Je, unafahamu kuwa Tanzania ina aina 3 za kakakuona?
Katika spishi au aina 4 za kakakuona wanaopatikana Afrika, Tanzania ina aina 3 za kakauona, ambao ni Kakakuona wa ardhini (Ground Pangolin), kakakuona tumbo jeupe (white-belied pangolin) na kakakuona mkubwa (Giant Pangolin).

Kakakuona wa ardhini. Picha kutoka https://ar.inspiredpencil.com/pictures-2023/pangolin-walking
Swali, Umeshawahi kuona aina ipi ya kakakuona hawa?
Licha ya kuwa ni wanyama wasioonekana mara kwa mara, kakakuona wanapoonekana wanakuwa na mvuto na hisia kubwa kwenye jamii.
Wengi huamini kakakuona ni mnyama anayekuja sehemu fulani kwa ajili ya kuleta ishara ya jambo fulani kwenye jamii.

Kakakuona tumbo jeupe au kakakuona anayepanda miti, picha na Guy Colborne
Hivyo watu humuona kama mnyama wa kipekee sana na mwenye nguvu fulani tofauti na wanyamapori wengine.

Kakakuona mkubwa kuliko wote (Giant ground pangolin), Picha kutoka africanpangolin.org
Pichani ni aina tatu tofauti za kakakuona ambao wanapatikana Tanzania, kakakuona wa ardhini, kakakuona tumbo jeupe, na kakakuona mkubwa.

Pichani ni aina ya kakakuona ambao wanapatikana Tanzania, wa kwanza kutoka kushoto ni Kakakuona wa ardhini, wa kati ni Kakakuona tumbo jeupe, na wa mwisho ni kakakuona mkubwa.
Kakakuona ni miongoni mwa wanyama wenye taarifa haba hasa kuhusu idadi yake, maeneo yao muhimu, chakula wanachopendelea kula na changamoto zinazowakabili hasa kwa hapa Tanzania.
Kubwa zaidi, ni imani na tamaduni za jamii husika zinazohusishwa kwa mnyama huyu. Hivyo, kuna mengi hayajulikani kuhusu namna wanavyohusishwa kwenye mambo ya Imani, na ukweli wa mambo hayo kisayansi.
Ni miongoni mwa wanyamapori wenye matumizi makubwa, hasa ikidhaniwa kuwa viungo vya kakakuona vinaweza kuwa dawa, bahati, ulinzi dhidi ya mabaya, biashara, mapambo na chakula.
Pamoja na sababu nyingine kama kuharibika na kupotea kwa makazi yake ya asili, wanyama hawa wameingia katika orodha ya wanyama walio hatarini kutoweka duniani.
Sehemu nyingine duniani zenye wanyama hawa kama nchi za Asia, kakakuona wameripotiwa kupungua sana kwababu hizo.
Tafiti za biashara haramu za wanyamapori, zinaonyesha kupungua kwa kasi kwa kakakuona wa bara la Asia kumefanya wanunuzi na watumiaji wa kakakuona kuhamia kwa kakakuona wa Afirka. Soma makala hii kufahamu zaidi Kakakuona Wanaelekea Kutoweka Bila Kuwa na Taarifa Zake
Kwa sasa Afrika imekuwa ndio sehemu ya kupata kakakuona ambao wanasafirishwa kuuzwa kwenye nchi za Asia na badhi ya nchi za Ulaya.
Hivyo, nchi za Afrika zenye wanyama hawa zinakabiliwa na ujangili na biashara haramu ya kakakuona. Hali hii inapelekea wanyama hawa adimu kuendelea kupungua kwenye maeno yao. Soma hapa kufahamu zaidi Spishi za Kakakuona wa Tanzania, na Mengi Usiyoyajua kuhusu Wanyama Hawa
Taarifa kutoka vyombo vya usimamizi wa wanyamapori nchini Tanzania na sehemu nyingine Afrika, zinaripoti ukamataji wa kakakuona na magamba yake katika maeneo mbali mbali kama vile maeneo ya hifadhi, forodha, bandari, au katika viwanja vya ndege.
Ukamataji huu mkubwa unaashiria namna mahitaji ya wanyama hawa ulivyo mkubwa kwenye nchi za Asia na Ulaya.
Hii inaashiria kuwa kakakuona wa Afrika na Tanzania sio salama tena kutokana na kushamiri kwa biashara hii chafu.
Kwasababu ya uharamu wa biashara hii, wengi wanaofuatilia mambo haya wanahofia huenda kuna kiasi kikubwa cha ujangili na biashara hii vinafanywa bila kupata taarifa zake.
Operesheni nyingi za kufuatilia mambo haya ya biashara haramu zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Lakini kuna wasi wasi mwingi hasa kwa maeneo ya vijijini ambako wanyama hawa huonekana.
Hivyo ndugu msomaji wa makala hii, hiyo ni picha tu ndogo inayooshesha changamoto zinawakabili kakakuona sehemu nyingi duniani.
Wakati mwingine wanyama hawa wanatokea kwenye makazi ya watu, na hapo watu bila kujua wanawaua, kuwasababishia majeraha na wengine kuwatunza kwenye nyumba zao.
Kakakuona ni moja ya wanyama ambao ni rahisi kuumizwa, au kuathiriwa na changamoto kidogo tu. Mfano, endapo kakakuona akibebwa vibaya anaweza kupata majeraha. Soma zaidi makala hii..Mkutano wa Dharura Kijijini Uliomuokoa Kakakuona
Ni wanyama ambao wana aibu sana, hivyo hawawezi kula au kuwa huru mbele za watu wengi au kwenye kelele, hivyo ukimkamata kakakuona ni vizuri akarudishwa porini haraka.
Wengi wetu hatujui kakakuona wanakula nini, hivyo tunawapa vitu ambavyo hawawezi kula. Kakakuona wanakula mchwa na siafu. Hivyo kama kakakuona atapelekwa porini baada ya kukamatwa anatakiwa aachiwe sehemu yenye maji na vichuguu.
Ukimuona kakakuona katika mazingira yake ya asili kama porini, unaweza kumuacha huko huko aliko. Lakini akitokea kwenye makazi ya watu ni vizuri kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji au kwa watu wa Maliasili walio karibu ili waje kumsaidia.
Naamini, utakuwa balozi mwema wa uhifadhi wa kakakuona na wanyamapori wengine.
Watumie wengine makala hii wasome na kujifunza zaidi.
Imeandikwa na Hillary Mrosso, +255 683 862 481, hmconserve@gmail.com
Tunaandika makala hizi ili tuongeze uelewa wetu kuhusu wanyamapori, tunaamini tukipata uelewa tutachukua hatua kushiriki katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake asilia.Kazi hii tunafanya kwa kujitolea na hakuna malipo yoyote, endapo umefurahia kazi zetu unaweza kutuunga mkono kwa kiasi chochote ili tupate mtandao, vifaa vyua kufanyia kazi kama kamera na komputa. Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana kwa mawasiliano haya; hmconserve@gmail.com |+255-683-862-481