Habari ndugu msomaji wa makala za mtandao huu wa makala za wanyamapori, nakukaribisha leo kwenye aina nyingine ya uandishi wa makala zetu kuhusu maliasili, utalii na utamaduni kwa njia ushairi. Rafiki yangu Lymo alitunga shairi zuri sana kuhusu utalii wa Tanzania na anatuhamasisha kila mmoja kuchukua muda na kufuatilia uzuri huu wa ajabu katika nchi yetu. Karibu ufurahie aina hii ya uandishi, ushairi katika utalii.
1. Tunayo ya kujifunza, huko kwenye utalii,
Ma’rifa tutayafyonza, tukitali’ kwa bidii,
Na polepole tuta’nza, kuinyanyua jamii,
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
2. Tukitali’ tutaona, mambo mengi tena mapya,
Na tena tutakutana, nao watu wengi wapya,
Nyoyo zetu zitavuna, vitu na mwam-ko mpya,
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
3. Palipo na vivutio, panafaa kutalii,
Tupakimbilie mbio, tupatali’ kwa bidii,
Na palete m’endeleo, kwa hao wanajamii,
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
4. Tusiwaache wageni, watalii peke yao,
Watatuacha gizani, kwa hizo juhudi zao,
Kwani huko safarini, wananoa bongo zao,
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
5. Chaneli ya utalii, tunayo tuitazame,
Habari za kitalii, kuskiliza tusigome,
Nyaraka za kitalii, kila mara tuzisome,
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
6. Utali’ wa hapa ndani, mengi umekumbatia,
Mambo ya kitamaduni, nayo ya kihistoria,
Yaki’ngia akilini, hakika hutajutia,
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
7. Nakweleza msomaji, mi’ sipendi kukuficha,
Utali’ wa uwindaji, na utalii wa picha,
Kama unauhitaji, tunao kila kukicha,
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
8. Utalii wa majini, na ule wa nchi kavu,
Wa fukwe za baharini, na wa m’eneo oevu,
Tuutie maanani, tusiupe ulegevu,
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
9. Yatembelee mapango, na hifadhi za Taifa,
Utaujaza ubungo, ujuzi na maarifa,
Na utaziba mapengo, yapitishayo maafa,
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
10. Twende kwenye makumbusho, mazito tutajulishwa,
Hapo panayo malisho, ya kale tutaonyeshwa,
Tutalipata fundisho, tutakinga kuyumbishwa,
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
11. Kilwa ni mji mkongwe, na Zanziba hilo jua,
Itali’ miji mikongwe, ina la kukuambia,
Siku ukiwa mkongwe, mengi utasimulia,
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
12. Yatembele’ makavazi, ujionee nyaraka,
Ujipatie ujuzi, uyaondoe mashaka,
Na uyafanyie kazi, mazuri uliyonyaka,
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
13. YUNESKO yayatambua, m’eneo ya Tanzania,
Yapo saba yatwambia, ni urithi wa dunia,
Wengi wayatembelea, ma’jabu wajionea
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
14. M’eneo yaliyotajwa, na YUNESKO ntakwambia,
Ngorongoro imetajwa, Serengeti nayo pia,
Kilimanjaro ‘metajwa, na michoro ya Kondoa,
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
15. Orodha ina vya bara, na vya kule kisiwani,
Imebeba mambo bora, na yapo mtandaoni,
‘Gofu za Songo Mnara, na za Kilwa kisiwani,
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
16. Mji mkongwe Zanziba, nao umeorodheshwa,
Nalo pori la akiba, la Selu lime’rodheshwa,
Hayo ni m’eneo saba, yote umeshajulishwa,
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
17. Yeye aonaye mengi, huyo huvijua vingi,
Talii sehemu nyingi, kwani zina mambo mengi,
Huko utaona mengi, na utavijua vingi,
Tujijengee tabia, ya kufanya utalii.
MTUNZI: Joachim Kenyatta Lyimo
SIMU: +255 624 747 058