazoea haya.
Kitendo hiki cha kuzoesha wanyamapori ni mchakato ambao wanyamapori wanazoea uwepo wa binadamu na hutokea pale ambapo hatua kwa hatua wanyamapori wanakuwa na uvumilivu zaidi na kuwa na muingiliano na binadamu. Baada ya muda wanyamapori wanakuwa hawaogopi tena uwepo wa binadamu. Baadhi ya wanyamapori hao ni Pamoja na tembo, twiga, Nyati, jamii ya nyani, lakini pia na Wanyama wakubwa wanaokula nyama kama vile simba na duma
Picha hii inaonyesha watu wakitembea pamoja na wanyamapori hatari kama tembo bila shida yoyote; chanzo cha picha ni www.thrillist.com
Sababu zinazochangia binadamu kuzoeana na wanyamapori.
1. Uwepo wa mara kwa mara wa binadamu.
Wanyamapori wanaweza kuzoeana na binadamu iwapo watakuwa wanaonana mara kwa mara na binadamu. Mara ya kwanza mnyamapori anapokutana na binadamu atakuwa mkali au ataogopa na kukimbia, lakini baada ya muda kupita akiwa anaonana mara kwa mara na binadamu mnyama huyu hataogopa tena au kukimbia hivyo atabadili tabia ya uoga au ukali na kuruhusu binadamu amsogelee.
2. Utoaji wa chakula.
Hii ni moja ya sababu kubwa inayochangia binadamu kuzoeana na wanyamapori. Sehemu ambapo binadamu wanapatikana na chanzo cha chakula kwa urahisi kinapatikana hivyo wanyama huenda sehemu hiyo ili waweze kupata chakula. Hivyo wanyama hawa hawatawaogopa tena binadamu na huweza kuwafuata na kupatiwa au kuiba chakula. Jamii ya nyani ndio wamekuwa waathirika wakubwa wa sababu hii
Picha ikionyesha mtu akilisha majani twiga, picha hii imetoka katika tovuti ya National geographic.com
3. Tabia za wazazi
Watoto wanaweza kujifunza tabia kutoka kwa wazazi wao. Ikiwa mama au baba yao huenda walipo binadamu na kupata chakula au wakiwa hawana hofu tena na binadamu hata watoto nao watajifunza tabia hiyo kutoka kwa wazazi wao na baadae na wao kuendeleza mazoea na binadamu.
4. Ukaribu na mali za binadamu
Wanyama waishio karibu na mali au rasilimali za binadamu kama mashamba au bustani hubadili tabia zao kwa sababu ya Upatikanaji rahisi wa chakula. Hivyo katika Maisha yao yote, wanyamapori hawa wanakuwa na mazoea na binadamu na kusabisha hasara na usumbufu kwa wamiliki wa mali hizo.
5. Mila na desturi
Katika baadhi ya jamii mila na desturi zao zinaweza sababisha wanyamapori wakabadili tabia zao. Baadhi ya Mila hizo hutoa Mwanya kuwa na mazoea na wanyamapori kwa lengo la kuwalinda au kuwa na Imani kwamba akikutana na aina Fulani ya wanyamapori basi ni baraka kwake. Kitendo cha kuendeea kukutana nao mara kwa mara basi kinatengeneza mazoea na kisha kuwasogelea au kuwapa chakula au kuwaabudu. Kwa kufanya hivyo mara kwa mara huleta ukaribu kati ya mnyamapori na binadamu na baada ya muda mnyama huyu atazoea na kuruhusu binadamu kumsogelea.
Picha hii inaonyesha watu wakicheza na mnyama fisi; imepigwa na Chase Jarvins.I
Athari za mazoea kati ya wanyamapori na binadamu
Mpendwa msomaji hapo juu tumeona sababu za wanyamapori kuzoeana na binadamu na mojawapo ni chakula. sasa twende tukaone madhara ya yanaweza kutokea endapo binadamu ataendelea na mazoea na wanyamapori. Kitendo hiki kina madhara hasi na chanya kwa binadamu, wanyama na mazingiraambazo ni ;
ATHARI CHANYA
1. Fursa za utafiti
Wanyamapori waliozoea binadamu hutoa fursa nzuri kwa watafiti kusoma wanyama hawa kwa ukaribu zaidi na kukusanya takwimu muhimu kuhusu tabia zao na mazingira. Takwimu hizi huweza kuchangia katika maarifa ya kisayansi na juhudi za uhifadhi wa wanyama hawa.
Picha hii imetolewa kwenye tovuti ya study.com, ikionyesha mtafiti huyu Dr. Jane Goodall aliyefanikiwa kujifunza tabia za sokwe baada ya kutengeneza mazoea nao kwa miaka mingi
2. Utalii
Wanyamapori waliozoea binadamu wanaweza kuwa ni kivutio kikubwa cha utalii kwani watalii wengi watakuwa wanakuja ili kuona wanyama hawa kwa ukaribu zaidi. Watalii hawa hulipia fedha ambazo husaidia kuzalisha mapato.
Picha hii ikionyesha watalii wakimshangaa mnyama aina ya chui; picha imetolewa katika tovuti ya African geographic.com
3. Uhusiano rafiki kati ya binadamu na wanyamapori
Kuzoesha wanyamapori kunasaidia sana kuboresha uhusiano na kuondoa imani potofu kuhusu wanyamapori kwani jinsi ambavyo binadamu na wanyamapori wanakuwa na ukaribu ndivyo ambavyo inajengeka akilini kwa binadamu kwamba si kila mnyamapori ni adui au anaweza mdhuru binadamu
Picha hii inaonyesha mahusiano ya karibu kati ya mtu na tembo; picha imetolewa katika tovuti ya national geographic.com
4. Elimu na uelewa
Wanyamapori waliowazoea binadamu wanaweza tumika kama kielelezo cha wanyamapori wengine ili kuweza kuongeza uelewa wa aina mbalimbali za wanyamapori na kuleta hamasa kwa watu mbalimbali kushiriki katika uhifadhi wa wanyamapori hawa.
ATHARI HASI
1. Wanyamapori kutegemea chakula cha binadamu
Wanyamapori waliozoea binadamu huanza kutegemea chakula cha binadamu hivyo kuathiri tabia zao za asili za utafutaji chakula. Hii husababisha lishe duni na matatizo ya kiafya kwa wanyama kwani chakula cha binadamu hakikidhi viwango vya chakula wanavyovipata porini.
Picha hii inaonyesha wanyama jamii ya nyani wakila vyakula vilivyoandaliwa na binadamu; picha imetolewa katika ukurasa wa nationalgeographic.com
2. Inaongeza uwezekano wa uwindaji wa wanyamapori.
Wanyamapori waliozoea binadamu wanaweza kuwa rahisi kuwindwa na wawindaji haramu kwani ni rahisi kuwakamata kwa kuwa huruhusu kusogelewa na binadamu. Hivyo humpa nafasi nzuri muwindaji kumkamata kwa urahisi.
3. Kuongezeka kwa Migogoro baina ya wanyamapori na binadamu
Kuzoeana kunaweza kusababisha migogoro kati ya wanyamapori na binadamu ambapo wanyamapori huvamia katika maeneo ya binadamu kama mashambani au kwenye bustani au makazi ili kutafuta chakula. Hii husababisha migogoro na huleta hofu na chuki pale ambapo wanyamapori wameharibu mazao/mifugo au mali za watu
Picha hii ikionyesha tembo akiwa ameuwawa katika mashamba ya watu; picha imetolewa katika ukurasa wa Careers in conservation.com
4. Hatari kwa afya
Kulisha wanyamapori chakula cha binadamu huleta athari kwa afya ya wanyamapori, kwani vyakula vya binadamu huwekwa viungo mbalimbali ambavyo vinaweza kuathiri afya ya wanyamapori na muda mwingine husabisha vifo vya wanyamapori.
5. Kuenea kwa magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Kutokana na kuwa na ukaribu kati ya binadamu na wanyamapori hii inaweza sababisa kueneza magonjwa ambayo huambukiwa kutoka kwa mnyamapori Kwenda kwa binadamu Mfano wa magonjwa haya ni Ebola,COVID -19, na Kimeta.
5. Uharibifu wa mali za binadamu.
Wanyamapori wanapokuwa wamewazoea binadamu hupenda kutumia vitu vya binadamu na kwakuwa hawana ustaarabu kama alionao binadamu hupelekea kuharibu vitu vya binadamu.
Picha hii ikionyesha wanyama jamii ya nyani wakiwa ndani ya gari; picha imetolewa katika tovuti ya mirror.com
Nini kifanyike ili kupunguza mazoea kati ya binadamu na wanyamapori.
- Binadamu wasikaribie sana wanyamapori ili kuzuia muingiliano utakaosababisha wanyamapori kuwazoea binadamu.
- Epuka kuwapa chakula wanyamapori kwani utoaji wa chakula huweza kusababisha wanyamapori kutegemea zaidi chakula cha binadamu.
- Kufuata miongozo na sheria zilizowekwa na mamlaka ya hifadhi husika kuhusiana na umbali na miongozo mbalimbali ya utalii.
- Watafiti wafanye tafiti zao kwa kukaa sehemu ambazo zimejificha ili kuzuia wanyamapori kuwazoea na kuathiri tabia zao.
HITIMISHO
Muingiliano wa mara kwa mara baina ya wanyamapori na binadamu unaathari kubwa sana kwa wanyamapori, mazingira yao Pamoja na sisi binadamu. Hivyo ni jukumu letu kupunguza athari hizi kwa wanyamapori na mazingira yao ,pia kuilinda asili ya mazingira na spishi mbalimbali zinazopatikana katika ulimwengu huu.
Makala hii imehaririwa na Alphonce Msgwa ambaye ni mwikolojia hifadhi za Taifa TANAPA.Ukiwa na maswali, maoni au mapendekezo kuhusu makala hii usisite kuwasiliana na mwandishi wa makala hii, kwa mawasiliano yake hapo chini.
Monica C. Mahilane
0652267935