Habari za siku nyingi ndugu msomaji wa makala za wanyamapori na maliasili, siku za hivi karibuni nilipokea barua nzuri sana kutoka kwa rafiki yangu Dr. Raymond Mgeni, aliandika mambo mazuri sana kuhusu utalii na vivutio vilivyopo hapa Tanzania, kubwa zaidi alichonifurahisha rafiki yangu huyu ni kuchukua hatua na kuanza kutembelea maeneo mbali mbali yenye vivutio hivyo. Katika barua yake kwangu ameandika mambo haya.
Habari ndugu yangu, Nakumbuka lakabu yako ya ushairi kama “Malenga wa Pori”. Zile tungo zako tunazikosa sana siku hizi. Naamini utakuwa tu umebanwa na hali ya kutafuta mkate wa maisha. Hongera sana kwa juhudi zako za wakati ule za kutumia ushairi kutetea maisha ya wanyama pori. Kwangu siwezi kusahau “tumbusi” maana ulionyesha kuumia kwako kupitia mtandao mmoja wa kijamii {facebook}.
Nakumbuka darasa lako ambalo ulipata kufundisha kupitia kundi la whatsapp juu ya mbuga za wanyama, mapori ya kitalii na fursa tele za uwekezaji kitalii eneo la wanyamapori na maeneo yenye kuvutia. Kwa kweli nilihamasika sana na sikutaka kuishia pale bila kufanyia kazi. Nikuambie nilitembelea baadhi ya maeneo ya kitalii jijini Arusha na Morogoro kwa mwaka jana na mwaka huu mwanzoni Januari.
Kwa njia ya kusafiri eneo moja na lingine kuna faida kubwa lakini si zaidi pale unapopata mazingira mazuri ya wanyama. Hali ya kuwaona wanyama na mazingira yao ina funzo pana kwetu binadamu. Kukaa na kujifunza maisha yao ni somo tosha la utulivu kwetu sisi binadamu. Hakika nyie mlioko karibu na mazingira haya mnafaidi sana. Hongera sana Kaka.
Hodi hodi! Hakika nami sitaki kupitwa na uzuri ambao mnao katika sekta hii adhimu na yenye heshima kubwa sana. Hodi mimi ni mgeni katika sekta hii na ninapenda kuwa mwenyeji. Najua kuwa mgeni ni taabu na gharama basi naomba uliye mwenyeji wangu unionyesha mengi nisiyoyajua mimi niliye mgeni kwa uhalisia na pili jina langu la mwisho nalo Mgeni (nacheka hapa huu mfano). Nikaribisheni huko nataka kuwekeza sekta hii ya utalii na wewe ni mwenyeji wangu.
Mimi mgeni napenda kujua mengi kupitia wewe, kupitia watu unaofahamiana nao, kupitia rejea za vitabu, kupitia rejea za blogu (ya kwako itanisaidia sana kuyajua maeneo ya vivutio). Nitashukuru sana mgeni huyu akipokelewa. Wanasema mgeni ajapo basi ndio heri ya mwenyeji. Basi mgeni leo anabisha hodi katika nyumba yako ya UTALII. Mwenyeji kazi kwako! (nina furaha sana).
Nikutakie mwitikio wako wa hodi yangu! Nipo mlangoni nagonga hapa hodi!, hodi!
Ni Mimi Mgeni Raymond, Malenga wa Ubena na mwandishi. Nangoja ukaribisho wako.
14.05.2019
Malenga wa Ubena.