Karibu, na habari za mwanzo wa siku ya wiki ndugu msomaji wa makala hizi za wanyamapori. Ni matumaini yangu umzima wa afya na unaendelea na majukumu ya kimaendeleo kama kawaida ili kupambana na hali ya uchumi kwa mafanikio ya hapo baadae. Nami nikuunge mkono katika mapambano hayo kwani mwisho wa siku matunda ya upambanaji wako yataonekana huku yakiwa yamejaa mafanikio ya hali ya juu.
Basi kama ilivyo kawaida na mimi leo mwanzo wa juma la wiki naingia darasani kukujuza kidogo kuhusu mambo yetu ya wanyamappori ili unapokuwa unashughulika na majukumu yako ukumbuke pia tuna rasilimali nyingi sana hapa nchini ambazo mimi na wewe pamoja na majukumu tulionayo tunahitaji kutunza rasilimali hizi kwa faida ya vizazi vijavyo. Katika darasa la leo tutamuona mnyama machachari sana mwenye umbo dogo lakini makini sana katika shughuli zake awapo porini na hasa anapotaka kufanya mawindo yake. Na moja kwa moja leo tutamuweka mezani mnyama “MBWEHA”
Kabla sijaendelea napenda utambue kuwa kuna jamii nyingi sana za mbweha ambazo miongoni mwao ni kama;
- Mbweha Mgongo Mweusi,
- Mbweha wa Mbuga,
- Mbweha Dhahabu,
- Mbweha Miraba na
- Mbweha Habeshi.
Sasa katika jamii hizi nilizo orodhesha hapo juu leo tutamchambua mmoja tu ambae ni “MBWEHA MGONGO MWEUSI” (Black Backed Jackal)
UTANGULIZI
Mbweha mgongo mweusi ni jamii ya mbweha ambao wanapatikana bara la Afrika pekee tu. Mbweha hawa ukiwaangalia kwa haraka haraka unaweza kuwachanyanya na jamii nyingine za mbweha kwani wana fanana maumbile na hata ukubwa wa miili yao. Kuna sifa mbali mbali ambazo ukiwachunguza vizuri ndo utagundua kuwa ni jamii tofauti za mbweha. Sasa leo nataka ufahamu sifa za kuwatofautisha mbweha hawa na jamii nyingine za mbweha.
SIFA NA TABIA MBWEHA MGONGO MWEUSI
1.Wana rangi nyeusi iliochanganyika na alama za rangi ya fedha mgongoni. Rangi hizi ndo huwatofautisha mbweha hawa na mbweha wengine na hata jina lao limetokana na uwepo wa rangi hii katika migongo yao.
2.Wana miguu mirefu kidogo, miili ya wastani na pua ndefu iliyo chongoka kama ya mbwa.
3.Sehemu nyingine za miili yao zina rangi ya uwekundu unaofanana na kahawia ambapo rangi hii hushamiri miguuni na kwa upande wa ndani ya miili yao na sehemu ya chini wana rangi nyeupe.
4.Wana mikia minene ambayo kwa sehemu ya nchani ina rangi nyeusi lakini pia wana masikio yaliyo chongoka.
5.Miguu ya mbele ina mifupa iliyo shikana, na hii huwafanya wanyama hawa kuwa imara zaidi wakati wa kukikmbia na tafiti zinaonyesha mbweha hawa wana uwezo wa kukimbia kwa mwendo wa kawaida kilometa 12km hadi 16km kwa saa.
6.Ukiwachunguza vizuri sehemu za pembeni mwa pua wana alama ya mstari mweupe ambao unakuja mpaka karibu na nusu ya nyuso zao.
7.Wana vidole vitano katika miguu ya mbele huku miguu ya nyuma ina vidole vine tu.
8.Mbweha mgongo mweusi ni wanyama ambao wanaishi kwa namna mbili za kutafuta chakula ambapo wakula mizoga wanapokuta mnyama kafa au kuuwawa na mnyama mwingine lakini pia ni wawindaji ambapo wana uwezo wa kumkimbiza mnyama na kumkamata kama walivyo jamii ya wanyama wengine walao nyama.
9.Wanyama hawa huwa waaminifu na dume mmoja huishi na jike mmoja tu wakati huo huishi kwenye kundi ambalo linajumuisha watoto, wazazi pamoja na mbweha wengine wakubwa ambao huwa hawazaliani ndani ya kundi hilo na kuishi kama wasaidizi lakini hawa pia wanatokana na kizazi cha wazazi wa kundi hilo.
10.Wanyama hawa wana uwezo wa kuona vizuri mchana na usiku japo huwa wapo vizuri sana wakati wa usiku na kama ni mchana wanaonekana sana maeneo ambayo hayajaaribiwa sana na shughuli za kibinaadamu kama kilimo.
11.Ni wanyama ambao wanaishi kwa mipaka na himaya ambapo eneo lao linaweza kuwa na kilometa za mraba 10.6km na mara nyingi huweka alama kwenye mipaka yao kwa kutumia mkojo.
12.Hulinda himaya yao kwa jitihada zote hususani kwa mbweha wengine au kizazi kingine kisije kuvamia eneo hilo.
UREFU, KIMO NA UZITO WA MBWEHA MGONGO MWEUSI
Urefu=Kuanzia kichwani hadi kiwiliwili mbweha hawa huwa na urefu wa sentimita 96 hadi 110 huku mkia pekee ukiwa na sentimita 26 hadi 40.
Kimo=Mbweha hukuwa na hufikia kimo cha sentimita 30 hadi 48.
Uzito=Tafiti zinaonesha kuwa mbweha mgongo mweusi wa Afrika ya Mashariki huwa na uzito mkubwa kidogo ukilinganisha na na wale wa Zimbabwe. Ambapo mbweha wa Afrika Mashariki hufikia uzito wa kilogramu 7kg – 13.5kg, wakati wale wa maeneo ya Zimbabwe yaani maeneo ya Magharibi huwa na uzito wa kilogramu 6.8kg – 9.5kg.
MAZINGIRA
Kama tulivoona hapo juu mbweha hawa wana patikaba barani Afrika tu na si sehemu nyingine tena hapa duniani. Hapa barani Afrika wanapatikana maeneo ya Mashariki mwa Afrika na maeneo ya Kusini-Magharibi mwa Afrika huku Tanzania tukijivunia kuwa na wanyama hawa kwa wingi tu.
Katikati ya maeneo haya kuna bonde la ufa kubwa ambalo lina mazingira mabaya sana kwa mbweha hawa kuishi kitu ambacho kinasemekana ndo sababu ya mbweha hawa kugawanyika katika makundi yanayoishi sehemu mbili.
Mbweha mgongo mweusi huishi katika mazingira mbali mbali yakiwemo yenye nusu jangwa na maeneo yenye miti mingi. Japo kwa asilimia kubwa sana hupatikana maeneo yaliyo wazi na hasa hii ni kutokana na asili ya uwindaji wao.
CHAKULA
Mbweha hawa wanakula vyakula aina mbali mbali kama nyama,mimea, viumbe wasio na uti wa mgongo, reptilian, wadudu pamoja na amfibia.
KUZALIANA
Dume na jike huishi pamoja kwa muda mrefu sana bila kuwa na usaliti kama tulivyoona hapo juu. Mara nyingi wanyama hawa hupandana kipindi cha mwezi wa tano hadi mwezi wa nane. Kipindi hiki cha miezi minne ndo mara nyingi majike huwa wanakuwa kwenye kipindi kizuri cha kupata mimba.
Jike anapo pata mimba hukaanayo kwa muda wa miezi miwili (takribani siku 60). Anapo karibia kuzaa jike hutafuta shimo zuri na mara nyingi hupenda kuingia kwenye mashimo yaliyo chimbwa na mnyama ajulikanae kama ‘Muhanga” kwani mashimo hayo huwa na njia nyigi za kutokea endapo kuna hatari. Endapo hakuna shimo karibu basi jike hulazimika kuchimba shimo mwenyewe ndani ya himaya yao shimo ambalo huwa na urefu wa mita 1-2.
Baada ya hapo huzaa watoto hadi wanne japo mara nyingi wanaokuwa huwa ni kati ya mmoja hadi watatu. Watoto wanapo zaliwa huwa na rangi ya kahawia inayofanana na nyeusi na huzaliwa wakiwa hawaoni, halii hii hukaa nayo na kuanza kuona baada ya siku kumi tangu kuzaliwa.
Kwa muda wa wiki tatu mara tu baada ya kuzaa mama hukaa ndani ya shimo ya vichanga wake bila kutoka kabisa nje. Wakati huu baba pamoja na ndugu wengine huenda kuwinda na kumletea mzazi chakula kwani huwa muda wote anakuwa na watoto bila kutoka nje huku suala la ulinzi wa shimo likiwa mikononi mwa mbweha dume.
Baada ya wiki tatu watoto pamoja na mama huanza kutoka nje ya shimo japo hawaendi mbali na shimo hilo. Ifikapo miezi mitatu watoto huanza kuungana na kina mama huku wakishuhudia jinsi wazazi na wakubwa zao wanavyo winda. Watoto wanapo fikisha miezi sita huanza windo lao la kwanza rasmi na kipindi cha miezi 6 – 8 huanza kutafuta himaya yao wenyewe. Baada ya miezi 11 watoto huwa tayari wana uwezo wa kuanza kuzaliana na kipindi hiki huwa tayari wamekwisha anzisha himaya zao binafsi na mbweha wengine.
Maisha ya mbweha mgongo mweusi anapokuwa katika maeeo asilia ya hifadhi huishi kwa takribani miaka minane lakini kama anafugwa chini ya uangalizi mzuri basi kufika hadi miaka 14.
UHIFADHI
Kwasasa wanyama hawa bado hawaja tiliwa maanani sana na mashirika ya uhifadhi. Hii ni kwasababu bado wanapatikana katika maeneo mengi ya hifadhi na kwa wigi zaidi.
Ukiangalia kwenye chapisho la mwaka 2014 la Shirika linalo husika na masuala ya Uhifadhi Maumbileasili Duniani (International Union for Conservation of Nature- IUCN) utaona kuwa wanyama hawa wanapatikana nchi kumi na saba (17) hapa Afrika kitu ambacho kinaleta fahari kwa kuwa na mtawanyiko mkubwa wawanyama hawa.
Tafiti zimefanyika nyingi sana ili kujua tabia za wanyama hawa na hasa kuangalia mahusiano ya ki ikolojia na wanyama wengine. Kubwa zaidi lililo gundulika kwa wanyama hawa ni kwamba, Mbweha mgongo mweusi ni wanyama ambao wana beba vimelea vya ugonjwa wa kichaa cha mbwa, na huu ni ugonjwa wa virusi japo kwa wanyama hawa hauna athari kubwa ukilinganisha na wanyama wengine hususani wanyama wafugwao.
CHANGAMOTO KWA MBWEHA MGONGO MWEUSI
Moja kati ya chanamoto kubwa inayo wakumba mbweha hawa ni migogoro baina ya binaadamu na wanyamapori kwa suala la wanyama hawa kuvamia mifugo hasa watoto wa mbuzi na kondoo kasha nao kuuwawa. Hili linapelekea wanyama hawa kuuwawa kwani wafugaji wanalazimika kuwapa sumu au kuwachoma na mikuki hali kadhalika mishale. Wakati mwingine hulazimika kuwatega hata kwa waya ili kuwauwa tu.
Ajali za bara barani hasa kwa njia ambazo zinapita maeneo ya hifadhi za wanyamapori zimekuwa zikiwauwa wanyama hawa sana.
Kutokana na kubeba kwao vimelea vya ugonjwa wa kichaa cha mbwa, wanyama hawa wamekuwa pia wakiuwawa la wafugaji sana sana kwa dhana ya kuwa endapo wataendelea kuwepo basi wata eneza ugonjwa huu kwa mifugo yao.
Kuna baadhi ya magonjwa ambayo yamekuwa yakiwatesa sana wanyama hawa hasa jamii za wanyama walao nyama. Mfano ugonjwa kama “canine distemper” unauwa sana wanyama hawa na jamii nyingi za wanyama walao nyama.
NII KIFANYIKE ILI TUENDELEE KUWA NA WANYAMA HAWA HAPA NCHINI
Jamii za wafugaji ambazo zinaishi karibu na maeneo ya hifadhi za wanyamapori zitafutiwe maeneo sahihi kwa ajili ya mifugo yao. Hii itasaidia kupunguza kuuwawa kwa mbweha mgongo mweusi kwani tatizo la kuliwa kwa mifugo litapungua lakini pia kuuwawa kwa wanyama hawa kwa dhana ya kuepuka maambukizo ya kichaa cha mbwa kwa wanyama wengine litaisha kabisa.
Sheria za uendeshaji wa magari na mwendo hasa katika hifadhi za wanyama zitiliwe mkazo kwani tumeona moja kati ya matatizo yanayo wakumba wanyama hawa ni ajali za bara barani. Hivyo maderva wote wanao kiuka vibao vya alama za hifadhini wanyang’anywe leseni zao na kupewa adhabu kali ili iwe fundisho kwa madereva wengine.
Kuepuka uvamizi wa maeneo ya hifadhi za wanyamapori kwani hili hupelekea uharibifu wa mazingira na kupelekea wanyama hawa kuhama baadhi ya maeneo kitu ambacho kama hakitotiliwa mkazo kita sababisha wanyama hawa kuanza kutoweka kabisa baadhi ya maeneo.
HITIMISHO
Wanaoona mbali husema huwezi ona thamani ya kitu mpaka kitakapo kutoka kitu kile. Basi hili liwe funzo kwetu sote kama Watanzania kwani uwepo wa wanyama hawa ni faida kwetu sote na si kwa maslahi ya wachache.
Pongezi sana kwa TANAPA kwa kazi kubwa sana tena sana wanayo ifanya ya kujenga maboma hasa kwa wafugaji ilikupunguza uvamizi wa wanyama hawa kwani mifugo inakuwa katika hali ya usalama kwasababu mbweha wanashindwa kuingia ndani ya maboma.
Ahsanteni sana…
Kwa mengi zaidi na ushauri kuhusu wanyamapori na Makala hizi pia kwa ujumla wasiliana na mwandishi kupitia
Sadick Omary
Simu= 0714116963/ 0765057969 / 0785813286
Au tembelea= www.mtaalamu.net/wildlifetanzania
”I’M THE METALLIC LEGEND”