Tanzania ni moja ya nchi zenye mandhari za kuvutia na hifadhi za wanyamapori zinazojulikana duniani kote. Tanzania inajivunia hifadhi na mbuga za wanyamapori zinazovutia maelfu ya watalii kila mwaka.

Maeneo ya Hifadhi za Taifa kama Serengeti, Katavi, Ngorongoro, Mikumi, Nyerere, na Ruaha ni mifano hai ya uzuri wa asili na urithi wa wanyamapori. Hata hivyo, ili kufurahia safari yako kwa usalama na bila usumbufu, unahitaji kufuata tahadhari maalum. Makala hii inaeleza tahadhari muhimu za kuchukua ili safari yako iwe ya kipekee, salama, na isiyosahaulika.

Fuata Maelekezo ya Waongoza Watalii

Waongoza watalii ni watu wenye uzoefu wa mazingira ya hifadhi na tabia za wanyama. Wanajua maeneo salama, njia za kufuata, na jinsi ya kukabiliana na hali yoyote isiyo ya kawaida. Ni muhimu kufuata maelekezo yao ili kuepuka hatari. Kwa mfano, ikiwa waongoza watalii wanakuambia usiondoke kwenye gari wakati wa safari ya game drive, ni kwa sababu wanyama wa porini, kama simba au tembo, wanaweza kuhisi tishio ukikaribia. Kuwapuuzia waongoza watalii kunaweza kusababisha hatari kubwa kwa maisha yako.

Epuka Kusogelea Wanyama wa Porini

Wanyama wa porini wanapaswa kuheshimiwa katika makazi yao. Hata kama wanaonekana wapole au wavivu, unapaswa kuwa mbali nao. Tembo, nyati, au hata swala wanaweza kuwa wakali ikiwa watahisi tishio. Mtu anayesogelea mnyama wa porini anaweza kusababisha wanyama hao kujihami, hali ambayo mara nyingi husababisha ajali mbaya. Fuata kanuni ya dhahabu ya “kutazama lakini kutogusa.”

Watalii wakitalii katika hifadhi za Taifa Tanzania, epuka kuchepuka kutoka barabarani kuwasogelea wanyama

Usilishe Wanyama wa Porini

Kulisha wanyama ni kosa ambalo linaweza kuonekana dogo lakini lina madhara makubwa. Tabia hii huathiri mfumo wa asili wa wanyama, na kuwafanya wawe tegemezi kwa binadamu. Kwa mfano, tumbili au nyani wanaweza kuwa wakali wakiona chakula mikononi mwako. Hii inaweza kuhatarisha usalama wako na pia kupunguza nafasi ya wanyama hawa kuishi kwa kujitegemea katika mazingira yao. Soma hapa ili kufahamu zaidi madhara ya kulisha wanyamapori Zijue Sababu Zinazochangia Binadamu Kuzoesha/Kuzoeana na Wanyamapori (Wildlife Habituation)

Kuna maeneo maalumu ya kulisha wanyama, lakini hifadhini hairuhusiwi

Vaa Mavazi Yanayofaa

Mavazi yanayofaa ni muhimu kwa safari za hifadhi. Rangi zisizo kali kama beige, khaki, au kijani kibichi husaidia kujificha katika mazingira ya asili, na pia hupunguza uwezekano wa kuvutia wanyama. Pia, mavazi yenye mikono mirefu yanaweza kusaidia kujikinga na kuumwa na mbu au mchwa. Hakikisha viatu vyako vinafaa kwa matembezi, hasa ukitembelea maeneo yenye mawe au nyasi ndefu. Soma hapa kufahamu mavazi yanayofaa kwa utalii mbugani Mavazi Sita(6) Muhimu Unayotakiwa Kuvaa Unapotaka Kutembelea Hifadhi au Porini

Hawa ni watalii, wakiwa na mavazi mazuri ya utalii pamoja na vifaa vya muhimu kwa ajili ya utalii.

Hifadhi Chakula Vizuri

Kuweka chakula wazi kunaweza kuvutia wanyama kama vile nyani, tumbili, fisi, tembo, ndege, nk. Katika kambi za hifadhi, hakikisha chakula kimefungwa vizuri na kimehifadhiwa ndani ya magari au vyombo maalum. Wanyama hawa ni wepesi wa kunusa chakula na wanaweza kuwa wakali wanapokiona, hali inayoweza kuhatarisha maisha yako.

Epuka Kutembea Usiku Peke Yako

Wanyama wengi wa porini wanafanya shughuli zao nyingi nyakati za usiku. Usitembee nje ya kambi au maeneo yaliyotengwa bila kiongozi au askari. Hii ni muhimu hasa katika hifadhi ambapo wanyama kama chui au fisi wanaweza kupita karibu na kambi. Tembea kwa makundi au na mwongozo uliyoidhinishwa.

Kuwa na Vifaa Muhimu vya Dharura

Vifaa kama tochi, Dira, simu iliyojaa chaji, ramani, na kifaa cha huduma ya kwanza ni muhimu unapokuwa hifadhini. Kwa mfano, tochi itakusaidia kuona njia au kuwatisha wanyama wadogo  nyakati za usiku. Simu yenye chaji pia ni muhimu kwa mawasiliano ya dharura iwapo utapotea au kukumbwa na hali isiyotabirika. Soma zaidi hapa kufahamu zaidi Zijue Sheria  Na Taratibu Kumi Na Moja (11) Za Hifadhi Za Taifa

GPS, Kifaa hiki kiwaweza kusaidia endapo umepotea, pia kinaweza kutoa muelekeo wa sehemu

Uzingatie Sheria za Hifadhi

Kila hifadhi ina sheria zake za kulinda wanyama na wageni. Usivuke mipaka ya maeneo yaliyotengwa kwa wageni, usitumie moto kiholela, na epuka kutupa taka ovyo. Sheria hizi zipo kuhakikisha hifadhi inabaki salama na endelevu kwa kizazi kijacho. Kumbuka, ukilinda mazingira, unalinda uzuri wa Tanzania. Unaweza kusoma hapa zaidi kufahamu baadhi ya sheria muhimu za hifadhini Utaratibu Wa Kutembelea Mbuga Za Wanyama.

Matembezi ya kuwaona sokwemtu

kama utatembelea hifadhi kama Gombe au kisiwa cha Rubondo ambazo sokwemtu hupatikana kwa wingi ni muhimu kuchukua tahadhari kama kuambatana na mwongoza watalii muda wote. Pia kama unaumwa magonjwa kama ya kifua, mafua, homa ya manjano, homa ya ini na mengine, hauruhusiwi kufanya matembezi haya. Ni muhimu kuzingatia kuwa Watoto chini ya miaka 12 hawaruhisiwi kufanya matembezi haya. Soma hapa kufahamu mengi kuhusu Sokwe Maajabu Ya Sokwe Wa Hifadhi Ya Taifa Gombe

Watalii wakiwa katika hifadhi ya Gombe, kuangalia Sokwemtu

Utalii wa magari

Dereva mwongoza watalii usizidishe mwendo wa gari zaidi ya kiwango kilichowekwa na mamlaka husika kuepuka ajali au kugonga wanyama ndani ya hifadhi pia usiendeshe gari nje ya barabara. Fuata alama zilizowekwa, usimkimbize mnyama na gari, usiwasogelee wanyamapori zaidi ya umbali uliowekwa. Usipige kelele na epuka sauti  kubwa pamoja na muziki hii inaweza kusababisha usumbufu kwa wanyama

Utalii wa magari, katika hifadhi za Tanzania, picha na footlopestour.com

Utalii juu ya daraja la kamba

Kutembea katika daraja la juu ya miti kwenye hifadhi kama Manyara, Udzungwa, na Ruaha ni uzoefu wa kipekee unaotoa mtazamo wa juu wa mandhari na wanyamapori. Hata hivyo, usalama unapaswa kupewa kipaumbele ili kuhakikisha unafurahia matembezi hayo bila hatari. Kwanza, hakikisha unafuata maelekezo ya waongoza watalii na tembea kwa uangalifu. Epuka kutembea wakati wa mvua Kwani nyaya au njia za mbao zinaweza kuwa telezi. Muongoza watalii zingatie usizidishe Idadi ya wageni iliyopendekezwa.

Utalii juu ya daraja la kamba katika hifadhi ya Taifa ya ziwa Manyara, Tanzania

Panga Safari na Kampuni ya Kuaminika

Safari iliyopangwa na kampuni inayotambulika, hutoa uhakika wa usalama na huduma za kitaalamu. Kampuni hizi zina timu ya waongoza watalii wenye ujuzi wa kutosha na huhakikisha unapata uzoefu wa kipekee bila kuhatarisha usalama wako. Ukiataka kutalii na kampuni za uhakika usisite kuwasiliana nasi, tutakushauri na kukuongoza vizuri.

Hitimisho

Kuzingatia usalama na tahadhari ukiwa kwenye hifadhi za Tanzania ni njia bora ya kuhakikisha safari yako inakuwa ya kusisimua na isiyosahaulika. Tanzania ni nchi yenye uzuri wa asili na urithi wa wanyamapori unaostahili kuhifadhiwa. Kwa kufuata maelekezo ya waongoza watalii, kuheshimu wanyama wa porini, na kutii sheria za hifadhi, utaweza kufurahia kila sekunde ya safari yako.Karibu Tanzania, na ufurahie uzuri wa asili kwa tahadhari na usalama!

Makala hii imeandikwa na Cecilia Mwashihava, na kuhaririwa na Hillary Mrosso. Kwa maswali, maoni, ushauri na mapendekezo usisite kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa namba hapo chini.

 

Cecilia Mwashihava

mwashihavacecilia@gmail.com

+255747268217

Tunaandika makala hizi ili watu waongezewe uelewa kuhusu kulinda na kutumia Maliasili muhimu bila kuathiri uwepo wao wa sasa na baadaye; kazi hii tunafanya kwa kujitolea na hakuna malipo yoyote, endapo umefurahia kazi zetu kutuunga mkono kwa kiasi chochote ili tupate nguvu, na ari ya kuandika makala nyingine nzuri, usisite kuwasiliana nasi kwa maelezo zaidi