Mbwa mwitu wa Afrika (African Wild Dog) ni mnyama wa porini mwenye umbo la mbwa wafugwao japokuwa wana utofauti wa moja kwa moja kwenye Idadi ya vidole vyao vya miguu ya mbele, rangi ya ngozi zao na umbo la masikio yao. Mosi. Idadi ya vidole vyao vya miguu ya mbeleni vinne na hawa wakufugwa wanavidole vitano. Pili mbwa mwitu ngozi yake imepambwa na madoa ya rangi nne ambazo ni nyeusi, kahawia, nyeupe na njano ambazo humfanya avutie zaidi. na hawa wakufugwa wengi wao wana rangi moja ya kahawia, au nyeusi . Tofauti nyingine yenye kuonekana kwa urahisi ni umbo la masikio ya mbwa mwitu wa Afrika kuwa mduara yenye kumwezesha kuwasiliana na wanafamilia wengine kwa njia mbali mbali za sauti. Vile vile  masikio haya humsaidia kuweza kuratibu changamoto za usawa wa joto kwenye miili yao.

Picha (kwa hisani ya www.asiliaafrika.com ); mbwa mwitu wa Afrika alivyopambwa na madoa yenye rangi ya kahawia, nyeusi, nyeupe na njano.

Mistari au madoa kwa kila mnyama huweza kumtofautisha kati ya mnyama mmoja na mwingine. Baadhi ya wanyama hao ni  kama vile chui, duma, pundamilia, tandala, fisi na mbwa mwitu.  Hivyo sifa hiyo imekuwa ikitumika katika utafiti na utambuzi wa kila mnyama wa jamii husika.

Sifa hii kubwa ya utofauti wa namna ya mpangilio wa madoa na mistari katika ngozi za wanyama una kazi kubwa katika kuratibu mifumo mbalimbali ya mwili kama vile kurekebisha na kusawazisha kiwango cha joto kwenye miili yao. Hii inaoneka sana kwenye mistari myeusi na myeupe ya pundamilia. Pia wanyama hawa wamekuwa wakipata faida ya kutokugundulika na maadui/mawindo zao kwa sababu mara nyingi mistrari/madoa yanaendana na mazingira pamoja na uoto wa maeneo wanayopendelea kushinda, mfano mbwa mwitu wa Afrika, madoa yake yamekuwa yakiendana na uoto wa mazingira wanayokuwepo na hii imewasaidia wasionekane na mawindo yao wakati wa uwindaji hasa nyakati  zisizokuwa na mwanga mkali hususani mawio na machweo.

Muundo wa familia; Haijalishi idadi kubwa ya wanafamilia wanaokuwepo katika kundi, wote huongowa na kutawaliwa na wanafamilia wawili ambao ni jike na dume wanaozaa. Wanyama hawa hukaa katika makundi yenye wanafamilia 6 hadi 30. Hata hivyo uwingi wao kwenye familia haujawahi kuhusishwa na kupigania vyeo kama ilivyo kwa jamii nyingine ya wanyama wanaokula nyama kama vile Simba. Wanafamilia hawa huishi kwa ukaribu zaidi kitu ambacho kimewafanya wawe miongoni mwa jamii ya mbwawenye mwingiliano mkubwa. Hii huonekana wakati wa uwindaji ambapo baadhi ya wanafamilia huenda kuwinda na hurudisha windo kwa wanafamilia wote waliobaki pasipokuwasahau watoto. Mara nyingi wanafamilia wakubwa hutapika chakula walichokula wakati wa kuwinda ili kuwalisha watoto.

Wanafamilia wamekuwa wakifanya mawasiliano baina yao kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kugusana, kuchezesha mikia na kutoa aina tofauti za sauti, ambazo ni ‘short bark’ambayo mara nyingi hubweka kupeana ishara/alarm, ‘howl’ ambayo hutolewa kwa lengo la kukutanisha wanafamilia wote kama mikutano ya hadhara na ‘bell-likesound’ ambayo hutolewa kwa lengo la kuwasiliana na wanafamilia ambao wapo umbali mrefu.

Mfumo wa uwindaji na mawindo yao; Mbwa mwitu wa Afrika ni miongoni mwa wanyama wenye umbo la kati hivyo kwa kiasi kikubwa huwinda wanyama wanaoendana kiumbo au wenye umbo dogo zaidi. Mawindo hayo ni pamoja na swala wadogo (swala pala, swala tomi na swala granti), tandala, na nyumbu. Huwawinda katika mfumo uhusishao zaidi ya wanafamilia 6 mpaka 20 ambapo kabla hawajaanza kuwinda hufanya sherehe ya kucheza yenye kuambatana na utengenezaji wa mduara baina yao kisha hushikana na kutoa sauti ambazo huwasisimua kwa ajiri ya kulikabili windo.

Mfumo huu wa uwindaji katika makundi huambatana na uvumilivu mkubwa wa mbio za mawindo yao pamoja na uwezo wa kutengeneza mbinu wezeshi za uwindaji kama vile kugawana katika makundi mawili, ambapo baadhi hutangulia mbele ya windo walilokusudia na wengine waliobaki husogea karibu na kuzunguka windo hilo, hivyo huwasaidia kufanikiwa zaidi katika uwindaji. Na hii imedhibitishwa na baadhi ya watafiti kwamba mbwa mwitu wa Afrika ndiye huongoza kufanikisha mawindo yao kwa asilimia 80%.

Picha (kwa hisani ya www.youtube.com ); Namna mbwa mwitu wanavyojigawa kwenye makundi wakati wa kuwinda.

Uzalianaji wao; Mbwa mwitu wa Afrika ndiye mnyama katika jamii ya mbwa mwenye uwezo wa wakuzaa watoto wengi kuanzia 2 mpaka 20 kwa uzao mmoja (na ujauzito wake hukaa kwa muda wa siku 70). Kutokana na uwingi huo huhitaji eneo kubwa kwa ajiri ya kutafuta mawindo (eneo linalohitajika ili waweze kulitumia ni kilomita za mraba 3500)) Ukubwa wa eneo linalohitajika kwa ajili ya mawindoyaoumechangia kuwa miongoni mwa wanyama wanaohitaji jitihada za ziada ili kuweza kuwahifadhi. Umri wao wa kuishi ni miaka kati ya 10-12 wakiwa na uzito wa 18-36kg na urefu wa 1m. Katika watoto wanaozaliwa, madume huwa ni wengi zaidi mara mbili ya majike na katika makuzi ya watoto hawa wanafamilia wote wanajukumu la kuwalisha na kuwalinda hivyo hukua katika uchangamfu ambao huwasaidia kujamiiana na kuingiliana kwa urahisi. Mwingiliano huo mkubwa huwasaidia kuwakwepa maadaui zao wakubwa ambao  simba na binadamu. Baad ya kuzaliwa na kukomaa kwa viungo vya uzazi majike huondoka kwenye familia kwa ajili ya kuanzisha familia yao na madume hukaa kwenye ‘natal pack’ ambalo ni kundi la vijana.

Picha (kwa hisani ya www.haspikdokum.com ): Mwanafamilia mkubwa akitapika nyama aliyokula ili kumlisha motto.

Ngazi ya uhifadhi na usambaaji wao; Miaka 20 iliyopita mbwa mwitu wa Afrika walipatikana katika nchi zisizopungua 40 katika ukanda wa kusini mwa jangwa la Sahara. Lakini miaka ya hivi karibuni iliyoambatana na changamoto ya ukuaji  wa shughuli za maendeleo ya binadamu, uvamizi wa binadamu kwenye maeneo yaliyohifadhiwa, migogoro na wafugaji pale wanyama wakubwa wanaokula nyama kama simba, fisi, chui, duma na mbwa mwitu mwenyewe wanapovamia mifugo (, na uelewa mdogo wa uhifadhi vimechangia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa idadi yao na kuwa miongozi mwa wanyama waliohatarini kutoweka yaani Critically endangered species, Kwa sasa makadirio yao ni uwepo wa mbwa mwitu wa Afrikaa 6,600 katika nchi zisizopungua 10 mpaka 25 ikiwa ni pamoja na Tanzania, Botswana, Zambia, Namibia, Afrika kusini, Zimbabwe na Kenya.

NB; Takwimu na taarifa zenye kuhusisha nchi, idadi ya mbwa mwitu wa Afrika na vipimo vyake zimetolewa kwenye ukurasa wa Africa Wildlife Foundation na www.lionworldtravel.com.

Ni matumaini yangu kwamba wewe msomaji wa makala hii umeweza kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu mbwa mwitu wa Afrika ambaye kwasasa anashika nafasi ya pili baada ya Mbwa mwitu wa Ethiopia kuwa hatarini kutoweka. Hivyo basi jitihada za pamoja zinahitajika ili kuweza kuhakikisha ya kwamba wanyama hawa wanahifadhiwa kwa jitihada zote huku kila mdau akitimiza wajibu wake ipasavyo. Makala hii imehaririwa na Alphonce Msigwa, Mwikolojia hifadhi za taifa Tanzania.

Makala imeandikwa na;

Leena Lulandala

      0755369684

lulandalaleena@gmail.com