Habari ndugu Mtanzania, Karibu tena kwenye makala hizi za blogu yako ya Wildlife Tanznia, ambapo unapata nafasi ya kujua mambo mbali mbali ya hifadhi zetu na pia mambo ya msingi na ufahamu utakaokusaidia kuelewa baadhi majukumu ya hifadhi za Taifa kuweza kushiriki katika uhifadhi wa Wanyamapori na mazingira yao.
Katika kuadhimisha siku ya mazingira duniani, serikali ya Tanzania imetoa ruhusa kwa watanzania kuingia hifadhi za Taifa bure kabisa, Hivyo pamoja na kuingia hifadhini bure baadhi ya Watanzania wengi hawajui sharia na taratibu mbali mbali za hifadhi za Taifa, kwa kuliona hilo nimeamua kuandika mkala hii yenye kuonyesha baadhi ya sharia na taratibu muhimu sana kuzizingatia unapotembelea hifadhi yoyote ya Taifa. Hivyo nikukaribishe uungane nami kwenye kuangalia na kujifunza sharia na taratibu hizi za hifadhi.
- Usisumbue Wanyama
Unapotembelea hifadhi yoyote ile ya Wanyama, jihadhari usiwasubue Wanyama kwa namna yoyote ile, kwa kuwaita, kupiga honi za magari au filimbi, au kuwapiga kwa mawe, au kupiga kelele uwapo hifadhini, au kuacha barabara kuu uliyopitia (kuchepuka); mambo hayo hayaruhusiwi na kabisa na hifadhi yoyote ya Taifa na utachukuliwa hatua kali na utatozwa faini au adhabu kubwa. Hivyo mtanzania mwenzangu zingatia hayo niliyokushauri ili ufurahiye safari yako.
- Usiwalishe chakula Wanyama
Hapa napo ni mahali pa kuangalia kwa makini unapotembele hifadhi yoyote duniani, nimarufuku kabisa kuwalisha Wanyamapori chakula au kitu chochote ulichokuja nacho. Najua unaweza kuwa na furaha sana, au kuwapenda sana wanyamapori, au wakakuvutia kiasi kwamaba ukaamua kuwalisha baadhi ya vitu ulivyo navyo; jambo hilo haliruhusiwi na hifadhi yoyote kwa sababu za kisayansi na za kimazingira. Kwa kuwalisha wanyamapori kitu kingine tofauti na walichozoea kula utaharibu ile hali ya uasili wao, yani ile genetic (vinasaba) yao inabadilika, na vile vile tabaia ya asili inaweza kupotea kwa wanyamapori hawa, hivyo kusababisha tabia ambazo hazitarajiwi kwa Wanyama hawa, pia magonjwa mbali mbali ya kuambukiza.
- Usifanye kelele ambazo zitawasumbua ama kuwaudhi wageni wengine
Epuka usumbufu wowote kwa ajili ya wageni wengine, kuna wengine wanaitana kwenye magari, au kupigiana honi za magari au miluzi. Ijulikane kuwa watu wanatembelea hifadhi wakiwa na malengo mbali mbali, wengine wanachukua picha, wengine wanaangalia tu wanyamapori, wengine wanachukua filamu, au video, hivyo hata kama unamfahamu mwenzako akiwa kwenye gari tofauti na lakwako epuka kusababisha kelele nan a usumbufu kwa wageni wengine. Huruhusiwi hata kuwasha redio au kufungua mziki kwenye simu yako, utawasumbua wengine na hata Wanyama wanaopenda utulivu.
- Usichume maua ama kukata mimea
Unapofika hifadhini pia usichume au kukata miti au maua ya miti iliyopo hifadhini, hata kama mti huo ni dawa, au ni maua mazuri yanayokuvutia hautakiwi kuchuma au kuakata. Ikumbukwe haya ni maeneo ya kiasili na kila kinachofanyika ndani ya hifadhi kinaendana na utunzaji wa uhalisia na ecologia ya viumbe hai wote, hivyo epuka kabisa kukiuka sharia hizi ili kufurahia safari yako ndani ya hifadhi.
- Usitupe takataka ama mabaki ya sigara
Endapo utakuwa na takataka zozote zile kwenye gari au kwenye mifuko yako, usitupe ndani ya hifadhi kwasababu zinzleta madhara makubwa kwa kuharibu uhalisia wa mazingira haya na Wanyama hivyo tunza takataka zako uziweke sehemu maalumu iliyoainishwa na mamlaka ya hifadhi, uzuri ni kwamba kila unapotaka kuingia ndani ya hifadhi utafika kwenye lango maalumu la kulipia nah apo ndipo unaweza kuacha taka zozote ili kuepuka usumbufu uwapo ndani ya hifadhi. Hata kama unavuta sigara hapo kwenye lango ndio sehemu ya kufanya hivyo.
- Usilete Wanyama wa kufugwa ndani ya hifadhi
Kuna wale watu wanawapenda sana Wanyama wa kufungwa kiasi kwamba hupenda kusafiri pamoja nao, wanyama kama mbwa, au paka, au ndege, au samaki au nyoka, au Wanyama wengine wowote sharia za hifadhi ni kali sana kwenye hili jambo hiyo unapojipanga kutembelea hifadhi yoyote epuka hilo jambo. Endap utakuja na wanyama wa kufungwa utasababisha usumbufu, na pia hautaruhusiwa kuingia naye, au mnyama huyo anaweza kusababisha kelele atakapowaona wanyama wengine huko hifadhini, au anaweza kuruka na kupotelea ndani ya hifadhi.
- Usiende kutembea safari za miguu bila kuwa na askari
Ukishaingia ndani ya hifadhi, usipende kushuka shuka na kutembe kwa miguu bila ulinzi wa askari, porini kuna hatari kila wakati, kuna wanyama wakaili, kama simba, Nyati au tembo, nyoka na wengine ambao endapo utatembea kwa miguu bila kuwa na ulinzi wa askari. Hivyo hata kama unataka kupiga picha vizuri usishuke ndani ya gari bila maelekezo kutoka kwa viongozi ulio nao, pia kuna wale wanaopenda kupiga selfie wakiwa na wanyama ndani ya hifadhi hii itahatarisha sana maisha yako na maisha ya wengine ulio nao endapo utashuka ndania ya gari. Zingatia hilo rafiki.
- Usiwashe moto hifadhini
Unapofika hifadhi jihadhari kabisa usichome moto sehemu yoyote ndani ya hifadhi, au ukavuta sigara ukiwa ndani na kusababisha kuchoma misitu na mali asili nyingine muhimu kwa makazi ya wanyama, epuka kabisa uchomaji moto uwapo hifadhini. Mioto yote inayochomwa ndani ya hifadhi ni mioto inayochomwa kitaalamu, kwa makusudi mbali mbali na kwa maeneo maalumu na watu maalumu ndio wenye kazi ya kuchoma moto hifadhini. Kwa wewe mgeni unayetembelea tu hifadhi usifanye hivyo, itakugharimu sana na utasababisha uharibifu kwa viumbe hai waliopo hifadhini.
- Uwindaji hauruhusiwi
Kati ya jambo jingine hatari zaidi ni uwindaji ndani ya hifadhi, kama umekuja kutembelea hifadhi kwa malengo yako mengine ambayo ni kinyume na sharia na taratibu za hifadhi, kama vile uwindaji, chonde chonde usifanye hivyo, maana sharia ni kali mno. Pia si hivyo tu huruhusiwi kubeba silaha za uwindaji kama vile bunduki, manati, panga, kisu, fimbo, au zana yoyote inayoweza kuhusishwa na uwindaji ndani ya hifadhi. Hata kama umemwona ndege ameanguka hurusiwi kumchukua, hata kama umeona dikidiki amelala au amevunjika mguu, huruhusiwi kumchukua, hata kama umeona tembo amekufa na ana meno yake huruhusiwi kuyachukua wala kuyatoa, bali unaruhusiwa kutoa taarifa kwa uongozi wa hifadhi hiyo ili wajue cha kufanya; hivyo basi utakavyovikuta hifadhini viache humo humo
10. Usiache chochote ulichokuja nacho
Pia huruhusiwi kuacha vitu vyako ulivyokuja navyo ndani ya hifadhi, hakikisha umechukua kila kitu ulicho kuja nacho, kama ni maji, au kamera, au nguo usiache ndani ya hifadhi, hakikisha vitu na vifaa vyako vungine umevichukua unapotoka hifadhini
11. Usiendeshe gari nje ya barabara za hifadhi
Unapotembelea hifadhi yoyote zingatia sana sharia na kanuni zilizopo ili uweze kufanya safari zako vizuri na ufurahiye. Kwa wale madereva hawaruhusiwi kabisa kuchepuka nje ya barabara ambazo zimewekwa kwa ajili ya kutalii, wakati mwingine dereva anaweza kushawishiwa na wageni wake au yeye mwenyewe kuchepuka (off road) na kuendesha sehemu ambazo haziruhusiwi na mamlaka ya hifadhi, endapo utachepuka na kukamatwa utalipa faini kubwa sana na siku yako itaharibika. Pia kwa kuchepuka utawasumbua Wanyama na kuharibu mazingira ya hifadhi.
Hizo ni baadhi tu za zilie sharia muhimu sana unapotembelea hifadhi yoyote ya Taifa, au hifadhi yoyote nje ya Tanzania. Zingatia haya uanapotembelea hifadhi ili ufurahie safari yako na ujifunze mengi kutoka hifadhini.
Kuna mengi ya kujifunza na kufanyia kazi kutoka kwenye hifadhi zetu, hivyo usiache kufuatilia blog hii ili upate maarifa na taarifa muhimu za hifadhi na wanayamapori, pia unaweza kuwashirikisha wengine makala hii ili wazijue na kupata ufahamu kuhusu sharia hizi muhimu za hifadhi.
Asante sana; makala hii imeandaliwa na kuandikwa na
Hillary Mrosso
0742092569