Nilizaliwa huko kaskazini mwa Tanzania, baada ya kukua na kuanza kutembea niliona nimezungukwa na vitu vingi, mandhari nzuri za mazingira yaliyohifadhiwa na kutunzwa kwa ubora sana, katika yote hayo nilivutiwa zaidi na mlima mkubwa sana, mlima huu wakati mwingine hufunikwa na mawingu, na wakati mwingine barafu. Mlima huu ambao ni mrefu sana nilijua umefika mbinguni, niliwahi kuwauliza wazazi wangu kama kuna mtu anaweza kupanda na kufika hadi kilele cha mlima huu; wakati tunatembea barabarani tulikuwa tunapishana na magari yaliyobeba wazungu, ndio mara yangu kuwaona wazungu, nakumbuka baba aliniambia wale ni wazungu wametoka Ulaya wanakuja kupanda ule mlima. Baba aliniambia ule mlima unaitwa Kilimanjaro ndio mlima mkubwa kuliko yote barani Afrika, nilipenda sana hadidhi za mlima Kilimanjaro na jinsi watu walivyokuwa wanakuja kutoka sehemu mbali mbali kupanda mlima Kilimanjaro.

Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuzaliwa Tanzania, nchi iliyojaa uzuri na upekee wa kila aina, nchi hii imejazwa na uzuri wa asili, nchi hii imezungukwa na vivutio vya kupendeza. Nchi hii inavutia sana kuanzia Kusini hadi Kaskazini, Mashariki hadi Magharibi ni maajabu yake nchi hii. Nchi hii ina mipaka ya ajabu na ya kustaajabisha pande zake zote; Tanzania imezungukwa na maji, kaskazini lipo ziwa Viktoria, kusini lipo ziwa Nyasa, mashariki ipo bahari ya Hindi na mgharibi lipo ziwa Tanganyika.

Nchi hii ni muungano wa nchi mbili huru, yaani Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Zanzibar. Mashujaa wetu waliunganisha nchi zote mbili kwa kuchanganya udogo wa nchi zote na kuunda jina tamu sana la Tanzania. Walituanchia nchi nzuri sana, yenye watu walioongozwa na kulelewa kwenye misngi ya uzalendo, upendo na umoja.

Nchi hii ya ajabu iliyoundwa na watu wenye tamaduni za aina nyingi kutokana na tofauti za makabila yaliopo, inazidi kuifanya nchi ya kuvutia na kupendeza sana. Katika juhudi za mashujaa wetu kutuweka pamoja na kuondoa ubaguzi wa kila aina miongoni mwetu, waliyuunganisha kwa lugha moja ya Kiswahili.

Niambieni jamani, kabla sijaendelea na ujumbe wangu ni nchi gani duniani yenye mchanganyiko wa watu na makabila zaidi ya 120 ambao wanaongea lugha moja adhimu na tamu kama Kiswahili. Nchi hii imejaa amani, imejaa watu wakarimu na wenye umoja; nashukuru kuzaliwa Tanzania.

Nchi hii yenye utajiri wa kutisha kuanzia  utajiri wa nchi kavu na utajiri wa majini, nchi ambayo ardhi yake imebeba madini na vito vya thamani kubwa sana, udongo wake umebeba virutubisho vingi vya kufaa kwa kilimo chochote. Nchi  hii ambayo ina uoto wa asili, mabonde mengi ya asili, milima, mito, maziwa na mbuga za wanyama.

Nikiendelea kutaja kila kitu kizuri kilichopo Tanzania naweza nisimalize na hata kama nitamaliza kutaja kila kitu kilichopo Tanzania makala hii itakuwa ndefu sana, na nisingeweza kuandika kwa siku moja. Hata hivyo naamini kabisa sifa na vivutio vyote nilivyotaja katika makala hii sio vyote, na ni vile tu ambavyo nimebahatika kuviona, kuvisoma na kuvisikia. Naamini kabisa kuna vingi zaidi ambavyo sivijui  na sijaviandika katika makala hii kuhusu Tanzania.

Nataka ijulikane, kama inavyojulikana na kufahamika sehemu nyingi duniani kuwa Tanzania ni nchi iliyojaa rasilimali za kila aina. Wezee wetu na mashujaa wetu au watangulize wetu walitambua hilo, na wakaweka mikakati endelevu ya kuzifanya rasilimali za nchi yetu ziwe na manufaa endelevu kwa vizazi vingi vijavyo. Hivyo walitenga maeneo mbali mbali na kuyatungia sheria na taratibu za usimamizi na uendeshaji wake. Maeneo hayo kama vile maeneo yote ya wanyamapori; misitu ya aina zote, maeneo ya kihistoria, mito, mabonde na milima. Kila kitu kiliwekewa utaratibu wa matumizi, usimamizi na utunzaji wake.

Aidha, uwepo wa rasilimali hizi katika nchi yetu umechangia sana kusukuma gurudumu la maendeleo kwenye sekta zote muhimu kama vile sekta ya miundominu, sekta ya elimu, afya nk.

Tanzania inajulikana duniani kote kwa sababu ya upekee wa rasilimali zilizomo. Tanzania ni miongoni mwa nchi chache sana hapa duniani ambazo zimetenga asilimia kubwa sana ya eneo lake la nchi kwa ajili ya uhifadhi wa rasilimali zake muhimu kama vile misitu na maeneo ya wanyamapori.

Pamoja na hayo yote, ujumbe wangu kwa taifa ni huu, maendeleo tunayoyatafuta, maisha tunayoyatafuta usiku na mchana yasiwe sababu ya kuondoa uzuri na kuziweka rasilimali tulizo nazo rehani.

Nasema haya kwasababu naona kasi iliyopo katika nchi yetu, miradi mikubwa, shughuli za maendeleo kama kilimo, biashara ujenzi, zikishika kasi na kuanza kusogelea au kugusa maeneo muhimu ya hifadhi za wanyamapori na misitu.

Hivyo basi ujumbe wangu kwa jamii yote ya Tanzania ni huu, tuzilinde rasilimali zetu kwa manufaa ya sasa na kwa vizazi vingi vijavyo. Watoa maamuzi, washauri na watalaamu wa mambo haya wafanye kazi zao kwa weledi ili kutoruhusu mihemuko na hisia za kuwa na maendeleo zikaharibu uzuri wa rasilimali zetu adhimu. Kila kitu kifanyike kwa weledi na kwa kufuata taratibu zenye afya kwa pande zote.

Hillary Mrosso

+255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania

 

Shares:
  • Lusubilo Kayange
    Lusubilo Kayange
    July 9, 2019 at 2:12 pm

    Safi sana mhifadhi, makala nzuri sana iliyobeba ujumbe mzuri.

    Reply
    • wildlifetanzania
      wildlifetanzania
      July 10, 2019 at 4:15 pm

      Asante sana Mhifadhi Lusubilo, karibu sana

      Reply
  • Leena Lulandala
    Leena Lulandala
    July 10, 2019 at 8:12 am

    Niceeee, I like it

    Reply
    • wildlifetanzania
      wildlifetanzania
      July 10, 2019 at 4:14 pm

      Asante sana, Karibu Mhifadhi Leena

      Reply
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *