Natambua na kuthamini kila juhudi, kila jitihada na nafasi yako ambayo unaitumia pale unaposoma makala nzuri za waandishi tofauti tofauti za Maliasili na wanyamapori. Ikiwa 07/07 ni siku yangu ya kumbukumbu ya kuzaliwa, nina zawadi kwenu, zawadi ambayo itakurudisha nyumbani kwetu kabisa tulikotoka, zawadi ambayo itakujenga zaidi katika maswala ya uhifadhi na kuthamini vitu asilia, zawadi ambayo itakufanya uipende Tanzania mpaka kufa na kuwa mzalendo, zawadi ambayo haitokugharimu pesa nyingi au muda kama ilivyozoeleka tunapata zawadi kutokana na kuwekeza labda muda mwingi katika masomo, zawadi ambayo hutojutia zaidi utakuja kunishukuru baadae kwa kuipokea.

Yes,nashukuru kila mtu kwa kugusa maisha yangu kwa namna yoyote ile kwa sababu maisha pasipo kugusana katika jambo lolote lile huko ni kuishi na sio maisha!!!!, maana yake tunaishi kwa kutegemeana mfano nyani, pundamilia, swala pasipo tembo mbugani msambaratisha misitu, wana asilimia ndogo sana ya kufurahia maisha yao porini.

Twende Hifadhi ya Taifa Ruaha; nina kila sababu ya kukupa zawadi hii kwa sababu naamini utafurahi kuwa mbugani, hata hivyo bado kuna vitu vya kipekee ambavyo naamini zawadi hii itakufaa. Ruaha ni hifadhi ya taifa iliyopo mkoani Iringa, inafikika kwa njia ya gari na ndege ambapo unashukia ndani kabisa ya hifadhi hiyo.

Kwanza kabisa tambua Ruaha inapokea makundi tofauti ya watu na kwa kiingilio nafuu, maana yake wakubwa kwa wadogo na kwa ada inayoridhisha mfano mtu mkubwa ni kiasi cha 5000Tshs ambacho si gharama kubwa, pia hifadhi hii inatoa malazi sehemu mbali mbali na zenye bei ya kitanzania kabisa na kukupa kibali cha kuotea moto jioni pamoja na kuangalia michezo ya kimasai hasa kipindi cha sikukuu; kwa nini zawadi yangu iwe Ruaha?!

Ni hifadhi kubwa zaidi Afrika Mashariki na ya pili kwa Afrika. Ikiwa ni hifadhi kubwa Afrika Mashariki, imeundwa na tabia ya nchi tofauti tofauti na za kipekee.

Mfano mzuri ni kwamba kuna kila aina ya wanyama wakubwa kwa wadogo mpaka wadudu kama nyuki, nyigu na mchwa, kuna aina nyingi za mimea kama nyasi mpaka mibuyu miti minene zaidi duniani, kuna uoto ama miombo wenye kuvutia na uliopangwa vema na Manani, pia inaweza kuwa ni bahati kwako kujipatia eneo la kuwekeza kama kujenga hoteli na hata maduka ya vitu asilia.

Ni hifadhi ambayo haina msongamano mkubwa sanaaaa wa watalii hivyo kukupa nafasi ya kuona vyema mnyama kwa muda mrefu tofauti na hifadhi nyingine zenye majina makubwa kama Serengeti ambako watalii wanapeana muda wa kuona mnyama ili mwingine nae pia amuone kutokana na msongamano mkubwa wa watalii.

Ni hifadhi ambayo utapata kuona wanyama watano wakubwa (big five), ambao kwa Ruaha ni tembo, chui, simba na nyati na kwa bahati mbaya sanaa faru alishatoweka miaka ya 1980s ila naamini hakijaharibika kitu kwa sababu wanyama hawa kwa hifadhi hii ki rahisi kuonekana maana getini tu unaweza kukaribishwa na makundi ya tembo , japo pia kuna wanyama wengine wengi kama tandala mdogo ambae ni ngumu sana kupatikana hifadhi nyingine.

Ni hifadhi ambayo inaongoza kwa asilimia kubwa kuwa na simba wengi zaidi duniani pamoja na makundi makubwa na mengi ya tembo. Hivyo tegemea kufurahia zaidi safari yako kwa sababu Nina uhakika hutojutia zaidi utafarijika na kuanza kukijengea ratiba ya kutembea hifadhi zetu .

Ni hifadhi pekee ambayo ndani yake ina maeneo ya kihistoria mfano utajifunza mengi kuhusu kabila la wahehe chini ya kiongozi wao chifu Mkwawa ambae alitumia sana eneo la hifadhi kipindi cha zamani anapigana vita na wajerumani pia kuhusu wagogo ambao imeenda zaidi na kuonyesha kua eneo hilo lilipendwa zaidi mpaka chifu Mapenza wa Wagogo alizikwa ndani ya eneo la hifadhi; ukiwa mbugani utakutana na majina ya sehemu ndani ya hifadhi kama Telekimbogha neno lenye asili ya kihehe. Mpaka hapo wewe ni nani hata ukiingia usifurahie jamaniiii?!!.

Ni hifadhi ambayo ina mazingira mazuri sana ya kufanyia tafiti za kisayansi kuhusu wanyama na mazingira yake, ambapo maisha kwa ujumla eneo linaloizunguka hifadhi na ndani pia hakuna gharama kubwa za chakula wala malazi hivyo katika tafiti yako hutotumia pesa kubwa zaidi sanaa utafurahi kutokana na utulivu mkubwa uliopo na kuona mwingiliano ulivyo na kutegemeana kwa wanyama porini.

Ni miongoni mwa hifadhi zenye daraja la kamba ambako utafurahia zaidi kutembea kwenye daraja hilo na lililopo juu ya mto Mwagusi na kuchukua picha ambayo utajivunia maisha na kukufanya upate hamu zaidi ya kutembelea hifadhi nyingine nyingi na duniani kwa ujumla.

Naamini mpaka hapo tuko pamoja sasa, pasipo kupoteza muda nakuombea Mungu akusaidie na akubariki zaidi ili ufike  Hifadhi ya Taifa Ruaha na kuweza kusherehekea zawadi yangu ya siku ya kuzaliwa kwangu. Kwa sababu naamini pamoja tunaweza tukainua na kukupa pato la taifa kupitia utalii huu wa kusini.

Mungu ibariki Tanzania,

Mungu ibariki Ruaha,

Ameeen!!.

Imeandikwa na;

Leena Lulandala

Mwanafunzi wa mwaka wa pili- UDSM

( Shahada ya Sayansi ya Wanyamapori na Uhifadhi)

0755369684

Lulandalaleena@gmail.com.