Jua lilikuwa karibia kuzama wakati tukishuka milima ya kijiji cha Kisilwa ambayo inapakana na hifadhi ya taifa ya Ruaha. Tulikuwa tumechoka sana kutembea kilomita nyingi kwa miguu katika pori hilo la kijiji. Tulikuwa tunatekeleza mradi wa kamera vijijini, ambazo tulizitega kwa ajili ya kuangalia wanyampori waliopo kwenye mapori ya vijiji.
Mradi wa kamera vijijini unasimamiwa na mradi wa kanivora ambao upo katika eneo hili la Ruaha. Katika utafiti huo tulioufanya kwa muda mrefu katika eneo hilo, tulibaini kuwa maeneo ya mapori ya vijiji yana idadi kubwa na aina nyingi za wanyamapori.
Lengo la mradi wa kamera vijijini ilikuwa ni kubaini wanyamapori waliopo kwenye mapori ya vijiji, kutoa zawadi kwa vijiji vyenye mapori yenye wanyamapori. Ili watu waone faida ya wanyama hao kwenye mapori ya vijiji vyao, na kuendelea kuvumiliana na wanyama hao kutokana na faida wanayoipata.
Maeneo mengi ya vijiji yanayopakana na hifadhi za wanyamapori yana muingiliano mkubwa watu na wanyamapori. Wanyamapori wengi wanafika vijijini, na pia hata watu ni rahisi kuingia kwenye maeneo ya wanyamapori.
Hivyo, wanyamapori kuonekana vijijini na kwenye makazi ya watu ni jambo la kawaida kabisa katika eneo hili. Watu kuwaona tembo, nyani, simba, twiga, tandala, fisi, nguruwe pori, ngiri, swala kwenye maeneo yao ni jambo la kawaida, na wengi wameshazoea.
Hiyo basi, baada ya kushuku kutoka mlimani, tulifika tulipoacha gari letu. Ilikuwa imeshatimia saa 11 jioni, watu wengi wamesharudi majumbani mwao kupumzika, baada ya pilika pilika za nyingi za uandaaji wa mashamba kwa ajili ya msimu wa kilimo, wanafunzi nao wakirudi nyumbani. Wafugaji nao walikuwa wakirudisha mifugo yao nymbani baada ya kutoka malishoni, wengine muda huo walikuwa kwenye vilabu vidogo vya pombe wekipata moja moja.
Baada ya kuagana na wenyeji wetu wa kijiji cha Kisilwa, tuliwasha gari na kuanza kuzitafuta kilomita zaidi ya 13, yalipo makazi yetu. Muda ulikuwa umeenda, na tunatamani kuwahi ili na sisi tukampumzike baada ya kazi nzito ya siku hiyo.
Tukiwa tunakaribia kijiji cha Mahuninga tuliona watu wakikimbia kuelekea ilipo ofisi ya kijiji. Tukajiuliza kulikoni, mbona watu wanakimbilia ofisi ya kijiji, kuna jambo gani la dharura saa hizi?
Tuliona hata wale waliokuwa kwenye vilabu vya pombe, wafugaji na waendesha bodaboda, wanafunzi waliokuwa wemtoka shule wakikimbia kuwahi ofisi ya kijiji. Nikamwambia mwenzangu, lazima kutakuwa na jambo muhimu sana hapo kijijini.
Tukafika tukaona umati mkubwa wa watu wamsimama nje ya ofisi ya kijiji, wakishangaa, kupiga picha na kumzunguka mnyama wa ajabu ambaye hawakuzoea kumuona. Ndio, alikuwa ni KAKAKUONA. Lakini nilisikia wenyeje ambao wengi walikuwa wahehe na wabena wakisema kwa kilugha chao ni ng’akakuona!

Baadhi wa wanakijiji waliofika na kuanza kumshika kakakuona, wakiamini mnyama huyu ameleta bahati hapo kijijini
Nilisikia watu wakisema, huyu ni “mnyama wa bahati”, akionekana ujue kuna jambo zuri linakuja, wengine walisema ni “mtabiri”, tulisikia ni mnyama wa maajabu, “anaweza kutokea na kupotea kimazingara”, “mwaka huu tuna bahati sana”, “mnyama anayeleta mvua” “magamba yake ni dawa” nk.
Siku zote watu wa eneo hili walizoea kuwaona wanyama wengine wakija hapo kijijini, lakini wengi hawakuwahi kumuona kakauona. Hivyo alipoonekana hapo kijijini aliteta mshangao na mvuto kwa wengi. Wengi walikuwa na shauku ya kumuona, kiasi cha kuacha shughuli zao, mapumziko yao ili waje kumuona mnyama huyu wa kipekee aliyeonekana kijijini.
Kakakuona alikuwa amezungukwa na watu wengi, alikuwa amejikunja na kuwa kama mpira, niliona watu wamempa unga na matikiti maji ili ale. Lakini sikuona kama kakakuona aliweza kula, muda wote alikuwa amejikunja kama mpira.
Kwenye ule umati alikuwepo mwenyekiti wa kijiji, mtendaji, na wazee wa kimila. Wale wazee wa kimila walimzunguka kakauona kwa karibu wakawa wanafanya mambo yao ya jadi na kimila. Kiongozi moja wa wale wazee wa jadi akachukua maji, mtama, mahindi, na mkuki akaviweka kumzunguka kakauona.

Picha hii inaonyesha namna ilivyokuwa hapo kijijini baada ya kakakuona kuonekana. Hii picha nimeipata mtandaoni. Lakini inasaidia kuonyesha uhalisia wa kile kinachofanyika sehemu nyingi Tanzania, kakakuona anapoonekana.
Baada ya kuweka vitu hivyo kumzunguka kakakuona, walitulia na kusogea pembeni kidogo ili waone kakakuona atagusa kitu gani kati ya vile vitu walivyomuwekea. Kulingana na mila ni kwamba, endapo kakauona atagusa chochote kati ya vitu walivyoweka kumzunguka, kitu hicho kinaweza kutokea siku za baadaye.
Mfano, endapo kakakuona atagusa maji, ni ishara kuwa kutakuwa na mvua nyingi mwaka huo, endapo akigusa mahindi, ni ishara kuwa kutakuwa na mavuno au chakula kingi mwaka huo, endapo atakusa panga au mkuki, ni ishara kuwa kutakuwa na vita mwaka huo.
Hayo yalikuwa ni maelezo ya kiongozi wa jadi aliyekuwa anafanya hizo mila na jadi hapo kijijini. Yule mzee wa jadi alieleza kuwa enzi za utawala wa machifu, wazee wao walimtumia kakakuona kutambika, kuomba dua na kutabiri, lakini pia alisema kakakuona ni mnyama anayeheshimika sana tangu enzi za utawala wa machifu.
Wakati hayo yakiendelea, tulimshauri mtendaji na mwenyekiti watoe taarifa kwa wahifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na Afisa Wanyamapori Wilaya, waje kumchukua na kumrudisha hifadhini. Ambao walifika eneo hilo bila kuchelewa na kumchukua kakakuona.
Baadhi ya watu walitufuata pale tulipo na kuanza kutuuliza baadhi ya maswali kuhusu kakakuona. Licha ya muda kwenda sana, ilikuwa inakaribia saa moja na nusu usiku, ilibidi tubaki tuyajibu maswali hayo.
Kijana mmoja aliuliza, hivi kakauona anazaa au anataga? Nikamjibu, kakakuona ni wanyama jamii ya mamalia, wanazaa pia wananyonyesha, ananyonyeshaa? Nikamjibu ndio, ee, maajabu haya! Akashangaa mama mmoja wa kihehe aliyekuwa anatusikiliza!
Akaendelea kuuliza tena, anazaa watoto wangapi? Nikamjibu, mara nyingi anazaa mtoto mmoja tu kwa mwaka, akashangaa, ndio maana ni wa chache sana.
Mtendaji akauliza, chakula cha kakakuona ni nini? nikamjibu, kakakuona wanakula mchwa na siafu..aloo kumbe, sasa mbona walimpa matikiti na unga? Nikamjibu, watu wengi wanafanya hivyo kwasababu hawajui, ila chakula kikuu cha kakakuona ni siafu na mchwa.
Eee, Napata elimu hapa, kuna kijana mwingine mwendesha boda boda akauliza, kakakuona anabeba mimba kwa muda gani? Nikamjibu, anabeba mimba kwa siku 120 hadi 150. Akizaa mtoto wake anamlea, lakini pia humbeba mtoto wake mgongoni. Akashangaa, kwahiyo anabeba mtoto mgongoni kama binadamu? nikajibu, ndio.
Mwanafunzi aliyekuwa pale anatusikiliza akualiza, nimeona kakakuona emejikunja kama mpira, maana yake nini? Nikajibu, swali zuri sana, kakakuona ni wanyama wenye aibu sana, na pia huwa anajikunja hivyo ili kujilinda na maadui zake, pia magamba yake ndio humsaidia asipate madhara.
Mwanafunza akauliza tena, kwani adui yake ni akina nani? Nikamjibu, wanyama wanaokula nyama kama simba, chui, mbwa, fisi anaweza kuwa adui wa kakakuona. Nikaongeza, hata binadamu kwa sasa amekua adui mkubwa wa mnyama huyu.
Kivipi binadamu amekuwa adui ya kakakuona? Nikamjibu, taarifa nyingi za ujangili na biashara haramu zinamuhusisha sana kakakuona. Kila mwaka, mamilioni ya kakakuona na magamba yake hukamatwa yakiwa yanasafirishwa kwenda katika nchi za Asia na Ulaya, ambako kuna matumizi makubwa ya mnyama huyu kama vile chakula na dawa. Soma hapa kufahamu zaidi Usichokijua Kuhusu Biashara Haramu Ya KAKAKUONA, Jinsi Anavyoelekea Kutoweka Kabisa Katika Uso Wa Dunia.
Makubwa haya, niliwasikia wenyeji wakijibu, yani yule kakakuona analiwa kama chakula? Nikajibu, ndio, kuna baadhi ya makabila na watu wanakula huyu mnyama kama kitoweo.
Lakini pia baadhi ya nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania, watu wamekuwa wakiwatumia kakakuona kwenye mambo ya imani za kishirikina na pia kwenye mambo ya utabiri kama tulivyoona wazee wa jadi walivyofanya hapa kijijini muda mfupi uliopita.
Akauliza tena, Tanzania tuna kakakuona wangapi? Nikamjibu, swali zuri sana, kwa sasa, hakuna idadi kamili ya kakauona inayojulikana, lakini Shirika la utafiti na Uhifadhi Tanzania, wanafanya kazi kubwa sana kuendelea kutafiti wanyama hawa ili tuwe na taarifa za kutosha, ikiwemo kujua idadi yao.
Nikaongezea, Tanzania tuna aina tatu za kakakuona, kakakuona wa ardhini mfano huyu aliyeonekana hapa leo, kakakuona mkubwa wa ardhini na kakakuona anayepanda miti au kakakuona tumbo jeupe. Watu wote wakashangaa!
Mwanafunzi akauliza tena, makazi yao ni wapi? Nikajibu, kakakuona wanaweza kuishi maeneo yenye misitu, mapango, mashimo, savanna, mashambani, na maeneo karibu na maji.
Mwenyekiti wa kijiji alifurahi na kusema, kweli umetufungua macho sasa, sikuwahi kujua kama kuna kakakuona watatu, pia sikujua kama kakakuona wanakula mchwa na siafu, kweli elimu hii ni muhimu sana kwa uhifadhi wa wanyama hawa.
Muda ulikuwa umeenda sana, ilikuwa inakaribia saa mbili na nusu usiku, nikawaambia kuna mambo mengi ya kujifunza kuhusu kakakuona, mfano, sijaeleza kwa kina aina za kakakuona, changamoto, matumizi na mambo ya kufanya kakakuona anapponekana kijijini.
Hivyo, nikawaambia waturuhusu tuendelee na safari yetu, ili siku nyingine tumuombe mwenyekiti wa kijiji aitishe tena mkutano, ambao hautakuwa wa dharura kama leo, niwaeleze mambo yote muhimu kuhusu kakakuona uhifadhi wake.
Asante kwa kusoma makala hii, imeandikwa na Hillary Mrosso
Tunaandika makala hizi ili watu waongezewe uelewa kuhusu kulinda na kutumia Maliasili muhimu bila kuathiri uwepo wao wa sasa na baadaye; kazi hii tunafanya kwa kujitolea na hakuna malipo yoyote, endapo umefurahia kazi zetu kutuunga mkono kwa kiasi chochote ili tupate nguvu, na ari ya kuandika makala nyingine nzuri, usisite kuwasiliana nasi kwa maelezo zaidi
Hillary Mrosso
+255683862481