Ukiwa eneo la Ruaha kusikia sauti nzuri za ndege, fisi, nyani, simba, tembo na wanyama wengine ni jambo la kawaida sana. Pia sio jambo la kushangaa kusikia sauti za viboko wakicheza na kufurahia maji ya mto Ruaha Mkuu unaokatisha katika hifadhi ya taifa ya Ruaha.

Nilibahatika kufanya kazi za utafiti wa kanivora katika mradi wa Ruaha Carnivore, ambao kwa sasa umebadili jina na kuitwa Lion Landscape. Ni mradi ambao unafanya kazi nyingi za utafiti na uhifadhi katika vijiji vinavyozunguka hifadhi ya taifa ya Ruaha.

Pichani ni Hillary Mrosso mwandishi wa makala hii akitegua mitego ya waya iliyotegwa na majangili katika eneo la Ruaha.

Nikiwa katika mradi huu wa Lion Landscape, nilijifunza mambo mengi kuhusu wanyamapori hasa kanivora (kanivora ni wanyama wanaokula nyama) wakubwa kama vile simba, chui, duma, fisi na mbwa mwitu. Pamoja na mambo mengine, nilijifunza pia kuzitambua sauti zao.

Hivyo, nikisia sauti yoyote ya kanivora naweza kujua huyu ni fisi, simba, duma, chui au mbwa mwitu. Hata hivyo, kwasababu mradi huu ulikuwa vijijini, na vijiji vingi vilikuwa karibu na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na  Hifadhi ya Jamii ya MBOMIPA (WMA). Tuliona na kushuhudia aina nyingi za wanyamapori katika eneo hili.

Siku moja majira ya jioni, tulisikia sauti ambayo ilikuwa tofauti kabisa na sauti ambazo tumezoea kuzisikia mara kwa mara katika eneo hili. Ilikuwa ni sauti ya simba, lakini ilikuwa tafauti na siku nyingine, ilikuwa sauti ya simba dume ikiita na kulia tofauti kabisa.

Haikuwa sauti ya kuita familia yake kwenda mawindoni, haikuwa sauti ya kutishia simba na wanyama wengine wasiingie katika himaya yake, haikuwa sauti ya kuita jike wala haikua sauti ya kuita watoto wake; ilikuwa ni sauti iliyojaa uchungu na maumivu, ikiomba msaada.

Picha hii ikionyesha athari za mitego ya waya kwa wanyama, huyu simba amefia hapo akiwa anapigania uhai wake kutoka kwenye mtego huo mbaya.

Ilikuwa ni sauti kama ya mnayama anayeelekea kukata roho, ilikuwa ni sauti ya dhiki kuu, ilikuwa ni sauti ya mnyama anayepigania pumzi yake ya mwisho baada ya kunyongwa au kupatwa na kifo cha mateso. Ilikuwa ni sauti ya dhiki iliyokuwa ikiomba msaada wa haraka.

Tulihisi simba yule amekamata nyati au tandala, lakini tulipoona suti inazidi kuwa kubwa, tuliwasha gari kwenda eneo la tukio umbali wa kilomita kama 8 kutoka ilipo kempu yetu. Tulifika tukaona simba dume katikati ya miti miwili akipigania uhai wake baada ya kunaswa na waya wa chuma. Ndio zilikuwa ni nyaya ngumu za chuma zilizoishika shingo ya simba yule kiasi cha kutaka kuikata ile shingo ya simba.

Wanya wa chuma uliokuwa umeishika shingo ya simba yule, ulimsababishia maumivu na mateso makali sana, ambayo ilipelekea simba yule kuita kwa sauti tofauti, ilikuwa ni sauti ya dhiki  ikiomba msaada wa mapema.

Masikini simba yule, alikuwa mzuri, amejaa masharubu yake, alikuwa na nguvu na afya tele, lakini  yupo katika dakika za mwisho za uhai wake. Mayoya yake mazuri yalikuwa yamejaa damu na majeraha mengi na michubuko mengi, damu nyingi ilikuwa imemwagika chini, zile waya za chuma zilikuwa kama zimeichinja shingo ya simba, ni kifo kibaya na cha huzuni kweli.

Picha hii ikionyesha simba alivyojeruhiwa na mitego ya waya za chuma; PIcha kutoka – Naturinda – Queen Elizabeth National Park, Uganda, WCS, LRF

Nilitamani nishuke kwenye gari nikamuokoe, kumbe ndio alikuwa anaelekea kukata roho na kuhema kwa nguvu; wenzangu niliokuwa nao walisema ni hatari kushuka kwenye gari katika mazingira yale. Hivyo, nilibaki tu namuangalia yule simba.  Macho yake makubwa yalibakia yakituangalia sisi tukiwa juu ya gari letu, hatuna cha kufanya, alikata roho, alifia kwenye mtego wa waya za chuma uliotegwa na majangili. Iliniuma sana, machozi yalinitoka.

Tangu siku ile niliichukia sana ujangili, hasa huu wa kutumia mitego ya waya; ujangili na kuuwa wanyama kwa aina hii ya mitego inawasababishia wanyama mateso na maumivu makubwa sana kabla ya kufa. Katika sheria ya uhifadhi na usimamizi wa wanaymapori, imeweka wazi kuwa hutakiwi kumsababishia mnyama maumivu, majeraha au mateso wakati wa kuwinda na wakati wa kumsafirisha kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

Nakumbuka tukiwa Chuo Kikuu tulisoma moja ya njia ambazo majangili hutumia kuwinda wanyamapori, tulisoma kidogo kuhusu mitego “snares” sikujua madhara ya mitego hii hadi nilipoona kwa macho yangu, mnayama mzuri kama simba anakata roho mbele yetu, na macho yake makubwa yalitungalia kama ishara ya kumba msaada ambao hakuupata.

Athari za mitego ya waya kwa wanyamapori, picha na Lucy Laing, Kwa maelezo na taarifa zaidi unaweza kusoma hapa Lion with poacher’s wire around neck in Tanzania | Daily Mail Online

Wale watafiti wenzangu wa mambo ya simba walisikitika pia, wakasema huyu simba atakuwa na umri wa miaka kama 4-5 hivi, ni umri ambao simba dume anategemewa na familia yake kwa ulinzi, kutafuta chakula na kuzalisha majike yaliyo kwenye himaya yake. Ikumbukwe kuwa, simba ni wanyama wanaoishi kama familia, familia ya simba inaweza kuwa na simba kuanzia 3 hadi 30 na zaidi. Hapo kuna mchanganyiko wa watoto, majike na dume mkubwa, ambaye ndio mlinzi mkuu wa familia hiyo.

Nikawaza sana, kama huyu simba alikuwa ndio baba wa familia ina maana familia yake sasa haina tena ulinzi, watoto wake watauwawa na fisi na wanyama wengine huko nyikani, nikawaza sana kama huyu simba ndio alikuwa anategemewa katika kuwinda na kulisha familia ina maana familia yake itatawanyika, watoto wanaweza kufa, na kupelekea idadi yao kupungua sana.

Duniani kote, idadi ya simba ni ndogo sana,  changamoto inayopelekea kupungua kwao ni pamoja na kuuwawa kikatili kama kutega mitego ya waya za chuma, kuwekewa sumu, uharibifu wa mazingira yao, uwindaji kwa ajili ya nyara na changamoto nyingine za migogoro ya wanyama hawa na wafugaji. Unaweza kusoma zaidi kuhusu simba hapa; Mambo Themanini Na Tano (85) Usiyoyajua Kuhusu Maisha Ya Simba, Kifo Cha Simba Aliyeitwa Cecil Na Hatima Ya Uhifadhi Wa Simba Barani Afrika

Pamoja na dunia kuwa na idadi ndogo ya simba, inakadiriwa kuwa, asilimia 10 ya simba wote duniani wapo katika eneo la hifadhi ya Ruaha. Hifadhi ya taifa ya Ruaha ni moja ya eneo muhimu sana kwa uhifadhi duniani kutokana na uwepo wa wanyamapori wengi, hasa simba. Lakini bahati mbaya simba wengi wanakufa kwa mitego ya waya, sumu, ujangili nk.

Kutokana na umuhimu wa eneo hili kwa uhifadhi, watafiti wameanza kufika katika eneo hili kwa ajili ya kuweka program mbali mbali za utafiti na uhifadhi, mfano mzuri ni mradi wa Lion Landscape, Wildlife connection, Southern Tanzania Elephant Project (STEP)  na miradi mingine ambayo wamejikita kufanya tafiti na uhifadhi wa wanyamapori pamoja na maeneo yao ya asili. Kutokana na  juhudi kubwa za uhifadhi, hasa uhifadhi wa kanivora, idadi kubwa ya vifo vya simba imepungua sana.

Kwingineko hifadhini, wanyama wetu hawapo salama, kuna sauti nyingi za dhiki kwa wanyamapori, sio simba tu, bali hata wanyamapori wengine kama swala, nyati, fisi, pundamilia, tembo.nk

Baada ya kuona ukatili ule kwa yule simba, niliwaza sana kwanini wamuue huyu simba? Kwanza haliwi kama kitoweo, basi tu yani. Wale watafiti wenzangu waliniambia wategaji wa mitego hii hawakutega ili wamnase simba, walitega ili wanase wanyama wengine kama tandala, swala, dikidiki, pofu, nyati maana ndio wanyama ambao huliwa sana kama nyamapori katika eneo hili.

Mitego hii ya waya, haichagui mnyama wa kumkamata, inakamata mnyama yeyote atakayepita kwenye mtego huo. Baada ya hapo, nilitaka kujua madhara ya mitego hii ipoje, nilisoma tafiti nyingi kuhusu mitego ya nyaya, nilisoma kuanzai tafiti zilizofanya Asia hadi Afrika na Tanzania. Nilishangaa sana kuona ni janga kubwa sana kwa wanyamapori.

Mitego ya nyaya au waya, ni njia mbaya sana inayotumika kuwindia wanyamapori, njia hii imesababisha wanyamapori wengi kuuwawa, kuwa na vilema, makovu, vidonda, kupoteza meno, masikio, pembe,  na miguu.

Picha hii inaonyesha madhara ya mitego ya waya za chuma yalivyosababisha kilema na majeraha kwa simba huyu; Picha hii imechukuliwa kutoka, the Snares to Wares Initiative

Hata hifadhi ya taifa ya Nyerere, ambayo ilikuwa ni sehemu ya Pori la Akiba la Selous,  pamoja na ukubwa wake na umaarufu wake duniani; bado kunasika kilio na sauti ya dhiki kwa wanyama wetu,  inakabiliwa na changamoto za mitego ya waya ambayo hutegwa kukamata wanyamapori.

Nilishangaa kuona hata Hifadhi ya Serengeti pamoja na umaarufu wake duniani kote; bado inasumbuliwa na uwepo wa mitego hii ya waya. Mitego hii imetegwa kwenye njia za wanyama. Bila kujali ni mnyama gani atapita kwenye mitego hiyo, mitego hii haichagua mnyama wa kumkamata, inakamata wakubwa kwa wadogo, inakamata majike inakamata madume.

Mitego hii ni rahisi kupatikana, na pia ni rahisi kutega; kwenye maeneo mengi ya vijijini mitego hii hupatikana, inaweza kuwa ni mabaki ya nyaya za umeme, spoku za baiskeli, na nyaya nyingine ambazo hupatikana kiurahisi kwenye maeneo ya vijijini.

Urahisi wa kutumia mitego hii unatokana na kwamba mtegaji akishatega anaondoka eneo hilo, hivyo sio rahisi kukamatwa na askari wanaofanya doria. Pia mitego hii sio rahisi kuonekana pale inapotegwa, hii hufanya hata askari wanaofanya doria kushindwa kugundua au kuona mitego hiyo.

Mfano, Profesa  Alfani Rija, wa Chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine,  aliwahi kufanya jaribio moja muhimu sana katika moja ya tafiti zake alizofanya katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti mwaka 2016. Katika utafiti wake alitega mitego feki au mitego bandia 2316, lego lake ilikuwa kupima uwezo wa askari wa wanyamapori kubaini mitego hiyo aliyoitega maeneo mbali mbali ndani ya hifadhi ya taifa ya Serengeti. Matokeo ya jaribio la utafiti wake ulibaini kuwa uwezo wa askari kutambua mitego inayotegwa na majangili ni mdogo sana. Unaweza kusoma zaidi kazi yake hapa; Improving Efficiency of Ranger Patrols in Detecting and Preventing Poaching in Serengeti National Park and Adjacent Reserves.

Kutokana na utafiti huu, inatuonyesha kuwa mitego inayotegwa na majangili kwa ajili ya kukamata wanyamapori ni ngumu kugunduliwa na askari wanaofanya doria, kwasababu inafanana na mazingira ya maeneo inapotegwa. Lakini pia maeneo ambapo mitego hii hutegwa ni ngumu kwa askari wa wanyamapori kufika, hii inaweza kusababishwa na uhaba wa askari au vitendea kazi.

Utafiti wa hivi karibuni (2023) uliofanywa na Sarah Benhaiem katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti ulibaini kuwa moja ya madhara makubwa yanayowapata wanyama wanaokamatwa kwenye mitego ya waya ni kupunguza uwezo wao wa kuzaliana. Sarah, alibainisha kuwa wanyama jamii ya fisi ambao ndio waathirika wakubwa wa kunaswa kwenye mitego hiyo inayotegwa na majangili inapelekea wanyama hao kushindwa kuzaliana kama kawaida.

Katika utafiti wake, Sarah alisema kuwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inakabiliwa na changamoto kubwa ya ujangili kwa njia ya mitego ya nyaya, mitego hiyo hutegwa kwenye njia za wanyamapori hasa kipindi ambacho wanyama wana hama kutoka eneo moja kwenda eneo jingine. Mfano wanayamapori jamii ya nyumbu kwenye misafara ya kuhama.

Wanyama wanaokula nyama kama vile fisi, huwa wanapenda kufuata njia za wanyamapori ili wapate mawindo yao, katika harakati hizo nao hujikuta wamenaswa kwenye mitego hiyo inayotegwa kwenye njia za wanyamapori, kama vile nyumbu, pundamilia nk.

Mitego hii sio tu inasababisha vilema na vifo kwa wanyamapori, lakini pia imekuwa ni chanzo cha kuenea kwa magonjwa kwa wanyamapori. Mitego hiyo huwa inatumika kunasa wanyama wa aina mbali mbali, hivyo mnyama anaweza kunaswa akiwa ni mgonjwa na kusambaza magonjwa hayo wa wanyama wengine ambao watanaswa kwenye mitego hiyo.

Hata hivyo, mamlaka za uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori zinafanya kazi kubwa sana ya kutoa mitego kwenye maeneo yote yanayokisiwa mapitio ya wanyamapori. Mfano hifadhi ya taifa ya Seregeti kuna program maalumu ya kutoa mitego ya waya hifadhini. Pia nimeona mashirika makubwa kama Frankufurt Zoological Society wakishirikiana na hifadhi ya taifa ya Serengeti kutoa mitego ya waya hifadhini. Jambo hili ni kubwa na linatakiwa kuungwa mkono na serekali na jamii kwa ujumla.

Picha hii ikionyesha mitego ya waya za chuma iliyotelewa na askari wa wanyamapori, kwa kushirikiana na FZS. Katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti

Jamii, hasa zinaoshi kando ya hifadhi za wanyamapori zinatakiwa kuachana na shughuli za utegeji mitego kwenye maeneo ya wanyamapori, kwasababu hasara yake ni kubwa, kwa taifa linapoteza mamilioni ya fedha kuondoa mitego ya waya, lakini njia ya kikatili ya uwindaji maana inaua na wanyama wasiolengwa na mtegaji wa mitego. Kwa ujumla wake, ujangili wa aina yoyote ule ni kinyume na sheria.

Asante kwa kusoma makala hii, naamini umepata ujumbe muhimu, na pia utawashirikisha wengine makala hii ili wajifunze na wawe msitari wa mbele kupiga vita ujangili, hasa wa mitego ya waya.

Imeandikwa na; Hillary Mrosso, +255 683 862 481; hmconserve@gmail.com