Dunia imebarikiwa kuwa na wanyama na ndege wa aina nyingi, kuna warefu kama twiga, wanene kama kiboko, wakubwa kama tembo na nyangumi, wadogo kama sungura, wenye mbio kama duma, wajanja kama fisi, walio hodari na jasiri kama simba, wakatili kama mbwa mwitu, na walio wagumu kuonekana kama kakakuona.

Licha ya umuhimu wa wanyamapori katika kukuza uchumi na kuweka sawia mifumo ya ikolojia na mazingira, wanyama wana umuhimu mkubwa sana kwa binadamu. Kuna mahusiano ya karibu sana kati ya binadamu na wanyama, ndio maana watu wanapenda wanyama, wengine wanawafuga, wengine wanapanga safari na kulipa fedha nyingi kwenda kuwaona wakiwa porini au wakiwa katika bustani za kutunzia wanyama kama vile zoo. Na wengine wamefikia hatua ya kujiita majina ya wanyama, wengine wameamua kuvipa vitu majina ya wanyama na kuwapa wanyama majina ya watu.

Mfano, kuna watu wanajiita simba, wengine chui, wengine wanajiita tembo, wengine wanajiita mamba, wengine wanajiita mafisi, nk. Nakumbuka wakati tunasoma Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, kuna mwenzetu alikuwa anajiita Joka, mwingine alijiita Koboko. Hii inaonyesha uhusiano wa karibu uliopo kati ya wanyama na binadamu, lakini pia watu wanaona fahari kujiita majina ya wanyama. Pamoja na hayo, kuna wanao vipa vitu majina ya wanyama mfano klabu za mpira wa miguu kama Simba sport club, kuna clubu ya mpira huko Senegal inaitwa Simba wa Teranga, kuna nyingine inaitwa Super Eagle huko Nigeria (eagle ni ndege aina ya tai), nyingine inaitwa Tembo huko Ivory coast, nyingine inaitwa Vipers Sport Club ya Uganda (Viper ni aina ya nyoka wenye sumu).

Hata katika maandiko matakatifu, tunasoma Mungu akijifananisha na Simba, mfano kitabu cha Ufunuo wa Yohana 5: 5, inasema, “Na moja wapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile mhuri zake saba”. Sehemu nyingine tunaona kwenye maandiko Mungu akifananisha utendaji wake kazi kama wa ndege aina ya Tai, Kitabu cha Yeremia 48:40 na kitabu cha Ezekieli 1:10, vinaeleza Mungu anavyotumia wanyama na ndege kufikisha ujumbe wake kwa wanadamu. Hii inamaanisha wanyama na ndege sio tu wana umuhimu kimazingira, lakini pia wana historia takatifu inayounganisha Mungu na binadamu.

Historia ya binadamu kutumia wanyamapori imekuwepo kabla ya enzi za tawala za kale za Mesopotamia katika miaka ya 2334–2154 BCE, utawala wa Alexander Mkuu na utawala wa Roma, tawala za Nubia na Kushi kaskazini mwa Afrika, hadi kwenye tawala za Kisultani zilizoshamiri Afrika Mashariki kati ya miaka 1200-1509. Watu walitumia wanyamapori kufanya biashara, kuabudu, kufanyia kazi, kupigania vita, kufanyia mapambo na kuimarisha himaya zao za kifalme na kisultani. nk. Hakuna kwenye historia, utawala ambao haukutumia wanyama kwenye enzi za utawala wao. Hii inazidi kuonyesha jinsi tulivyo na muunganiko wa karibu na wanyamapori, wanyama wana vitu vingi vinavyotufurahisha, kuburudisha, kufundisha, na kutufanya tuendelee kuishi kwenye hii dunia. Hii ndio maana mara nyingi tunataka kuwa karibu na wanyama.

Hata hiyo, baadhi ya wanyama wamekuwa na mvuto wa kipekee sana kwa watu pale wanapookena. Miaka ya hivi karibuni tumekuwa tukiona na kupata taarifa za matukio mengi ya kuonekana kwa mnayama aina ya KAKAKUONA. Kakakuona kwa kingereza anaitwa “Pangolin”. Kakakuona ni mamalia pekee mwenye magamba, mnyama huyu amekuwa na mvuto na hisia za kipekee sana kwa watu, sio tu katika fani ya uhifadhi wa wanyamapori, bali hata katika jamii za watu wa kada mbali mbali.

Mfano, mnamo Januari 26, 2021, kakakuona alionekana katika kijiji Cha Wami Sokoine Wilayani Mvomero mkoani Morogoro. Kwenye tukio hilo, niliona jinsi watu walivyotekwa umakini wao na mnyama huyu wa ajabu, wengine walitaka kumshika, wengine walimsogelea karibu, wengine walipiga picha, na wengine waliomba kakakuona awasaidie kutatua shida walizo nazo. Pamoja na hayo walikuwepo wahifadhi wa maliasili pamoja na wazee wa jadi, wazee wa jadi waliweka vitu mbali mbali kumzunguka kakakuona, kama mahindi, maji, panga, mikuki, jembe nk. Unaweza kuangalia video hiyo hapa kuona tukio zima MAAJABU KAKAKUONA’ aonekana Morogoro |

Tukio jingine la hivi karibuini, mwaka 2023, liliripotiwa na kituo cha utangazaji cha WASAFI FM, katika kata ya Kihonda Manespaa ya mkoa wa Morogoro, kakakuona alionekana amehifadhiwa kanisani, kanisa la Matendo ya Mitume. Katika tukio hilo wakazi wa eneo hilo walikuwa wakiomba kakakuona awasaidie mambo mbali mbali kwenye maisha yao. Kuna waliomba wapate wachumba, wengine waliomba wapate watoto, wengine walisikiwa wakiomba amani, wakiomba vitu vishuke bei, na wengine waliombea Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) liache kukata kata umeme, wengine waliomba wapate fedha za kusaidia familia zao, wengine waliomba mvua inyeshe, wengine waliomba kuonyeshwa ishara yoyote ya upendo kutoka kwa kakakuona huyo. Unaweza kuangalia hiyo video hapa.KAKAKUONA AONEKANA KANISANI, WANANCHI WAMUOMBA ‘TANESCO WAACHE KUKATA UMEME

Katika karne hii ya sayansi na teknolojia, haya yanaweza kuonekana ni mambo ya ajabu na ya kushangaza, lakini haya ndio mambo yanayoendelea sehemu nyingi zenye wanyama hawa. Pia inaweza kuwa ni sehemu ndogo sana kati ya yale tunayofahamu kuhusu uhusiano uliopo kati ya wanyamapori na binadamu. Kama tulivyoona katika historia ya bindadamu, haya ni mambo yaliyokuwa yakifanyika kwa baadhi ya wanyama na baadhi ya tamaduni za watu. Hivyo, tunapofikiria namna nzuri ya kufanya uhifadhi endelevu wa wanyamapori tunatakiwa kuangalia kwa ukaribu tamaduni za watu na baadhi ya wanyama ambao wana wana maana sana kwenye mambo yao ya jadi au tamaduni zao.

Baadhi ya tamaduni zinaweza kuwa ni chanzo cha kuendelea kupungua kwa idadi ya wanyamapori sehemu nyingi duniani. Na huenda tamaduni hizo zikawa ni kichocheo cha wanyama hawa kuwa katika hatari ya kutoweka sehemu mbali mbali wanakupatikana wanyama hawa. Pamoja na sababu nyingine kama vile biashara za kakakuona na viungo vyake, matumizi kwa ajili ya chakula na dawa za kienyeji zimefanya kakakuona kuwa miongoni mwa wanyama wenye mahitaji makubwa sana duniani.

Kwa sasa kakakuona anashikilia nafasi ya kwanza duniani, kama mnyama anayeongoza katika biashara haramu za wanyamapori. Inakadiriwa kuwa zaidi ya kakakuona milioni 2 wanawindwa kila mwaka kuanzia mwaka 2000 hadi 2014. Kwenye tovuti ya Guinness World Records, inaonyesha kuwa kakakuona 300 wanawindwa kila siku kutoka maeneo mbali mbali duniani. Hizi ni takwimu za kusikitisha sana kuhusu uhifadhi endelevu wa mnyama huyu wa pekee. Hii imepelekea Shirika la Umoja wa Kimataifa linalohusika na Uhifadhi wa Mazingira Asilia, au kama linavyojulikana kwa kingereza, “International Union for Conservation of Nature” (IUCN), kuwaweka spishi wote wa kakakuona katika orodha ya spishi za wanyamapori walio hatarini kutoweka.Unaweza kusoma zaidi, kufahamu biashara ya kakakuona kwenye makala hii Usichokijua Kuhusu Biashara Haramu Ya KAKAKUONA, Jinsi Anavyoelekea Kutoweka Kabisa Katika Uso Wa Dunia.

Tani za magamba (scales) ya kakakuona yaliyokamatwa sehemu mbali mbali duniani, viroba vimejaa magamba ya kakakuona

Duniani kuna aina 8 za kakakuona, aina 4 zipo katika bara la Asia, na aina nyingine 4 zipo katika bara la Afrika. Hapa nimeacha majina yao ya kingereza na majina yao ya kisayansi, ili yaeleweke vizuri kama yalivyo. Spishi wa Kakakuona waliopo katika bara la Asia ni Chinese pangolin (Manis pentadactyla), Sunda pangolin (Manis javanica), Indian pangolin (Manis crassicaudata) na Philippine pangolin (Manis culionensis). Spishi zilizopo afrika ni black-bellied pangolin (Phataginus tetradactyla), white-bellied pangolin (Phataginus tricuspis), giant ground pangolin (Smutsia gigantea) na Temminck’s ground pangolin (Smutsia temminckii)

Katika aina hizo nne zinazopatikana katika bara la Afrika, Tanzania kuna aina 3 za kakakuona ambazo ni Temminck’s ground pangolin (Smutsia temminckii), white-bellied pangolins (Phataginus tricuspis), na giant pangolins (Smutsia gigantean). Katika spishi hizi za kakakuona, zinatofautiana ukubwa, tabia na mazingira wanapopatikana.

Ground pangolin au “kakakuona wa ardhini” ana majina mengine kama vile, Temminck’s pangolin, Cape pangolin au unaweza kumuita steppe pangolinTemminck’s. Huyu ndio kakakuona anayeonekana mara kwa mara, hata matukio mengi ya kuonekana, mara nyingi anakuwa ni huyu kakakuona wa ardhini. Ni miongoni mwa kakakuona wadogo, ana urefu wa sentimita kati ya 60-90, uzito wake ni kilogram kati ya 8-18. Mwili wake umefunikwa na magamba (scales), kasoro sehemu za chini kwenye tumbo hana magamba, idadi ya magamba kwenye mwili wake ni 382, mara nyingi hujikunja na kuwa kama kama mpira wa miguu endapo atahisi kuna hatari, mara nyingi wanatembea kwa miguu ya nyuma. Hakuna taarifa za uzalianaji lakini inakadiriwa jike anabeba mimba kwa siku 140-150, na huzaa mtoto mmoja, chakula chao ni mchwa na siafu. Wana uwezo mzuri wa kunusa harufu kuliko kusikia na kuona.

Kakakuona wa ardhini (Temminck’s ground Pangolin) akitembea, utaona akiinua miguu ya mbele akiwa anatembea. Picha kutoka www.sundestinations.co.za

White-bellied pangolin majina mengine ni three-cusped pangolin, tree pangolion au kwa Kiswahili anaweza kuitwa “kakakuona wa miti”, huyu ni kakakuona anayepanda miti. Hupatikana zaidi katika ukanda wa Ikweta, hutumia muda mwingi kuwa juu ya miti, ana sifa ya kuwa ni kakakuona mwenye mkia mrefu kuliko wenzake, mkia wake unaweza kufikia urefu kati ya sentimita 35 hadi 60. Mkia wake hutumika kama mguu wa tano pale anapopanda miti. Mwili wake umefunikwa na idadi ya magamba kati ya 790 na 1140, sehemu ya juu ya uso wake na sehemu za tumbo hazina magamba, uzito wa gamba moja ni gramu 0.66, ulimi wake unafika urefu wa sentimita 30, ana uwezo mkubwa wa kunusa harufu, anaweza kubeba mimba kwa siku 150, muda wa kuishi haujulikani, lakini inakadiriwa inaweza kuwa zaidi ya miaka 10 akiwa kwenye zoo au bustani za kuhifadhia wanyama.

Huyu ndio kakakuona anayepanda miti, tree pangolin au White-Bellied Pangolin, ukiangalia utaona ana mkia mrefu sana. Picha na Guy Colborne

Giant Pangolin, huyu ni kakakuona mkubwa kuliko spishi zote za kakakuona, hupatikana kwenye maeneo yenye misitu minene kama Africa Magharibi, Afrika ya Kati na maeneo ya Kaskazini Magharibi mwa Tanzania. Kakakuona huyu anakaribiana sana kufanana na Temminck’s, uzito wake unafikia kilogram 33, urefu wake ni mita 1.8, mwili wake umefunikwa na magamba 509-664, kucha za miguu ya mbele ni ngumu na hutumika katika kuchimba mashimo, vichuguu na kutafuta chakula, chakula kikuu ni mchwa na siafu, inakadiriwa anaweza kula zaidi ya wadudu million 7 kwa mwaka, ni ngumu sana kuonekana, shughuli zake nyingi hufanya usiku. Mengi hayajulikani kuhusu uzalianaji, lakini jike anakadiriwa kutumia siku 150 kubeba mimba, na mara nyingi huzaa mtoto mmoja, mtoto ana bebwa mgongoni. Kutokana na kuwa na uwezo mkubwa wa kunusu harufu, hutumia njia hiyo kutafuta chakula na kuwasiliana.

Huyu ndio Kakakuona mkubwa kuliko wote (Giant ground pangolin) kama anavyoonekana hapo akinywa maji, ukimwangalia kwa makini utagundua pua yake imechongoka zaidi kuliko wengine. Picha kutoka africanpangolin.org

Licha ya miili yao kufunikwa na magamba magumu kwa ajili ya kujilinda, pia kakakuona hutegemea sana mashimo kama makazi muhimu yao, mashimo haya huwalinda dhidi ya maadui, hali hatarishi za hewa kama vile mvua, jua kali, moto nk. Hata hivyo, mashimo ni sehemu muhimu ya kuzaliana na kulelea watoto.

Pamoja na upekee wa maumbile yao, kakakuona ni wanyama muhimu katika kuweka usawa katika mifumo ya ikolojia kwa kula wadudu kama mchwa na siafu, lakini pia kwa kurutubisha udogo kwa njia ya kuchimba mashimo. Hata hivyo, taarifa tulizo nazo kuhusu kakakuona ni chache, taarifa hizi hazitoshi kuweka mikakati imara ya uhifadhi endelevu wa kakakuona katika nchi zetu.

Mfano, kuna taarifa na machapisho mengi yakielezea kakakuona wan chi za Asia, changamoto ya biashara haramu, na majanga mengine yanayowakabili kakakuona, na ukosefu wa tafiti za kutosha kuhusu wanyama hawa. Hata hivyo, ili kuwe na njia bora za uhifadhi wa wanyama hawa lazima kila spishi ya kakakuona itambuliwe vizuri, na itengenezewe njia za uhifadhi ambazo zitaendana na mazingira yake na upekee wake.

Katika nchi yetu, ambako kuna spishi 3 za kakakuona, tunakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa taarifa za kina kuhusu kakakuona wote watatu. Jambo hili linatuwia vigumu kutekeleza mikakati imara ya uhifadhi wake, licha ya kusikia taarifa mbali mbali za kukamata watu wakisafirisha kakakuona na magamba yake, bado hatujui ni spishi ipi ya kakakuona imekamatwa, lakini pia hatujui ni kiasi gani cha biashara hii haramu inafanyika katika nchi yetu.

Pamoja na hayo, hatujui madhara ya kitamaduni yanayofanywa na watu pale mnayama huyu anapoonekana, lakini pia hatujui madhara ya kiafya pale watu wanampomshika au kugusana na kakakuona. Kubwa zaidi, hatujui hatma ya mnyama huyu pale anaporudishwa porini baada ya kuokolewa na watu, hatujui anaendelea kuishi au anakufa. Kiufupi, mengi bado hajulikani kuhusu kakakuona, hivyo ni wakati sahihi wa kuamka na kuanza harakati za uhifadhi wa mnayama huyu wa kipekee.

Taarifa za IUCN, Umoja wa Mataifa na machapisho mengine makubwa inaonyesha kakakuona ni mnyama anayeongoza kwenye wanyamapori wanafanyiwa biashara haramu dnuniani. Hata hivyo, mtandao wa biashara haramu za wanyamapori unaonyesha kiasi kikubwa cha kakakuona na magamba yake wanatoka katika nchi nyingi za Afrika, Tanzania ikiwemo. Hii ina maana kakakuona anamzidi tembo na faru kwenye biashara haramu za wanyamapori. Tunatakiwa kumuweka kakakuona kwenye vipaumbele vya uhifadhi na tafiti kama walivyo wanyamapori wengine.

Bahati nzuri, Taasisi ya Utafiti na Uhifadhi Tanzania, Tanzania Research and Conservation Organization (TRCO) imeanza kuonyesha njia kwenye jambo hili nyeti. Taasisi hii ya TRCO, inafanya tafiti za kina kujua mambo yote ya msingi kuhusu kakakuona waliopo Tanzania, idadi yao, biashara, changamoto zinawapata wanyama hawa, njia sahihi za kuwabeba, sehemu sahihi za kuwaachia endapo watakuwa wamekamatwa maeneo ya makazi ya watu nk.

TRCO inashirikiana na Mamlaka na Taasisi za Serikali, Wizara ya Maliasili na Utalii Tanzania, kuhakikisha tafiti za kina kuhusu kakakuona zinafanyika. Pamoja na mambo mengine ya utafiti, TRCO imejipaga kuandaa program za kuelimisha, kutoa mafunzo kwa wahifadhi na jamii kuhusu namna bora ya kuhifadhi kakakuona wa Tanzania. Kufahamu mengi kuhusu TRCO na kazi zake unaweza kutembelea tovuti yao hapa Tanzania Research and Conservation Organization

Nikimalizia makala hii, jamii inatakiwa kuamka kuhusu uhifadhi wa kakakuona, kwasababu kwa kiasi kikubwa kakakuona wanaonekana na wataendelea kuonekana kwenye makazi yao, au mashambani kwao, au barabarani. Unachotakiwa kufanya ni kutomdhuru au kumgasi kakakuona huyo. Endapo kakakuona ameonekana nyumbani kwako kwenye makazi ya watu, njia nzuri za kuhakikisha usalama wake na wako ni kutoa taarifa kwenye serikali ya kijiji, kwa watu wa maliasili kama vile Afisa Wanyamapori Wilaya, DGOs, TAWA, TANAPA, TFS, Watu wa hifadhi ya Ngorogoro au unaweza kutoa taarifa kituo cha polisi.

Kamwe, usimuhifadhi kakakuona nyumbani kwako, kwasababu ni hatari kwako na kwa kakakuona, maana anaweza kufa kwa njaa ukapata kesi ya ujangili. Kakakuona ni nyara ya serikali kama zilivyo nyara nyingine za meno ya tembo, pembe za faru, ngozi za simba nk. Kamwe usikubali kumuhifadhi ndani ya nyumba yako, labda kama una kibali cha maliasili cha kufanya hivyo. Njia nzuri ni kutoa taarifa mapema kwa uongozi wa kijiji au watu wa maliasili

Hivyo, endapo kakakuona ataonekana kwenye maeneo yenu, tusaidiane kutoa taarifa kwenye mamlaka husika ili kwa pamoja tushiriki katika uhifadhi wa mnyama huyu wa kipekee. Muhimu, kakakuona akionekana kwenye maeneo yenu, usimpige, usimfungie kwenye bodaboda, usimshikeshike, endapo utamshika, tumia nguo kama blanketi ambalo halitamuumiza, usimtupie kwenye gari bila kumuweka kwenye box maalumu ambalo lina hewa, lina kitambaa au nguo nzito chini ili utakapomsafirisha asiumie. Ukimuona kakakuona kwenye makazi yake asilia unaweza kumuacha bila kumgusa aendelee na maisha yake, toa taarifa pale atakapoonekana kwenye makazi ya watu.

Naamini umepata elimu kidogo kuhusu kakakuona, kama una maswali, maoni, mapendekezo, usisite kuwasiliana.

Imeandikwa na Hillary Mrosso, +255 683 862 481, hmconserve@gmail.com