Kusini mwa bara la Afrika, ndipo ilipo Edeni ya simba, sehemu ambayo viumbe hai wa majini na nchi kavu hupatikana kwa wingi, ni sehemu hii ambayo mamilioni ya wanyama, ndege  na mimea asilia imesitawi na kufanya mandhari ya nchi ya Zimbabwe kuwa ya kipekee. Ni katika nchi hii ambapo hifadhi maafuru duniani kwa uhifadhi wa wanyamapori wa kila aina hupatikana, ni sehemu hii ya Hifadhi ya taifa ya Hwange ndipo makundi ya simba na wanyama wengine wa jamii hii ya paka hupatikana. Hapo ilipo moyo na kitovu cha uhifadhi wa simba; mandhari nzuri yaliyohifadhiwa vizuri, chakula cha kutosha, maji na hali nzuri ya hewa imewavutia wanyama hawa na kuwafanya waone eneo hilo ndilo Edeni yao, na kama inavyojulikana na wenyeji wa nchi hiyo kama “Bonde la Simba” au “the Valley of Lions”.

 

Msomaji wangu wa makala hizi usishangae! leo katika uhifadhi wa wanyamapori tutapanda ndege na kushuka kilomita kadhaa Kusini mwa nchi ya Tanzania hadi nchi ya Zimbabwe. Hapa Zimbabwe tutakutana na hadithi nzuri sana za mashujaa wa nchi hiyo, waliopigania uhuru na kuhakikisha mali na ardhi ya Zimbabwe inakuwa ni ya wanazimbwabwe. Tukiachana na hadithi hizo za mashujaa twende moja kwa moja upande wa Magharibi tuingie katika hifadhi ya taifa ya Hwange na hapa ndipo tunapokutana na Andrew, unataka kumjua Andrew ni nani?, endelea kusoma makala hii hadi mwisho.

Ni katika eneo hili ambalo mtafiti nguli na wa muda mrefu Dr. Andrew Loveride alijikuta anatumia maisha yake yote kutafiti na kufuatilia kwa karibu na kwa kina zaidi maisha ya simba katika hifadhi ya taifa ya Hwange nchini Zimbabwe. Andrew anasema maisha yake ya uhifadhi na utafiti wa simba yaliathiriwa zaidi na wazazi wake hasa baba yake ambaye ndiye aliyemuambukiza roho ya uhifadhi.

Licha ya baba yake Andrew kupenda wanyamapori na kutumia muda mwingi kuishi nao, kuwatafiti na hata kuwatunza. Andrew anasema nyumbani kwao kulikuwa na bustani za wanyamapori wadogo wadogo kama vile mijusi, kenge, kobe, nyani, nyoka na wadudu wengeni. Baba yake Andrew anasifika sana kwa moyo wake wa uhifadhi sehemu nyingi barani Afrika, ila kwa kiasi kikubwa alitumia muda mwingi kujifunza na kuwatafiti mamba.

Utafiti wake wa muda mrefu aliufanya kuhusu mamba, aliasaidia sana katika kukuza na kuongeza idadi ya mamba katika hifadhi zao. Aliamua kuchukua mayai ya mamba na kuyatunza ili yaanguliwe kisha kuwalea wale mamba hadi kufikia hataua ya kujitegemea na kuwarudisha mtoni au ziwani. Jambo hili lilipelekea kuongezeka kwa idadi ya mamba.

Simba aliyefahamika kwa jina la Cecil. .AFP via Getty Images

Miaka ya 1960 kulikuwa na kupungua sana kwa idadi ya mamba sehemu nyingi za bara la Afrika, hatua ambao iliashiria hali mbaya sana ya kutoweka kwa wanyama hawa wa ajabu. Hii ilitokana na biashara za ngozi ya mamba kwa ajili ya matumizi ya kutengenezea vitu vya ngozi ambavvo viliuzwa kwa gharama kubwa sana. Katika hali hii ndio ilipelekea baba yake Andrew kuja na mbinu mbadala ya kunusuru kutoweka kwa wanyama hawa.

Jitihada na moyo huo ambao Andrew aliuona kwa baba yake ndipo alipoamua kuingia kaika harakati na vita hivyo vya kuokoa wanyamapori na kuendeleza jitihada za baba yake za kutafiti na kujifunza zaidi kuhusu wanyamapori. Tofauti na baba yake, Andrew alijikita kujifunza kwa kina tabia na maisha ya simba.

Mwaka 1992 ndipo Andrew alipoingia nchini Zimbabwe kama mtafiti wa simba, alifanya kazi katika mradi wa utafiti wa simba ambao ulikuwa unasimamiwa na Chuo Kikuu cha Oxford kilichopo Uingereza, katika kitengo cha utafiti yaani WILDCRU. Andrew anasema licha ya kupata hamasa kutoka kwa baba yake anasema walimu wake ambao walikuwa ni maprofesa wa Chuo Kikuu cha Oxford pamoja na timu ya utafiti iliyokuwepo katika kambi iliyokuwepo Hwange pamoja na wafanyakazi wa hifadhi ya taifa ya Hwange wamekuwa chachu kubwa sana katika kuingia na kufanya kazi zake ya utafiti wa simba huko Zimbabwe.

Ndugu msoamji wangu, leo tunakwenda kujifunza mambo mazito kabisa kuhusu maisha na tabia za simba ambazo huajawahi kuzisikia mahali popote. Katika makala hii nitakuchambulia hatua kwa hatua mambo yote muhimu yaliyonekana na kuandikwa katika kitabu hiki kizuri cha LION HEARTED, The life and Death of Cecil and the future of African Cats kilichoandikwa na Andrew Loveride.

Mwandishi wa makala hii Hillary Mrosso, akisoma kitabu cha LION HEARTED

Andrew amaendika mambo ya muhimu sana kuhusu wanyamapori hasa wanaokula nyama jamii ya paka au Kanivora, kanivora ni wanyama ambao wanakula nyama, kama vile simba, chui, mbwa mwitu, fisi, duma, mbweha nk. Katika kitabu ambacho tunakichambua leo kimesheheni historia za kusisimua, tabia za ajabu za simba, watu na uhusiano na simba, usimamizi wa simba na biashara ya uwindaji wa simba ilivyo na faida na hasara kwa uhifadhi wa simba.

Mambo yaliyoandikwa kwenye kitabu hiki ni matokeo ya utafiti wa kisayansi kabisa kwa kutumia teknolojia ya juu sana katika utafiti wa simba. Ni utafiti wa muda mrefu sana ambao uligharimu muda mwingi sana wa kuangalia miendendo na tabia za wanyama hawa. utafiti kwa njia hii ni hatari sana maana unahusisha wanyama ambao ni hatari na wana nguvu na akili sana, hivyo ni kazi kubwa sana iliyofanyika iliyomgharimu Andrew pamoja na timu yake kwa zaidi ya miaka 20.

Kwa miaka 20 iliyopita idadi ya simba imeporomoka kwa asilimia 43, hii ni kwasababu mbali mbali ambazo mtafiti Andrew amezitaja katika kitabu hiki. Simba wanaokisiwa kuwepo barani Afrika wanaweza wasifike hata 20,000, hii ni idadi ndogo sana kuliko hata idadi ya tembo.Simba ni mnyama anayependwa sana duniani, utafiti unaonyesha zaidi ya nchi 15 duniani zinatumia nembo ya simba kama alamu muhimu ya nchi zao. Mwandishi wa kitabu hiki anatuambia mambo ya kina aliyoyafanyia uchunguzi yaliyopelekea anguko la simba katika bara hili, futatana nami katika uchambuzi huu tujifunze kwa kina kila kitu kuhusu simba.

Hivyo karibu kwenye uchambuzi wa wa kitabu hiki na tujifunze mambo 85 muhimu sana katika uhifadhi wa simba, utafiti, biashara ya uwindaji, utalii, migogoro, umasikini, siasa, mifugo, suluhisho na juhudi za kimataifa katika uhifadhi wa wanyamapori hasa simba.

  1. Njia ya kisasa ya kufanya utafiti; utafiti wa simba sio kazi nyepesi hata kidogo, imegubikwa na hatari nyingi, hasara nyingi na pia changamoto nyingi sana. Hata hivyo pamoja na hayo yote lazima tujifunze njia nzuri za kuishi na wanyama hawa kwa kufanya utafiti za kina na wa kutosha. Utafiti wa simba katika eneo hili la Hwange ulifanyika kwa kuwafunga simba cola. Kola au Collar ni vifaa vinavyofungwa shingoni mwa mnyama yeyote kwa ajili ya kumfuatilia, kujua alipo na umbali anaotembea.
  2. Umuhimu wa kuwafunga wanyama kola, wanyama kama simba ni wanyama ambao wanaweza kusambabisha madhara kwa watu, hasa jamii ya wafugaji, hivyo kwa kuwa na njia ya kuwafunga kola ni rahisi kujua walipo na pia kujua wanakoelekea. Njia hii ni nzuri sana kwasababu inawasaidia wahifadhi na watafiti wa masuala ya uhifadhi kubuni mbinu bora za uhifadhi wa wanyamapori kama simba.
  3. Ufungaji wa kola kwa simba kwa ajili ya kumfuatilia ni kazi nzito ambayo inahitaji watu wenye uelewa na watalaamu wa kufanya hivyo. Sio kila mtu anaweza kumfunga simba kola, kuna watalamu wamesomea mambo hayo, wanajua namna ya kushika simba, namna ya kupima dawa ambayo inampa usingizi na sehemu za kumpiga dawa hiyo. Kitendo cha kumshika simba kinaitwa kudati, mnamdati simba kwa kumpiga kwa kutumia bunduki ambazo zina sindano zenye dawa ya usingizi sehemu husika akisha lala hapo ndio tayari kwa kumfunga kola, kuchukua sampuli kama vile damu na kinyesi kwa ajili ya kwenda kupima maabara.
  4. Hatari ya kupata magonjwa kutoka kwa simba kipindi cha kumfanyia utafiti, hasa kumfunga kola, kuchukua sampuli kama damu na kinyesi. Simba wana minyoo mibaya sana inayoitwa “Taenia spp”, pale unapogusana au kumshika simba kuna mayai ya miyoo hiyo hatari ambayo usipokuwa mwangalifu unaweza kuambukizwa kwa kula na minyoo hiyo kuingia ndani ya mwili wako na kuanza kukusumbua na kusababisha hata kifo. Hivyo katika protokali za utafiti wa simba huwa wanazingatia sana jambo hilo, unawza kuvaa gloves, na baada ya kufanya shughuli zote, ni inashauriwa kunawa mikono kwa maji mengi na sabuni.
  5. Katika harakati za kufanya utafiti wa kanivora wakubwa kama simba inahitaji moyo na uvumilivu wa kutosha. Hii ni kutokana na tabia ya simba kuwa na mambo mengi (complicated behaviour), simba wanatumia muda mwingi sana kulala ili wasipoteze nguvu za kuendelea kuwinda. Hivyo kama lengo lako ni kutaka kumuona simba anazunguka na kutembea mara kwa mara unaweza usifanikiwe kwenye utafiti wako. Hivyo inahitaji uvumilivu na muda mwingi wa kuwafuatilia simba hao kwa kila kitendo.
  6. Sio mara zote itakuwa rahisi kutumia kola katika kufuatilia mienendo ya simba, hii ni kwasababu ni vigumu kuwafuatilia simba wadogo kwa kuwafunga kola, kwasababu ni wadaogo ukiwafunga kola na kuanza kuwafuatilia kwa muda mrefu ile kola inaweza kuja kuwabana na kuwaumiza simba, hii ni kwasababu wanaendelea kukua, ukisema uwafunge kola na kuwanza kufuatilia mmoja baada ya mwingine ni hatari sana. Hivyo sehemu ya simba wanaokua inaweza isijulikane kwa sababu hakuna anayejua wangapi wanakua na kuwa simba wazee.
  7. Kwasababu hiyo kuna mengi hyajulikani kuhusiana na simba vijana ambao wapo kwenye kundi kama wanafikia katika hatua ya kuanzisha familia zao. Hivyo kunaweza kusiwe na taarifa za maendeleo ya simba hao vijana, hii ni changamoto iliyopo kwa watafiti, na inabidi waje na njia nyingine bora zaidi ya kuwatafiti.
  8. Uzito wa simba, simba ana uzito mkubwa sana dume ana uzito usio pungua kilogramu 190 hadi 225, na simba jike uzito kuanzia kilogram 110 hadi 135; simba dume wana miili mikubwa kuliko majike na pia wana nywele nyingi sehemu za kifuni hizi nywele huwasaidia kujikinga dhidi wanapopambana na madume mengine wanapolinda mipaka yako na makazi yao, hivo miili yao ipo kwa jinsi hiyo kwa ajili ya ulinzi na kupigana ili kulinda familia yake. Simba jike hushika mimba na kuzaa baada ya miezi 3 na nus una huweza kuzaa Watoto kuanzia 2 hadi 6. Simba dume anaweza kuishi zaidi ya miaka 12 na jike anaweza kuishi hadi kufika miaka 20.
  9. Takwimu za simba, pamoja na nguvu na umoja walionao simba, bado ndio wanyama wanaokimbilia kutoweka kabisa hapa duniani, takwimu za miendendo ya tafiti za simba kwa upande wa Magharibi na sehemu za Afrika ya Kati, idadi inaonekana kupungua sana, inakadiriwa kuwa idadi hiyo inayokisiwa inaweza isifike hata simba 400. Hali hii inachangiwa na migogoro ya vita, uharibifu wa maeneo yao na kukosekana kwa hali ya usamala katika sehemu nyingi za maeneo hayo.
  10. Mashariki na sehemu za Kusini bara la Afrika, sehemu hizi za Afrika ambako taarifa za kitafiti zinaonyesha kuwepo kwa idadi nzuri ya simba. Lakini kuna kila dalili nyingi zinazoonyesha kushuka kwa kasi kwa idadi ya simba kwenye ukanda huu wa Afrika.
  11. Simba ni mnyama anayejulikana zaidi na kupendwa na watu wengi zaidi, watu wengi wanamchukulia simba kama alama ya ushujaa, ujasiri, nguvu na mamlaka, picha nyingi sana, vinyago na mabango mengi sana yana nembo ya simba. Filamu nyingi sana, nyumba na hata kwenye sehemu muhimu sana zina nembo ya simba. Simba amekuwa akihusishwa sehemu nyingi kama alama ya uwezo na uongozi, vitabu vingi sana vina picha za simba kuliko wanyama wowote wale. Mwandishi anasema katika jiji la London kuna picha, nembo na mapambo mengi yenye nembo ya simba kuliko simba walio hai katika Afrika Magharibi.
  12. Simba ni wanyamapori wanaoishi kifamilia, wanaishi kama ukoo au familia kwa kingereza inaitwa “pride” inaweza kuwa na familia ya simba kuanzia watatu hadi zaidi ya kumi. Katika familia hii simba dume kazi yake kubwa ni kuhakikisha familia inakuwa salama dhidi ya maadui kutoka nje, na maadui wanweza kuwa ni simba wengine ambao wanataka kumpiga dume aliyeko kwenye hiyo familia na kuua watoto wake na kuanzisha familia nyingine. Katika familia kuna mfumo na utaratibu wa uongozi na majukumu yanayoeleweka, kuna viongozi ambao ni simba dume na simba jike ambaye ndio huongoza katika harakati za kutafuta chakula, simba wengine hufuata utaratibu huo na kujifunza namna ya kuishi na kukabiliana na hatari za porini.
  13. Watoto wa simba hasa wale madume wakishakuwa na kufikia miaka miwili hadi mitatu hufukuzwa kwenye familia na kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine. Hivyo katika kipindi hiki wanachofukuzwa hutafuta madume wenzao ambao huunda kundi la madume ambao nao wanakuwa na lengo kubwa la kujihakikishia usalama, chakula na kwenda kipingana ili kupata sehemu ya kutawala na kanzisha familia.
  14. Simba wanapokuwa kwenye kundi au familia lazima kuwe na kiongozi wa familia hiyo na mara nyingi kiongozi wa familia huwa ni simba jike. Simba jike ndiye anayehusika na kupanga mipango ya kuwinda na pia kulisha familia. Simba dume ni kulinda na kuangalia usalama wa familia yake, jambo ambalo analifanya kwa ukamilifu kabisa simba dume yupo tayari hata kufa akitetea familia yake na kuiwekea ulinzi.
  15. Kundi la simba ambao ni ndugu wanaoishi pamoja huwa hawana uvumilivu sana na simba jike wengine wageni, ingawa sio mara zote huwa simba wageni wanapokuja kwenye kundi la simba wengine inatokea vita na mapigano makubwa sana na simba aliyekuja kwenye kundi la simba wengine anaweza kupigwa na kuumizwa vibaya au hata kuuliwa. Simba wakiwa kwenye familia huwa wanasaidiana hata katika mapigano na kuwafukuza simba wageni waloingia. Hii ina maana sana kwasababu ya ulinzi wa simba wengine na watoto wa simba, pia ni kuonyesha kuwa familia hiyo ni imara na simba wengine wageni au wanyama wengine wasumbufu wasijaribu kukaribia familia hiyo.
  16. Uwindaji wa simba, simba ni wanyamapori ambao ni rahisi sana kuwawinda, wale ambao wanafanya biashara ya uwindaji huwa hawatumii nguvu nyingi kumuua simba kwa sababu simba ni wanyama ambao wanaishi kwenye maeneo maalumu ambayo yana mipaka maalumu waliyojiwekea hivyo, kama kuna mtu anafahamu maneneo hayo na kumpeleka muwindaji ni rahisi sana kufanikiwa katika uwindaji wake.
  17. Uwindaji wa simba hufanyika kwa kufuata sheria maalumu za uwindaji ndani ya hifadhi ya nchi husika ambayo inatoa vibali ya uwindaji kwa wanyamapori.
  18. Vibali vya uwindaji lazima vionyeshe aina ya mnyama anayewinda, jinsia yake, umri wa mnyama huyo, na sehemu ambayo mnyama huyo atawindwa, maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya uwindaji yanaitwa vitalu au quota.
  19. Katika utalii wa uwindaji kila mnyama aliyeainishwa kuwindwa huwa na bei yake kulingana na utaratibu wa nchi ambapo kibali cha uwindaji kinatolewa.
  20. Kibali cha uwindaji kinapotolewa kwa mwindaji lazima muwindaji huyo awe na watalaamu wa kuwinda ambao wanaitwa “professional hunters, pamoja na wasaidizi wengine wa kusaidia mambo mengine ya uwindaji.
  21. Uwindaji huwa na sheria zake za matumizi ya vifaa vya kuwindia, lazima vyote vianishwe, utawinda kwa kutumia silaha gani, yenye uwezo gani nk. Silaha nyingi ambazo hutumika katika uwindaji ni bunduki na upinde pamoaja na mshale.
  22. Katika sheria za uwindaji wa mnayamapori yoyote sio weledi kabisa kumpiga mnyama unayemuwinda bila kumuua na kumsababishia maumivu makali au kumpiga mnyama sehemu ambayo atachelewa kufa. Kwa kifupi katika kuwinda hutakiwi kumjerehi mnyamapori. Na endapo umejeruhi mnyamapori unayemuwinda na kupotea inabidi umtafute kwa kila hali na kumuua.
  23. Kazi za watalaamu wa uwindaji au professional hunters ni kusaidia katika kuwinda kwa weledi kama inavyotakiwa na sheria za uwindaji wa wanyamapori, hvyo watalaamu hawa wanajua kabisa maeneo yote muhimu ambayo wakimpiga mnyamapori atakufa bila kumsababishia mnyamapori huyo maumivu au majereha. Pia ni kwa ajili ya biashara ya mteja wake, endapo mnyamapori atapigwa hovyo hovyo atakuwa ameharibu nyara ambayo mwindaji aliyetoa fedha anataka, hivyo suala la uwindaji linahitaji uelewa wa kutosha pamoja na utalamu katika kulitekeleza.
  24. Uwindaji wa simba una faida na hasara zake nyingi tu, kama ilivyoainishwa katika kitabu hichi tunachokichambua mtafiti Andrew ameonyesha namna ambavyo uwindaji una faida na hasara katika mfumo wa uchumi na ikolojia ya wanyamapori hawa jamii ya paka. (simba ni mnyama ambaye yupo kwenye wanyama jamii ya paka, wengine ni chui, duma na chui mwenye milia au tiger)
  25. Faida za uwindaji wa simba ni mapato wanayotoa wageni ambao wanataka kumuwinda mnayama huyo, mapato hayo unaweza kuyaona ni mengi na kweli ni mengi kwa mahitaji ya maisha ya mtu wa kawaida na unawea kuyatumia kufanya vitu vya maana; lakini ukilinganisha mapato hayo na gharama za uhifadhi wa mnayamapori huyo tangu anapozaliwa na kuwa mnyama anayefaa kuwindwa utaona ni fedha ndogo sana.
  26. Fedha ambazo makampuni ya uwindaji yanatoa na kusema wanasaidia katika uhifadhi wa wanyama hao pamoja na kusaidia maisha ya watu wanaoishi pembezoni mwa hifadhi za zenye wanyama hawa hazijawahi kuleta matokeo mazuri sana kwa sababu ni kaisi kidogo sana na hikwezi kugawanywa kutoka serikali kuu na kuwafikia watu wanaoishi kwenye maeneo hayo ambao ndio wahanga wa wanyamapori hawa.
  27. Sheria za uwindaji wa simba zinataka mwindaji kuwinda simba dume ambaye ameshakuwa mzee zaidi ya miaka 6, lakini sheria hii inaweza kutekelezwa kama inayotakiwa? Utafiti wa wanyama hawa unaonyesha kuwa simba hao wanao windwa katika umri huo wana nafasi kubwa sana katika familia au kundi la simba walio baki. Kazi ya simba dume ni kuilinda familia yake dhidi ya hatari ambao zinaweza kuharibu wanafamilia.
  28. Kundi la simba linaundwa na wazazi, vijana, na watoto, na hata mashangazi, linaweza kuwa ni kundi kubwa la simba ambao wanategemea sana ulinzi wa simba dume ili waendelee kuishi. Sasa fikiria mwindaji anakuja na hajui chochote kuhusu maisha ya kifamilia waliyonayo simba hao na kuua simba dume ambalo ndio tegemeo la familia nzima ya simba, kitakachotoea ni familia kusambaratika, wengine watakufa hasa watoto na simba wengine ambao bado hawajawa wazoefu kwenye mambo mengi yanayotegemea familia.
  29. Hata hivyo uwindaji wa simba jike una madhara makubwa sana kwa familia nzima ya simba, wawindaji wanapotaka kuwinda simba jike wanakuwa na ufahamu kidogo sana kwani wengi wanakuwa na mihemuko ya kufapa fedha nyingi hivyo kutojali kitakachotokea baada ya kumuua simba jike. Unaweza kufikiria hivi, mara zote wanaotafuta chakula na kufundisha wengine kuwinda ni simba jike, na simba jike anayewinda wanyama wingine kwa ajili ya familia anakuwa na uzoefu wa kufanya hivyo kwa muda mrefu, sasa ikitokea ameuwawa unafikiri nini kitatokea kwenye familia yake iliyobaki? Moja kwa moja itaathiri sana uwepo wa simba waliobaki kwenye familia ambao hawana uzoefu wa kutosha katika uwindaji au utafutaji wa chakula.
  30. Wawindaji wanaweza kuona wana haki ya kufanya uwindaji na kuua simba yoyote mkubwa kwenye kundi, lakini hawajui ni hasara gani au ni hali gani ambayo wanaiacha kwa simba wengine waliobaki kwenye kundi. Utafiti wa miaka zaidi ya 20 uliofanywa na Andrew pamoja na timu yake unaonyesha wazi kuwa uwindaji wa simba una madhara na hasara kwa simba wengine waliobaki, ambao wanaweza kufa au kupotea kabisa.
  31. Kwasababu ya tabia ya simba kuishi pamoja hii ndio imekuwa nguvu yao na usalama wao wawapo porini, kitendo cha kuua wategemezi kwenye familia inapelekea simba wengine kupoteza mwelekeo na kutawanyika kabisa. Katika hali za namna hii simba wanapo tawanyika na kuanza kutafuta chakula na makazi mapya na makundi ya simba wengine hali hii inasababisha kuvuka mpaka na kuingia kwenye makazi ya watu na kusababisha madhara kwa wafugaji na pia kwa maisha ya watu.
  32. Mwanzo wa migogoro unaanza na jamii inajenga chuki dhidi ya wanyama hawa, kitakachotokea wanyama hawa wanaingia kwenye kundi au orodha ya wanyama wasumbufu katika jamii. Jamii itaanza kulalamika na kuomba namna ya kuwaondoa simba hao, au jamii inaweza kujchukulia sheria mkononi na kanza kuwawinda simba hao na kuwaua kwa mikuki au kuwawekea sumu.
  33. Jamii inawapenda sana wanyama hawa endapo tu watabakia kwenye maeneo yao bila kuvuka mpaka na kuingia kijijini. Sehemu nyingi sana za Afrika wanyama hawa wamekufa kutokana na kuvuka mpaka na kuingia kwenye maeneo ya Kijiji na kusababisha hasara, wengi wameuwawa kwa sumu, wengine kwa kupiwa mishale na mikuki nk.
  34. Sheria za uwindaji zinatakiwa kurejelewa tena kwa kuangalia gharama za uhifadhi wa wanyama hawa na kiasi ambacho wanatoa wawindaji ili kuwawinda wanyama hawa.
  35. Gharama za uhifadhi wa simba ni kubwa sana, inajumlisha gharama za uhifadhi wa mazingira yake asilia, gharama za kuhifadhi wanyama ambao wanaliwa na simba ambao ndio chakula cha simba, gharama za utafiti na ufuatiliaji wake, gharama za kuzuia madhara mabaya kama vile mioto isiyokusudiwa, magonjwa na gharama za kuajiri maaskari kwa ajili ya doria na uhifadhi kwa ujumla.
  36. Kwa utafiti ulofanyika maeneo mengi ya Afrika unaonyesha gharama za uhifadhi kwa kilomita moja ya mraba kwa mwaka ni dola 500 sasa hi dola 500 ni ka kilomita za mraba moja tu, sasa chukulia hifadhi ina kilomita za mraba 20,000 au 14,000. Kwa ukubwa huo wa hifadhi zetu, na unakuta nchi kama Tanzania ina maeneo mengi sana makubwa kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori, kwa kweli sio gharama ndogo hata kidogo.
  37. Sasa tuje kwa simba, simba anaweza kuishi hadi zaidi ya miaka 12, na simba ana uwezo wa kutembea kwa siku zaidi ya kilometa 6, ukichukua kilomita hizo zidisha kwa mwezi na mwaka na mwaka na pia zidisha kwa umri anaoweza kuishi utapata ni mamilioni ya shilingi. Sasa chukulia huyo simba ametembea kilomita 500 kwa mwaka zidisha na gharama ya kila kilomita halafu zidisha tena kwa umri wake utapata mamilioni ya dola. Sasa huyo ni simba mmoja
  38. Gharama hizo ni kwa nchi nyingi za Afrika, sasa kwa nchi za wenzetu kama Marekani gharama za uhifadhi wa simba mmoja kwa kilomita moja ya mraba n idola 2,000 sasa zidisha hizo hela kwa kilomita alizotembea simba huyo ndani ya hifadhi kwa mwaka, halafu uzidishe na umri wasimba huyo hadi anafikia wakati wa kuuwawa, utapata ni mamilioni ya dola.
  39. Mfano mzuri ni kifo cha simba maarufu sana aliyeuwawa mwezi June mwaka 2015 katika hifadhi ya taifa ya Hwange nchini Zimbabwe, simba huyo alijulikana kwa jina la Cecil. Simba huyu alikuwa amefungwa kola na alikuwa anafuatiliwa mienendo yake na watafiti wa mradi wa utafiti wa simba katika hifadhi ya Hwange. Cecil aliuwawa kimakoosa na muwindaji aliyejulikana kwa jina la Walter Palmer ambaye ni daktari wa meno lakini pia ni mwindaji tajiri sana.
  40. Walter alifanya makosa makubwa sana kwa kumuua Cecil ambaye alikuwa kipenzi cha watalii na wageni wengi waliotembelea hifadhi ya Hwange. Tafiti zinaonyesha Cecili alipigwa picha zadi ya laki moja na wageni, hata wanakijiji walimfahamu sana simba huyu, hivyo walimpenda na akawa kivutio kikubwa sana katika hifadhi hiyo.
  41. Cecili aliuwawa akiwa na miaka 12, na aliuwawa na huyo mwindaji daktari wa meno ambaye alitumia upinde na mshale kumuua Cecil, mbaya zaidi Cecili hakuuwawa kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwindaji, hivyo aliuwawa kimakosa. Licha ya Walter kupewa leseni na kibali cha kuwinda simba kwenye hifadhi hiyo hakufuata masharti ya leseni yake, pia inaonyesha kwa watalaamu wake aliowapata katika hifadhi hiyo walifanya makosa makubwa sana kuwa kumruhusu kuwinda eneo ambalo haliruhusiwi kabisa.
  42. Walter alitoa dola 50,000 za kimarekani kwa ajili ya kupata kibali cha kuwinda na akaishia kumuwinda simba ambaye anapendwa na watu wengi, jambo alilolifanya lilimdhalilisha sana, magazeti mengi ya Ulaya na Marekani yaliandika habari za kuuwawa kwa Cecili na mwindaji katili kabisa, mitandao ya kijamii ilimshambulia sana Walter, alipelekwa mahakamani, alifikia hatua akahama hadi nyumba aliokuwa anaishi huko Menesota nchini Marekani na kwenda kujificha hadi hali ilipotulia kidogo mwaka 2016. Hata hivyo kitabu tunachokichambua leo ni matokeo ya gumzo lililotokea duniani baada ya kifo cha Cecil. Silaha aliyoitumia ya upinde na mshale kumuua Cecil ilikuwa njia ya mateso sana, wasaidizi waliokuwa pamoja na Walter wanasema kuwa Cecil alipigwa mshale na kukimbilia porini kujificha na hakufa, kitendo hicho kilisababisha Cecil kupoteza damu nyingi sana kwa muda wa zaidi ya masaa 13, hiyo watu waliona ukatili huo alioufanya Walter wa kumuua Cecil.
  43. Watafiti wa simba katika hifadhi ya Hwange walipiga mahesabu ambayo yanatufungua macho kuhusu uhifadhi na gharama zake pamoja na mchango wa uwindaji katika hifadhi zetu. Walter Palmer alioa dola 50,000 kumuua cecil, cecili aliishi miaka 12, na anakadiriwa kutembea zaidi ya kilomita za mraba 500 katika hifadhi hiyo, na gharama za uhifadhi wake katika hifadhi hiyo kwa kilomota moja ya mraba ni dola 2,000. Ukizidisha gharama za uhifadhi kwa mwaka na kilomita za mraba kwa mwaka utapata kwa mwaka mmoja, utapata dola milioni 1, ambazo zilitumika katika uhifadhi wa simba huyo, sasa tunajua aliishi miaka 12, hivyo chukua dola milioni moja na uzidishe kwa miaka 12 aliyoishi hadi anauwawa utapata ni dola milioni 12.
  44. Sasa yeye alitoa dola 50,000 na kwa haraka unawea kuona ni nyingi, lakini hazina manufaa makubwa kama kuwepo hai kwa simba huyo. Makampuni ya uwindaji yanapata faida sana katika biashara hii ya uwindaji, hasa kama mnyama aliyewindwa ni mkubwa kama cecil. Katika hali ya kawaida endapo manayama anakwenda kuuzwa kwenye makampuni ya uwindaji ni zaidi ya dola 100,000 kwa simba mmoja. Hivyo wanapata faida kubwa sana kulinganisha na kiasi wanachotoa kumuua huo simba.
  45. Aidha, kuuwawa kwa simba dume Celili kikatili kwa ajili ya mambo ya kujifurahisha sio tu kumeleta faida ndogo kiuchumi, lakini pia cecil ni dume la simba ambalo lilikuwa na familia kubwa sana ambayo yeye kama baba alikuwa anahakikiha ulinzi na usalama wa kila wanafamilia. Kuuwawa kwa cecili kumesababisha kusambaratika kwa familia yake na kupoteza matumaini kwa simba wengene waliobaki kwenye kundi hilo ambao walikuwa wanamtegemea cecili kama kiongozi na mlinzi wao.
  46. Kifo cha simba Cecil kiliibua mijadala mingi sana sehemu mbali mbali duniani watu walilaani na kumchukia sana mwindaji Walter. Mwaka 2016 katika gazeti maarufu nchini marekani the Times liliandika kuwa Simba Cecil amekuwa mnyama wa kwanza kati ya wanyama maarufu sana 100 duniani, makala nyingi sana zilandika kuhusu simba huyo, kuuwawa kwa Cecil kuliifanya dunia kufikiri kwa kina kuhusu uwepo wa simba na uhifadhi wake.
  47. Kuna watu wengi duniani hawajui kama kuna biashara ya uwindaji wa simba barani Afrika, baada ya kifo cha Cecil ndipo wakafahamu kuwa sehemu nyingi za nchi za Afrika kuna utoaji wa vibali vya uwindaji wa simba. Afrika, uhai wa wanyamapori wetu unategemea sana namna tunavyo wachukulia na kuwaona.
  48. Jambo la kuuwawa kwa Cecil linatupa kufahamu kwa kina kuwa watu wanapenda sana wanyamapori haswa simba, wanapenda kuwaona wakiwa hai, hata makampuni makubwa ya utalii na uwindaji wanakubaliana na hilo. Hapo ndipo tunapotakiwa kushirikiana katika uhifadhi wa wanyama hawa, sio jambo la nchi moja ni dunia nzima.
  49. Picha ambayo ipo kichwani kwangu ni hii, wawindaji hawa amabao wanakuja kwenye hifadhi zetu na kutoa vihela kidogo wanaua wanyama wetu wa thamani ili kwenda kuweka kama mapambo katika majumba yao ya kifahari wanapewa heshima kubwa sana katika nchi zetu za Afrika. Hakuna vitu vya maana sana ambavyo vinaweza kuhalalisha uwindaji kuwa jambo muhimu sana endapo hatutabadili jinsi tunavyozichukulia rasilimali zetu.
  50. Kwa upande mwingine mwananchi masikini ambaya anaishi kando ya hifadhi za wanyama hawa anapoingia porini ili kujipatia mnyama mdogo kwa ajili ya chakula na virutubisho vingine muhimu kama protini anapokamatwa anaishia kupigwa vibaya, kufungwa jela na hata kuwawa. Ikumbukwe mtu huyu anatafuta wanyamapori kwa ajili ya mahitaji muhimu kama chakula nk. Lakini mara nyingi akikamatwa anachukuliwa kama jambazi au jangili hivyo maisha yake yanakuwa hatarini.
  51. Kwa kusema hivyo sio kwamba nahalalisha jamii kuingia porini na kuwinda wanyama kama chakula, la hasha, tunatakiwa tubadili mitazamo yetu na sera zetu ili mwananchi ambaye ndiye mhanga wa wanyama hawa aone faida kubwa ya uwepo wa wanyamapori hawa kuliko kuingia porini na kuanza kuwinda. Tunawapa heshima wawindaji wakubwa na makampuni yao kwa kuwa ni watu matajiri na wanaotoa fedha; lakini wengi hawajui chochote kuhusu gharama ambazo watu na nchi yetu inaingia katika uhifadhi wa wanyamapori.
  52. Nimejifunza jamii zetu hasa zinazoishi kando ya hifadhi za wanyamapori ni wavumilivu sana na wamekuwa wakivumilia hasara kubwa sana zinazoletwa na wanyamapori walio karibu yao. Kama ni wakulima wanapata hasara kwa tembo au wanyama wengeni wanaokula majani kuharibu mazao na mashamba yao, kama ni wafugaji wanapata hasara kwa simba na wanyama wengine kama fisi, duma na chui kula mifugo yao. Kwa haraka mzunguko mzima na mtazamo walionao ni hasara kubwa kuliko faida. Tunatakiwa kubadili sera na sheria zetu kwenye eneo hili la uwindaji na uhifadhi kwa ujumla ili manufaa makubwa yabaki kwa wananchi waishio maeneo yaliyo karbu na wanyamapori.
  53. Licha ya hayo, kuna changamoto nyingine nyingi wanazokutana nazo simba wawapo porini hasa kwenye maeneo yao, utafiti wa Andrew ulionyesha namna simba wengi walivyokamatwa na mitego ya majangili iliyotegwa kwa lengo la kuwakamata wanyama wengine. Mitego hii ipo maeneo mengi sana kwenye maeneo ya wanyamapori na inawakamatwa hata wanyama ambao hawajakusudiwa, kwa kweli simba wengi wanaokamatwa katika mitego hiyo sio rahisi kupona na kuendelea na maisha yao.
  54. Mambo haya kama hayatachukuliwa kwa uzito wake tutakuja kushuhudia anguko kubwa kwa wanyama hawa wazuri ambao wana mchngo mkubwa kwa mfumo mzima wa maisha yetu na maisha ya wanyamapori wengine.
  55. Mara nyingi sana kwa nchi masikini ambazo zina wanyamapori ni nadra sana kuona uhifadhi ikiwa katika ajenda kuu za nchi. Nchi nyingi masikini hazina mahitaji muhimu kwa ajili ya kusaidia maisha ya wananchi wake yawe bora. Hivyo kutakuwa na ajenda nyingi sana za kuleta na kuharakisha maendeleo, ambazo ndizo hutengewa fedha nyingi za kuendesha sekta hizo, mfano ni sekta ya afya, elimu, kilimo na sekta ya miundombinu.
  56. Kwa changamoto za kiuchumi ambazo zinawagusa wananchi wengi imekuwa ndio msingi wa siasa za viongozi wengi wa nchi masikini, watatumia changamoto hizo kama mtaji wa kupata uongozi na nafasi nyingine za juu kwenye serikali. Hivyo hata wakati wa kupitisha na kuandaa bajeti za maendeleo ni bajeti kiasi kidogo sana zinazoelekezwa kwenye kukuza uhifadhi na mazingira asilia ya wanyamapori.
  57. Hata hivyo, nchi nyingi masikini hupata misaada kuoka nchi tajiri ambazo watu wake wana vyanzo vingi na vya uhakika vya kipato hivyo hutoa kodi kubwa na kutosheleza mambo yote muhimu kwa wananchi wake, tofauti na nchi masikini ambazo zikipata misaada hiyo hugawanywa sana na kufanya isitoshe hata katika uwekezaji wa sekta mbazo ni muhimu zaidi.
  58. Katika ombwe hilo, ni vigumu sana kwa viongozi wakuu wa nchi masikini kutilia umakini na uzito unaotakiwa kwenye masuala ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira. Hivyo kuhangaika na mambo mengine ambayo yanaleta faida za haraka na kutatua changamoto nyingi za wananchi.;hivyo kwa kuwa jambo la namna hiyo halipo kwenye akili na ajenda za viongozi wakuu, maswala ya kuwekeza katika uhifadhi endelevu linachukua muda sana hadi kuja kuleta faida tarajiwa.
  59. Kama hakuna uwekezaji maana yake hata ufuatiliaji haupo, na kama kuna uwekezaji mkubwa pia ufuatiliaji mkubwa unakwepo. Kwa kukosekana kwa mambo hayo katika nchi masikini kumesababisha udhafu katika usimamizi wa sheria, na ufuatiliaji wa mambo muhimu kama ya utafiti na uhifadhi wa wanyamapori.
  60. Kwasababu ya udhaifu huo, maliasili zetu muhimu zimekuwa zikipeperushwa na ndege, meli, magari na bandari zetu, viwanja vyetu vya ndege na barabara zetu zimekuwa njia za zikisafirishia maliasili zetu muhimu kwenda kwa matajiri wakubwa kwenye nchi za nje. Hii ndio sababu katika nchi masikini ujangili wa wanyamapori umekithiri sana. Hadi nchi hizi masikini zije kuwa sawa na kuamua sasa zinawekeza vya kutosha katika sekta hii, inaweza isitokee au inaweza kuja kuwa tumeshachelewa sana.
  61. Labda hii ndio sababu ya baadhi ya nchi ambazo zinataka kutoa misaada kwa nchi masikini zenye wanyamapori huwa na masharti yao kuwa misaada hiyo iende moja kwa moja katika uhifadhi wa wanyamapori. Kuna miradi mingi sana ya uhifadhi wa wanyamapori, miradi hii ina lengo la kuhakikisha inawekeza katika utafiti na kutoa faida kwa jamii kupitia uwepo wa wanyamapori. miradi hii ni muhimu kwa sababu kama tunashindwa kuwekeza kwa sababu ya uhaba wa fedha na vifaa tushirikiane na wadau wa maliasili ili kwa pamoja tutatue changamoto katika eneo hili muhimu.
  62. Historia za wanyama wanaokula nyama kama kanivora wakubwa zinasikitisha sana, mitazamo ya watu na kutokujua umuhimu wa wanyama hawa katika mfumo wa ikolojia kumechangia idadi kubwa sana ya wanyama hawa kuuwawa; historia inaonyesha kwa miaka ya nyuma watu wengi waliona hawa kanivora hasa simba ni wanyama katili na waonevu sana wanaua wanyamapori wenzao bila huruma, hivyo wakaonekana hawana faida, kilichofuata hapo ilitungwa sera ya kuwaangamiza wanyama hawa wanaokula nyama katika maeneo yao yote ya hifadhi. Mfano mwaka 1902 hadi mwaka 1960 sheria ya kuua kanivora hasa simba ilishika hatamu huko Afrika ya Kusini katika hifadhi kubwa na maarufu ya Kruga. Utafiti unaonyesha zaidi ya simba 3,031 waliuwawa vibaya sana, wengine walipigwa risasi, wengine walitegwa mitego, na wengine waliuwawa kwa kuekewa sumu.
  63. Bara la afrika ndio sehemu pekee duniani iliyobaki na paka hawa wakubwa, yaani simba. Lakini kuna sehemu nyingi sana za Afrika simba wametoweka kabisa, hasa maeneo ya Afrika ya Kati na Afrika Magharibi. Tafiti nyingi zinaonyesha idadi ndogo sana ya simba 400 katika sehemu hii ya Afrika.
  64. Simba ni wanyama wanaomiliki na kutembea maeneo makubwa, hivyo wanahitaji maeneo makubwa kwa ajili ya uhifadhi wao. Uharibifu wa mazingira asilia ya wanyamapori imekuwa ni tishio na chanzo kikuu cha kuendelea kupungua kwa idadi ya simba sehemu nyingi duniani.
  65. Afrika ni bara ambalo linakuwa kwa kasi kwa aidadi ya watu, kuongezeka kwa watu kunaenda sambamba na kuongezeka kwa mahitaji yao, hivyo makazi, maeneo ya kulima, ujenzi wa miundombinu muhimu kama barabara, reli, viwanja vya ndege nk vinahitaji maeneo makubwa kwa ajili ya uanzishwaji wake, hivyo hakuna jambo dogo linaloweza kufanyika katika ardhi ya Afrika lisiguse maeneo ya wanyama hao.
  66. Afrika ni bara ambalo linakabiliwa na migogoro mingi ya vita, ugaidi na kukosekana kwa hali za kiusalama baadhi ya maeneo. Endapo hali za kiusalama hazitakuwepo, kukawa na vita vya mara kwa mara, hasa vita vya wenyewe kwa wenyewe, halii hii itadhoofisha sana utekelezaji wa shaera na usimamizi kwenye maeneo mengi kutakuwa dhaifu na hapo ndipo ujangili, rushwa na ubadhrifu hushamiri sana. Sehemu za Afrika ya Magharibi mambo haya yanatajwa kuwa ndio chanzo cha kuendelea kuporomoka kwa idadi ya simba.
  67. Afrika kuna baadhi ya imani na mitazamo ya watu kuhusu simba, kuna watu wanasema kuna “simba watu”. Katika maeneo ya hifadhi ya Hwange ambapo utafiti huu ulifanyika kuna watu wanahusisha matatizo na balaa wanazokutana nazo kama adhabu kwa miungu yao. Ikitokea simba ameua na kula mtu zaidi ya mmoja wanaotoka katika familia moja au ukoo mmoja inasemekana kuwa ni adhabu ya miungu kwa mtu huyo au familia hiyo. Hii inaweza kuleta manufaa au madhara zidi kwa simba, anaweza kuuwawa au kuachwa kama ishara ya miungu au roho za miungu.
  68. Katika kipindi cha miaka ya 1940 mpaka 1950, nchini Tanzania katika mkoa wa Njombe imeripotiwa zaidi ya watu 1,500 waliliwa na simba. Katika kipindi hicho cha miaka 10 watu wengi walipoteza maisha kwa vipindi tofauti tofauti. Watafiti wanasema sio kwamba inaokea tu simba kuanza kula watu ila katika kipindi hicho idadi kubwa sana ya wanyama wanaokula majani ambao wanaliwa na simba walikufa sana kutokana na kushamiri kwa ugonjwa unaoitwa rinderpest, ni ugojwa mbaya sana uliowashika hao wanyama. Hii ndio ikawa sababu ya simba hao kuhamia kwa watu na kuanza kuwala hadi pale walipouliwa kwa kupigwa risasi na mwingereza George Rushby.
  69. Hali kama hii imetokea tena kwa nchi ya Kenya katika miaka ya 1898 wakati wa ujenzi wa reli kutoka Nairobi hadi Mombasa, katika kipindi hicho inaripoiwa watu zaidi ya 135 walipoteza maisha yao kwa kuliwa na simba. Hii ni kwasababu ujenzi wa reli hiyo ulikuwa unapita katika hifadhi ya taifa ya Tsavo ambayo ilikuwa na simba wengi sana. Pale ambapo simba wanapokutana na binadamu lazima uharibifu utokee.
  70. Utafiti uliofanyika kusini mwa Tanzania miaka ya 1990 hadi mwaka 2005, unaonyesha hali hii ikijirudia tena, katika kipindi hicho takwimu zinaonyesha watu zaidi ya 550 walipoteza maisha yao kutokana na kuliwa na simba. Hali hii pia ilichangiwa sana na kukosekana kwa wanyama walao majani ambao wanaliwa na simba (prey).
  71. Matukio ya watu kuliwa na simba Kusini mwa Tanzania miaka ya 2002 hadi 2004 yanaonyesha pia zaidi ya watu 35 walipoteza maisha yao katika vijiji vinavyozunguka mto Rufiji. Hali ambayo ilipelekea watu wengi kuhama makazi yao na kukimbilia mjini. Chanzo cha watu kuliwa na simba kwenye maeneo haya imeripotiwa kuwa ni kupungua kwa wanyama wanaoliwa na simba. Tafiti za kina zinaonyesha katika maeneo haya kulikuwa na nguruwe pori wengi sana wanawasumbua wakulima hasa wakati wa usiku. Hivyo ililazimika watu kulala mashambani kwa ajili ya kulinda mazao hayo. Na kwakuwa hakuna wanyama wanaoliwa na simba, simba walikuwa wanawawinda ngurue hao wakati wa usiku, na hapo ndipo watu walipokutana na simba na kuishia kupoteza maisha yao. Katika maeneo hayo simba aliyekuwa anakula watu walimuita Osama kwasababu ya madhara yake.
  72. Tukienda kusini mwa Afrika karibu na nchi ya Zimbabwe ndio tunatembea umbali wa kama kilomita 350 hivi kufika nchi ya Msumbiji. Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka ya 1960 hadi 2005, wakimbizi wengi waipoteza maisha yao kwa kukimbia mapigano katika nchi ya Msumbiji. Wakati watu wakiikimbia nchi yao na kwenda katika nchi za jirani kama Afrika ya Kusini walilazimika kupita kwenye maeneo ya hifadhi ya wanyama na hapo ndipo mauaji mbaya sana yanakisiwa kufanywa na simba. Idadi ya watu hao ni 13,380 ni watu wengi sana waliopoteza maisha kutokana na kuwawa na simba. Lakini pamoja na idadi hiyo kuwa kubwa hakuna mtu anayeweza kuthibitisha kuwa ni kweli kwa sababu inawezekana imezidi au ni chini ya hiyo, maana sio rahisi kuingia hifadhini na kuanza kuhesabu watu waliouwawa unaweza usione kitu lakini pia ni hatari.
  73. Utafti wa kina wa uliofanywa na timu ya utafiti kutoka katika mradi wa utafiti wa simba katika hifadhi ya Hwange huko Zimbabwe imeonyesha kuwa ili simba awe hai na aweze kuendelea na maisha yake anahitaji kula angalau kilo tano hadi 8 za nyama kila siku, ambayo ni sawa na kilo 3,000 za nyama kwa mwaka ambayo ni sawa na makadirio ya kula nyumbu 13 kwa mwaka au nyati 5 kwa mwaka.
  74. Tukibakia kwenye tafiti hizo, kundi la simba au familia ya simba moja inahitaji angalau nyumbu 150 kila mwaka kwa ajili ya chakula ili waishi, nyumbu hao 150 ni sawa na kilo 30,000 za nyama kila mwaka ili kuishibisha familia moja ya simba. Simba huwa wanapendelea kuua wanyama wakubwa ambao watatosha kula na familia yao, hivyo wanyama wanaowindwa sana na simba ni pundamilia, nyumbu, twiga, na nyati.
  75. Kwa kuwa simba wanawategemea sana wanyama hao prey kama chakula ili waendelee na maisha yao, hii inatupa kujua kuwa uwepo wa wanyamapori wanaoliwa na simba ni muhimu kama tunataka kuwahifadhi simba kwa muda mrefu. Uhifadhi unatakiwa kuangalia sehemu zote hizo kwani kupungua kwa prey ndio kupungua kwa simba, hivyo basi mipango yetu ya uhifadhi ianatakiwa iangalie sehemu zote hizo.
  76. Shughuli ya kuwinda ili wapate chakula cha kuwatosha familia nzima sio kazi ndogo, uwindaji ni hatari sana, simba wengi wameumizwa vibaya wakiwa wanawinda, wengi hawana meno, wengi wana makovu vifuani,wengine wana vilema vya kudumu wengine wameharibiwa sura zao usoni na hata kuvunjika baadhi ya seemu muhimu za miili yao. Hii ndio sababu wanatumia akili na ujanja mwingi kuwinda wanyama, wakati wa kiangazi simba wengi hukaa maeneo ambayo yana mashimo ya maji kusubiria wanyama waje kunywa maji ili wawakamate na kwa njia hiyo wanafanikiwa sana.
  77. Utafiti unaonyesha sehemu nyingi ambazo hakuna wanyama wanaoliwa na simba halafu kuna simba wengi kumekuwa na habari nyingi za simba kula watu. Inaonyesha pia simba wanaweza kuvumilia kwenda zaidi ya wiki mbili bila kula chochote. Maeneo yote yaliyoripotiwa kuwa na changamoto hizi za watu na simba chanzo ni kukosekana kwa mahitaji muhimu ya simba ili waweze kuishi.
  78. Bila tafiti za kina kuhusu simba, jamii itakuwa na picha mbaya kuhusu wanyama hawa, watawaona ni wanyama wasumbufu, waharibifu, wanaoua watu, wanyama katili na wasio na umuhimu kwenye jamii. Lakini tafiti zikifanyika za kutosha kuhusu tabia zao, miendendo yao na maisha yao kwa ujumla kutakuwa na sababu nyingi sana za kuiambia jamii kuhusu uzuri wa wanyama hawa. na jamii itaelewa kwanini simba anakuwa na tabia fulani au kwanini simba anakula watu. Hatuwezi kutoa majibu mepesi kwenye mambo mazito kama tuliyoyataja hapo juu kama hakutakua na utafiti wa kina kuhusu simba. “Wanasema kama hujafanya utafiti huna haki ya kusema”.
  79. Watafiti wa simba kila wanapojifunza tabia za wanyama hawa wanagundua vitu vingi ambavyo havionekani kwa urahisi. Kwa mfano kuna simba aliyepewa jina la DB au David Backam aliyekuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Uingereza, watafiti walimpa simba huyo jina hilo kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kutembea kilomita nyingi kuliko ilivyotarajiwa. Kwa kumfunga kola ya sateliti simba ni rahisi kuona umbali aliotembea kwa siku kadhaa. Na waligundua tambia ya ajabu sana na uwezo alio nao simba kutembea umbali mrefu kiasi hicho kwa siku chache tu.
  80. Simba huyo aliyetembea umbali mrefu kiasi hicho baada ya kufukunzwa kwenye familia ili aende kujitegemea na kuanzisha familia yake, simba huyo alipofukuzwa aliamua kwenda mbali sana kiasi cha kuvuka mpaka wa nchi na kuingia hifadhi nyingine kwenye nchi ya Zambia. Tabia hii ya simba kuwaondoa madume vijana ambao wamefika umri wa kujitegemea na kwenda kuanzisha familia zao ni tabia muhimu sana katika mfumo wa maisha na kiikolojia.
  81. Kuepuka kuzaliana au kuanzisha familia na simba wa karibu ambao wanaweza kuwa ni ndugu kuna madhara yake na simba wanafahamu hilo, hivyo huchukua hatari ya kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta simba wengine tofauti kabisa na kuanzisha familia huko, na hilo ndio jambo ambalo simba anaweza kulifanya bila kujali ni hatari gani atakutana nazo katika safari hiyo ya maisha mapya.
  82. Kiafya sio vizuri ndugu kwa ndugu kuzaliana, na hilo ndilo simba hawataki litokee kwao, madhara ya familia ya karibu kuzaliana ni makubwa na yanasababisha uzazi dhaifu wa simba, na pia ni rahisi kushambuliwa na magonjwa endapo simba mmoja atakuwa na magonjwa atawwambukiza wengine kirahisi.
  83. Mfano ulio wazi ni simba ambao wapo katika hifadhi ya eneo la Ngorongoro hapa Tanzania, simba hao ambao wapo chini ya kreta ya Ngorongoro, kuna ukuta wa kreta ambao unawazuia simba hao kutoka kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya kuanza familia na simba wengine tofauti. Taarifa za kitafiti kutoka katika hifadhi ya bonde la Ngorongoro zinaonyesha kuwa simba waliopo pale wanakabiliwa na tatizo la uzazi kutokana na kuzaliana ndugu kwa ndugu.
  84. Kwa mantiki hiyo ni kwamba, simba wanatembea sana kutembea huku ndiko kunakuwaletea mafanikio au kifo kwa maisha yao. Firikira simba anaanzisha familia yake karibu nae neo la kijiji na kuna mifugo maeneo ya karibu, kitakachofuata hapo ni migogoro isiyoisha ambayo inaweza kupelekea kundi lote la simba kuwa hatarini. Hii inatupa kujua na kufahamu kuwa uhifadhi wa maeneo ya wanyamapori una maana kubwa sana kwa wanyama kama simba ambao huitaji eneo kubwa kwa ajili ya maisha yao. Hivyo mipango ya kupunguza punguza na kuharibu maeneo ya hifadhi za wanyama ambayo yana simba inabidi iangaliwe tena na kubadilishwa ikiwezekana.
  85. Jambo jingine kubwa la kujifunza katika tabia hiyo ya kutembea umbali mrefu hasa kwa simba vijana ni kusaidi kutoa miongozo kwa watalamu na wasimamizi wa wanyamapori kuhifadi njia na ushoroba au kama inavyojulikana kama “corridor” ambazo ni njia za wanyamapori ambazo zinaunganisha hifadhi moja na nyingine. Maeneo kama ushoroba yanaonekana kutothaminiwa sana lakini ni muhimu sana katika kutunza ikolojia za wanyama na maisha yao kwa ujumla.

Nimalizie makala hii ndefu yenye mambo mengi na ya msingi kuhusu simba, maisha yao na changamoto zinawakabili. Ukweli ni kwamba suala la uhifadhi wa wanyamapori katika bara la Afrika halikuwa sera ya waafrika, hasa uwidaji wa simba na wanyamapori wengine. Baada ya ukoloni kuingia Afrika ndio waliingia na kukaa maeneo bali mbali ambayo mengi yaligeuzwa kuwa mashamba makubwa, miji mikubwa nk. Maeneo hayo mengine yalikuwa ni sehemu muhimu za wanyamapori kama simba.

Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya ndio wakaamua kuyatenga maeneo hayo kwa ajili ya shughuli za uwindaji, maeneo yaliyotengwa waliyaita “game reserves” ambayo yalikuwa kwa ajili ya uwindaji. Hadi kufikia sasa maeneo mengi ambayo ni game reserves sasa yamebadilishwa na kuwa hifadhi za taifa, hii ilifanyika baada ya kupata uhuru.

Hata hivyo katika kipindi hicho cha ukoloni waliokuwa na haki ya kuwawinda wanyama wakubwa kama simba ni familiza za kifalme, na watu matajiri sana. Hii ndio inaendelea hadi sasa, kwasababu Afrika kuna shida na hakuna fedha za kuendesha shughuli za maendeleo makampuni makubwa ya uwindaji hutoa fedha nyingi na kuingia kuwinda wanyamapori wetu. Ikumbukwe pia sera na sheria nyingi za usimamizi wa wanyamapori tulizo nazo ni matokeo ya utawala na sheria nyingi za kikoloni.

Nashauri sana serikali zetu kupitia tena sheria na sera za uwindaji na uhifadhi wa wanyamapori, uhifadhi una gharama sana kuliko fedha kodogo wanazotoa wawindaji wa kitalii, hata hivyo miaka ya hivi karibuni kuna sera imepitishwa kwa wale wanaotaka vibali vya uwindaji hapa Tanzania, kuvipata vibali hivyo ili wameliki vitalu vya uwindaji inafanyika kwa njia ya mnada; kila kitu kipitiwe na kuangaliwa tena ili uhifadhi uwe na manufaa makubwa.

Rafiki yangu, mambo yote nilikushirikisha ni baada ya kusoma kitabu hiki muhimu pamoja na taarifa nyingine na uzoefu kidogo nilio nao katika utafiti wa wanyamapori. ni kitabu kizuri sana ambacho nashauri kila mtu apate na kukisoma ili ajue ukweli huu.kuhusu simba; kitabu kina mambo mengi na historia nyingi za kitafiti kuhusu simba, hayo niliokushirikisha ni baadhi tu ya yale mengi yaliyopo katika kitabu hiki cha LION HEARTED, kilichoandikwa na  mtafiti nguli wa simba Andrew Loveride.

Nakushukuru sana kuwa kusoma makala hii ndefu, ombi langu kwako ni moja tu, nimetumia nguvu nyingi na muda mwingi sana kuandika makala hii ili kukushirikisha mambo haya muhimu, hivyo basi unaposoma makala hii mshirikishe na mwenzio ili wote tupate maarifa haya. Karibu tena kwenye makala nyingine bora sana hapa hapa.

Kama utakuwa na maswali maoni na mapendekezo usisite kuwasiliana nami kwa mawasiliano hapo chini, karibu sana.

“The future of lions may depend on how they are viewed by Africans”.

Makala hii ya uchambuzi imeandikwa na

Hillary Mrosso

Mhifadhi wanyamapori

+255 683 862 481/ +255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com