Miaka ya hivi karibuni milipuko ya magonjwa yanayotokana na wanyamapori imekua ikiongezeka kwa kasi, Magonjwa haya yamekua yakiathiri wanyamapori pamoja na binadamu. Wanyamapori wengi wapo hatarini kutoweka kwa sababu mbalimbali kama vile uharibifu wa mazingira, uwindaji haramu pamoja na magonjwa. Hivyo basi ni muhimu kuweka juhudi za kuhakikisha magonjwa kwa wanyamapori wetu si tishio tena, ili kukabiliana na changamoto hii ni lazima tuelewe kuhusu taaluma ya madakitari wa wanyamapori na namna wanavyofanya kazi zao kuhakikisha wanalinda na kuokoa uhai wa wanyamapori wetu hapa nchini.
Dakitari wa wanyama pori ni nani?
Dakitari wa wanyamapori ni taaluma muhimu sana ambayo imegawanyika katika makundi matatu. Ni vyema nikufahamishe kuwa hakuna utofauti wa kitaaluma kati ya dakitari wa mifugo na madakitari wa wanyamapori kwakua wote hupata mafunzo yanayofanana. Kundi la kwanza ni wenye ujuzi wa juu (shahada) ambao hawa husoma masomo yao kwa miaka mitano (Veterinary Doctors), kundi la pili ni la wale wenye ujuzi wa kati (diploma) ambao hawa husoma masomo yao kwa miaka mitatu kwa kiingereza ngazi hii ya elimu hujulikana kama (paraprofesionals), na kundi la tatu ni wenye ujuzi wa chini na hawa husoma taaluma hii kwa miaka miwili (certificate) na ngazi hii ya elimu kwa kimombo hujulikana kama (paraprofessional assistants).
Bado haiishii hapo dakitari wa wanyamapori mwenye ngazi ya juu shahada anaweza kujiendeleza kitaaluma na kusoma masomo ya ubobezi (masters) katika mambo mbali mbali yanayomuhusu mnyamapori na hii husaidia sana kuwawezesha wataaluma kuelewa jambo moja kwa undani sana. Ngazi hii ya elimu hutolewa katika mda tofauti tofauti kulingana na aina ya kozi muhusika aliyochagua, zipo kozi za miaka miwili, mitatu hadi minne. Wapo wataaluma wengine ambao huenda mbali zaidi na kusoma shahada ya uzamivu katika maswala yanayohusu utabibu wa wanyamapori(Phd)
Je ni namna gani ya kusoma taaluma hii?
Mtu yoyote mwenye ufaulu mzuri anaweza akasoma taaluma ya utabibu wa mifugo au wanyamapori hapa nchini Tanzania au nje ya nchi na kwa bahati mbaya si kila nchi hutoa mafunzo ya taaluma hii, Tanzania ni nchi ambayo imebarikiwa kuwa na wanyama wengi sana wafugwao pamoja na wanyamapori. Uwepo wa wanyama wengi ukaichagiza mamlaka ya nchi kuanzisha taasisi za elimu katika ngazi tofauti tofauti ambazo zimekua msaada mkubwa sana kuhakikisha rasilimali hizi za wanyama pori zinalindwa kwa ustadi wa aina yake.
Taasisi hizi za elimu hapa nchini Tanzania ni pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine pamoja na vyuo vya kati vitano vilivyopo maeneo mbalimbali ya nchi, vyuo hivi vya kati hujulikana kama LITA (Livestock Training Agency) vyuo hivi vina kampasi tofauti tofauti kama vile LITA Morogoro, Tengeru, Madaba, Buhuri na Mpwapwa. Vigezo vya kusoma taaluma hii vimetofautiana kutokana na ngazi ya elimu muhusika anayotaka kusoma. Kwa ngazi ya shahada muhusika ni lazima asome hadi kidato cha sita katika mchepuo wa sayansi na kusoma michepuo ya (PCB au CBG) au muhusika anaweza kujiunga na shahada kama amehitimu ngazi ya Diploma ya Afya ya Mifugo na Uzalishaji. Kwa wale wanapotaka kujiunga na ngazi ya certificate ni lazina wawe wamesoma hadi kidato cha nne.
Je dakitari wa wanyama pori hufanya kazi katika maeneo gani?
Nchini Tanzania Dakitari wa wanyamapori hufanya kazi zake katika maeneo ya uhifadi kama vile ndani ya Hifadhi za Taifa, Mapori Tengefu na maeneo yote yenye hadhi ya uhifadhi, pia baadhi ya mashirika binafsi ya uhifadhi huwa na madakitari wa wanyamapori. Taasisi hizi huwa na vitengo vinavyohusika na matibabu au utafiti unaohusiana na tiba ya wanyamapori. Endapo mnyamapori atapata matatizo nje ya hifadhi ya wanyamapori, dakitari wa wanyamapori anauwezo wa kwenda na kutoa huduma inayotakiwa kwa lengo la kuokoa uhai wa mnyma bila kujali eneo mnyama alilopo.
Ni vyema nikufahamishe kuwa ili dakitari afanye kazi zake ni lazima awe ameajiriwa na taasisi za kiserekali au mashirika yanayotambuliwa na mamlaka ya nchi. Ili kutoa huduma zinazohusiana na wanyamapori ni lazima dakitari asajiliwe na baraza la madakitari Veterinary Council of Tanzania (VCT)
Je! kuna faida zipi za ushirikiano kati ya dakitari wa wanyamapori na wataalamu wengine katika shughuli za kiuhifadhi?
Ushirikiano kati ya daktari wa wanyamapori na wataalamu wengine kama vile wataalamu wa ikolojia, wanyamapori, waongoza watalii, wanataaluma katika vyuo vya wanyamapori pamoja na watafiti ni muhimu sana katika juhudi za uhifadhi wa wanyamapori. Timu hizi hufanya kazi pamoja ili kufikia malengo ya kudumisha afya na ustawi wa wanyamapori, kuhifadhi mazingira yao asilia, na kuhakikisha kuwa mifumo ya ikolojia inabaki yenye usawa. Moja ya majukumu muhimu ya daktari wa wanyamapori ni kufanya uchunguzi wa afya na matibabu ya wanyamapori. Hata hivyo, ili kufanya kazi hii kwa ufanisi, wanahitaji ufahamu wa kina wa mazingira ambayo wanyama hao wanaishi.
Waikolojia; Hapa ndipo ushirikiano na wataalamu wa ikolojia unapokuwa muhimu. Wataalamu wa ikolojia wana ujuzi wa kina juu ya mifumo ya ikolojia, tabia za wanyamapori, na masuala ya uhifadhi. Kwa kushirikiana, daktari wa wanyamapori na mtaalamu wa ikolojia wanaweza kuelewa vizuri zaidi jinsi mabadiliko ya mazingira yanavyoathiri afya ya wanyamapori na jinsi ya kuchukua hatua kuzuia magonjwa au kurejesha afya ya wanyama waliokumbwa na matatizo.
Wataalamu wa wanyamapori; hawa pia ni sehemu muhimu ya timu hizi za ushirikiano. Wanafanya kazi katika maeneo yanayohusiana na uhifadhi wa wanyamapori na wanaweza kutoa taarifa za kina kwa dakitari wa wanyamapori juu ya idadi ya wanyama, mwenendo wa mabadiliko ya idadi ya wanyama, na hatari za kutoweka kwa spishi fulani. Habari hii inaweza kuwa muhimu kwa daktari wa wanyamapori katika kupanga na kutekeleza mikakati ya afya za wanyamapori.
Watafiti: Wao hufanya utafiti wa kisayansi ili kujifunza zaidi juu ya magonjwa yanayowaathiri wanyamapori, njia bora za matibabu, na mbinu za kuzuia magonjwa. Daktari wa wanyamapori anaweza kutumia matokeo ya utafiti huu ili kuboresha huduma za afya kwa wanyamapori. Mfano kwa Tanzania TAWIRI wanahusika na kufanya tafiti nyingi zinazohusiana na magonjwa ya wanayamapori na hutoa taarifa za tafiti zao kwa madakitari wa wanyamapori ili kuongeza ufanisi katika shughuli zao mbalimbali wanazofanya.
Watalamu wa utalii; Ni muhimu sana dakitari wa wanyamapori kushirikiana na wataalamu wa utalii kwakuwa hii huweza kulinda afya za watalii pale ambapo mlipuko wa magonjwa unapotokea katika hifadhi zetu. Ni vyema kutambua kuwa baadhi ya magonjwa kama kimeta yanaweza kuleta athari kubwa pale ambapo kutakua hakuna utambuzi na udhibiti wa magonjwa haya katika hifadhi zetu.
Wataaluma: hapa ninazungumzia taasisi zinazojihusisha na shughuli za ufundishaji wa maswala ya wanyamapori kama vile vyuo na taasisi binafsi, ni vyema na nimuhimu wataaluma kushirikiana na dakitari wa wanyamapori pale ambapo wanatoa mafunzo kwa wanafunzi hii husaidia sana kujenga wanafunzi wenye uelewa na mazingira halisi katika shughuli za uhifadhi.
Ushirikiano huu unawezesha kubadilishana maarifa, ujuzi, na rasilimali. Timu hizi zinaweza kufanya kazi pamoja katika shughuli za uchunguzi, matibabu, na uingiliaji wa upasuaji. Wanaweza pia kubuni na kutekeleza programu za chanjo, mipango ya udhibiti wa magonjwa, na mikakati ya uhifadhi wa mazingira. Kwa ujumla, ushirikiano kati ya daktari wa wanyamapori na wataalamu wengine ni muhimu katika kufanikisha uhifadhi wa wanyamapori. Kwa kushirikiana, wanaweza kulinda afya ya wanyamapori, kudumisha mazingira yao asilia, na kuhakikisha kuwa vizazi vijavyo vinaweza kufurahia utajiri wa wanyamapori wetu.
Ni majukumu yapi ya dakitari wa wanyama pori?
Uchunguzi na Tiba: Daktari wa Wanyamapori anahusika na kufanya uchunguzi wa afya na tiba kwa wanyamapori. Anashughulika na kuchunguza magonjwa, kutoa matibabu, na kufanya upasuaji kwa wanyamapori waliojeruhiwa au wagonjwa. Pia daktari wa Wanyamapori anasimamia mipango ya chanjo kwa wanyamapori ili kudhibiti magonjwa yanayoweza kuwaathiri. Wanapanga na kutekeleza programu za kinga kwa kuwapa chanjo wanyamapori na kufuatilia hali ya afya ya wanyama hao.
Kuhamisha na Kuweka Wanyamapori: Wakati mwingine, wanyamapori wanahitaji kuhamishwa kutoka eneo moja hadi lingine kwa sababu za uhifadhi au usalama. Daktari wa Wanyamapori anahusika katika mchakato huo kwa kuhakikisha usalama wao wakati wa usafirishaji na kuwaweka tena kwenye mazingira mapya.
Ufuatiliaji wa Afya: Daktari wa Wanyamapori anafanya ufuatiliaji wa mara kwa mara wa afya ya wanyama. Anachukua sampuli za damu, kinyesi, na tishu za wanyamapori ili kufanya uchunguzi wa maabara na kufuatilia mwenendo wa afya na magonjwa katika jamii ya wanyamapori.
Kuwafunga wanyama antenna (tracking devices): Ili kufuatilia mienendo yao jukumu hili muhimu katika uhifadhi, hufanywa na dakitari wa wanyamapori, wanyama ambao wapo katika hatari ya kutoweka kama vile kakakuona, mbwa mwitu, faru nk. Hufungwa vifaa hivi kwaajili ya kufuatilia usalama wao. Pia vifaa hivi vinaweza kufungwa kwajili ya shughuli za kitafiti mfano wanyma kama simba, tembo, twiga hufungwa vifaa hivi ili kubaini mienendo yao ya kila siku pia vifaa hivi husaidia kuwajulisha wahifadhi endapo mnyama ataingia katika maeneo ya makazi ya watu, na hii husaidia kupunguza migogoro kati ya wanyamapori na binadamu.
Usimamizi wa Magonjwa: Daktari wa Wanyamapori anashiriki katika usimamizi wa magonjwa yanayoweza kuathiri wanyama. Anafanya uchunguzi wa magonjwa, kufuatilia milipuko, na kuchukua hatua za kuzuia na kudhibiti magonjwa ili kuzuia kuenea kwa spishi zingine za wanyamapori.
Elimu na Mafunzo: Daktari wa Wanyama Pori anaweza kutoa elimu na mafunzo kwa wataalamu wa uhifadhi, wafanyakazi wa hifadhi za wanyama, na jamii inayozunguka maeneo ya wanyamapori. Wanaweza kutoa mafunzo juu ya afya ya wanyamapori, mbinu za kukabiliana na dharura za kiafya, na jinsi ya kuzuia magonjwa kati ya binadamu na wanyama pori.
Ushirikiano na Wadau Wengine: Daktari wa Wanyamapori anashirikiana na wataalamu wengine wa uhifadhi, wanasayansi, watafiti, na wadau wengine katika juhudi za uhifadhi na huduma za afya kwa wanyamapori. Wanaweza kushiriki katika mikutano, kushauri juu ya sera za uhifadhi, na kushirikiana katika utafiti na miradi ya uhifadhi.
Yafahamu baadhi ya magonjwa matano tishio kwa yanyamapori.
Dakitari wa wanyamapori huweza kutoa tiba kwa wanyamapori, chanjo au hata huduma ya kwanza pale wanyama wanapoumia. Kwa miaka mingi nchini Tanzania kumekua na dhana inayosema (LET NATURE TAKE ITS COURSE). Dhana hii au fikra hii imekua ikipelekea wanyamapori kukosa huduma stahiki wanazostahili. Ninakiri bila shaka kua kwa Tanzania nadharia hii kwa sasa imepoteza nguvu kwakuwa wanyamapori wanapata huduma stahiki za kitabibu pale ambapo wanakutana na changamoto mbalimbali.
Kimeta (Anthrax); Kimeta ni ugonjwa hatari wa kuambukiza unaosababishwa na bakteria wanaojulikana kama Bacillus anthracis. Ugonjwa huu hutokea kwa asili katika udongo na mara nyingi huathiri wanyama wa kufugwa na wanyamapori ulimwenguni kote. Watu wanaweza kuugua kimeta iwapo watakutana na wanyama walioambukizwa au bidhaa za wanyama zilizochafuliwa. Kimeta inaweza kusababisha ugonjwa mbaya sana kwa binadamu na wanyama, kimeta huweza kuathiri wanyamapori wengi kama vile pundamilia swala (impala) na kudu.
Brusela (Brucelossis); Brucellosis ni ugonjwa wa bakteria unaosababishwa na aina mbalimbali za bakteria wa Brucella, ambao kwa kawaida huambukiza ng’ombe, nguruwe, mbuzi, kondoo na mbwa. Kwa upande wa wanyamapori mara nyingi nyati huathiriwa sana pia Binadamu kwa kawaida huambukizwa ugonjwa huu kupitia mawasiliano moja kwa moja na wanyama walioambukizwa, kwa kula au kunywa bidhaa za wanyama zilizochafuliwa au kwa kupumua vijidudu vya ugonjwa huo vinavyosambaa hewani. Kesi nyingi husababishwa na kula maziwa Brucellosis ni mojawapo ya magonjwa ya kuambukiza yanayosambazwa na wanyama kwa binadamu, na katika maeneo yenye mlipuko, brucellosis kwa binadamu ina madhara makubwa kwa afya ya umma.
Malignant catarrhal fever. (MCF); Malignant Catarrhal Fever (MCF) ni ugonjwa unaosababishwa na maambukizi ya virusi vya Macavirus, ambayo ni sehemu ya familia ya Gammaherpesvirinae. Vimelea vya ugonjwa huu hubebwa na wanyamapori amabao hujulikana kama nyumbu. Ugonjwa huu husambaa kwa wanyama wafugwao kutoka kwa nyumbu hasa wakati wa mazalia ya nyumbu na kwenda kwa, ng’ombe, mbuzi, kondoo, na wanyama wengine wa kufugwa pale ambapo watakula malisho katika maeneo nyumbu walipozalia. MCF ni ugonjwa hatari na mara nyingi husababisha kifo kwa wanyama walioambukizwa. Hakuna tiba ya moja kwa moja ya MCF, na kinga ni muhimu katika kudhibiti ugonjwa huo. Chanjo zinapatikana kwa baadhi ya virusi vya MCF, lakini chanjo kwa wanyama wote haijapatikana kwa ufanisi. Ni muhimu kuchukua hatua za kuzuia, kama vile kudhibiti mawasiliano kati ya wanyama walioathirika na wanyama wengine, kuepuka malisho na maji yaliyochafuliwa, na kutekeleza hatua za usafi na usimamizi mzuri wa ufugaji ili kupunguza hatari ya kuenea kwa MCF kwa wanyama wa kufugwa.
Canine distemper; Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa distemper ni sehemu ya jenasi ya Morbillivirus, ambayo inaathiri spishi mbalimbali za wanyama. Inaweza kuambukizwa kupitia mawasiliano moja kwa moja na wanyama walioambukizwa, mafua, au vitu vilivyochafuliwa. Wanyama wanaoishi karibu, kama wale wanaoishi katika mazingira sawa au kuingiliana na wengine, wako hatarini kupata ugonjwa huo. Kwa wanyamapori simba na mbwa mwitu wanapata maambukizi ya distemper, wanaweza kuonyesha dalili mbalimbali, ikiwa ni pamoja na dalili za upumuaji (kukohoa, kupiga chafya, utoaji wa kamasi puani), dalili za mfumo wa chakula (kutapika, kuhara), dalili za neva (kutetemeka, kifafa, kupooza), na hatimaye kushuka kwa kinga ya mwili. Ugonjwa huo unaweza kuwa mbaya, na hata kuwa na madhara kwa viumbe vichanga au wale walio na kinga dhaifu. Magonjwa ya distemperi ya mbwa yameonekana kusababisha mlipuko kwa watoto wa simba na mbwa mwitu wa porini, na kusababisha viwango vikubwa vya vifo. Ugonjwa huu unaweza kuwa na athari mbaya kwa uhifadhi wa spishi hizi, kwani unaweza kusababisha kupungua kwa idadi ya watu na kuathiri afya ya mfumo mzima wa mazingira.
Rift valley fever; Ugonjwa wa Rift Valley fever (RVF) au Homa ya Bonde la Ufa ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vya Rift Valley fever virus (RVFV). Ugonjwa huu unaathiri wanyamapori, pamoja na wanyama wengine wa kufugwa. Pia, unaweza kuathiri binadamu. Ugonjwa wa Rift Valley fever unaweza kuwa hatari kwa wanyamapori, kwani unaweza kusababisha vifo vya kundi kubwa la wanyama. Pia, kuna hatari ya kusambaa kwa binadamu kupitia mawasiliano na wanyama walioambukizwa au kupitia kuumwa na mbu walio na virusi. Unaweza kusoma zaidi hapa kujua athari za magonjwa kwa wanyamapori Magonjwa Manne Hatari Zaidi kwa Watumiaji wa Nyamapori
Changamoto wanazokumbana nazo madakitari wa wanyamapori.
Angalizo!!! Changamoto ambazo nitaziainisha ni mtazamo wangu binafsi kwakuwa hakuna tafiti rasmi iliyofanywa kuthibitisha ukubwa wa changamoto hizi. Uzoefu nilio nao katika taaluma ya uhifadhi wa wanyamapori pamoja na utabibu wa wanyama umenisukuma kuandika na kutoa maoni yangu kuhusu changamoto zinazowakumba madakitari wa wanyama pori.
Idadi ndogo ya madakitari wa wanyama pori.
Kutokana na ukubwa wa hifadhi zetu nchini pamoja na idadi ya hifadhi zilizopo nchini Tanzania pia uwepo wa wanyama wengi sana wa aina tofauti tofauti idadi ya madakitari wa wanyamapori ni ndogo, hivyo ni muhimu kwa mamlaka zinazohusika kuhakikisha wataaluma wanaongezwa kulingana na ukubwa wa hifadhi husika mfano hifadhi ya Serengeti yenye ukubwa wa kilomita za mraba 14,763 ina jumla ya madakitari wawili au hifadhi ya mkomazi yenye ukubwa wa kilomita za mraba 3,245 ina jumla ya madakitari wawili pia.
Jografia pamoja na uoto wa baadhi ya hifadhi zetu.
Hifadhi kama ya Mlima Kilimanjaro ni hifadhi ambayo eneo lake kubwa lipo milimani na hivyo kufanya ugumu kufikika kwa urahisi pia uoto wa mapori au misitu inafanya vigumu kwa maeneo hayo kufikika kwa urahisi.
Uhaba wa vitendea kazi vya kisasa.
Vitendea kazi kama vile Helikopta za kufanyia doria kuchunguza na kufuatilia hali za wanyama pamoja na kuwachoma sindano za usingizi pindi wanapotaka kufanyiwa matibabu. Mfano wanyama kama vile twiga, faru au tembo huhitaji sindano ya usingizi (darting) kabla ya kuanza kwa matibabu yao pindi wanapopata changamoto za kiafya.
Uchache wa hosipitali za wanyama pamoja na maabara za kisasa kwaajili ya kufanyia vipimo.
Nchini Tanzania kuna hosipitali moja ya rufaa ya wanyama iliyopo Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine. Hosipitali hii imekua msaada sana japo haijitoshelezi kutokana na ukubwa wa mahitaji yaliyopo. Kwa mtazamo wangu ni vyema serekali ya Tanzania ione umuhimu wa kuongeza hosipitali zinazohusika na kutoa huduma kwa wanyama. Pia ni muhimu kuongeza idadi za maabara za kufanyia uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ya wanyama.
Asante sana kwa kusoma makala hii, imeandikwa na Leon Hermenegild na kuhaririwa na Hillary Mrosso. Ukiwa na maswali, maoni, mapendekezo na ushauri kuhusu Makala hii usisite kuwasiliana na mwandishi kwa mawasiliano hapo chini;
Leon Hermenegild
+255 742 398 956
leonehermenegild@gmail.com